Suzana: Biashara ninayoifanya imewapunguzia mzigo wazazi

Suzana: Biashara ninayoifanya imewapunguzia mzigo wazazi

Kama mnavyofahamu kahawa ni kinywaji maarufu na kinachopendwa na watu wengi na imekuwa ni zao mashuhuri la kibiashara duniani kwa muda mrefu.

Kwa hakika umaarufu na kupendwa kwa kinywaji hiki unatokana na manufaa kadhaa yanayopatikana ndani ya kinywaji hicho.

Hata hivyo leo kupitia makala hii tunaona jinsi ambavyo kijana mwenye umri wa miaka 22 alivyoibadilisha kahama na kuwa biashara kwake inayomuingizia fedha za kujikumu awapo chuoni.

Mwanadada huyu mrembo amenivutia hata mimi kuweza kufikiria ni zao gani jinyine maarufu hapa duniani linaweza kutumika kama uzalishaji wa bidhaa nyingine kwa manufaa ya jamii.

Hapa tunamzungumzia Suzana Kaijage ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambaye yeye ameamua kulitumia zao hilo la kahawa kutengenezea scrabu ya asili inayoondoa upele na chunusi usoni.

Kaijage ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho akichukua kozi ya Masoko na Rasilimali Watu anasema ameamua kufanya baishara hiyo ya kutengeneza na  kuuza scrabu kwa wanafunzi wenzake hapo chuoni na mtaani ili kuweza kuwapunguzia majukumu wazazi wake.

“Kiukweli biashara hii ya scrabu imenifanya nipate fedha za kujikimu hapa chuoni, nimeacha kabisa kumwambia mzazi mahitaji yangu madogo madogo kama sabuni, marashi na taulo za kike za kujisiri wakati wa hedhi,” anasema.

Anasema kwa sasa wazazi wake wamekuwa wakimlipia ada ya chuo lakini wamekuwa wakifurahi kumuona akifanya biashara na kujipatia fedha za kuweza kujikimu mahitaji yake mengine.

“Kiukweli wakati naanza sikutegemea kama scrabu hii ya kahawa ingeweza kunipatia fedha na kunifanya kufikiria kufanya vitu vikubwa zaidi,” anasema. 

Hata hivyo anasema kupitia biashara yake hiyo ameamini vitu vya asili vina nguvu kubwa kwani kila kukicha wateja wake wamekuwa wakimpatia ripoti juu ya matatizo yao ya ngozi kutibika na scrabu yake.

“Kama tunavyojua sasa hivi watu wengi ni wahanga wa ngozi na hiyo ni kutokana na kutumia vipodozi vyenye kemikali hivyo scrabu hii ni kama mkombozi kwao,” anasema.

Kaijage anasisitiza kuwa yeye ni miongoni mwa wanafunzi ambao wanapenda kujishughulisha kwa kufanya bishara licha ya kusoma.

Safari yake ya biashara ilivyoanza…

Anasema safari yake ya biashara ilianza kwa yeye kupenda masuala ya urembo hasa ule wa kutumia vitu vya asili na si wa kisasa unaotumia kemikali ambazo baadaye huweza kuleta madhara katika ngozi.

Kaijage anasema wakati anapenda mambo hayo ya urembo aliwaza kuanzisha sabuni zake za asili ambazo ataweza kuziuza kwa wanafunzi wenzake chuoni na mtaani pia.

“Wazo likatimia wakati wa kufundishwa sasa namna ya kutengeneza huenda huyo aliyenifundisha alikosea au mimi nilisahau maana nilifanikiwa kununua kila kitu ninachopaswa kuwa nacho ili kuweza kutengeneza sabuni lakini cha kushangaza baada ya kuvichanganya hakuna kitu chochote kilichotokea.

“Niliumia sana maana nilipata hasara kutokana na kununua baadhi ya vitu, ila sikukata tamaa nilirudia kwa mara ya pili napo nikashindwa mpaka pale nilipoangalia kipindi cha ujasiriamali katika moja ya televisheni ambapo mjasirimali alitaja kemikali zinazotakiwa kuchangwa katika sabuni,” anasema.

Anasema baada ya kuziona na kujua majina ya kemikali zinazotakiwa kuchangwa katika sabuni akakumbuka kuwa wakati anafanya mchanganyo kipindi cha nyuma alikuwa akikosea.

Pia, anasema kabla ya kuamua kufanya biashara hiyo ya sabuni na sasa scrabu, alishawahi kuuza sidiria za wanawake, baishara ambayo ilimfanya awe na fedha lakini wateja wakawa wanapungua.

“Wateja wangu walipungua kutokana na kwamba ilifika mahali wanazo sidiria zaidi ya tano hivyo wala hawakuwa na haja ya kununua zingine, nilichanganya akili mpaka likaja hilo wazo la kutengeneza scrabu ya kike hiyo inayotengenezwa kwa kahawa na mafuta ya nazi.

“Kabla zijaisambaza nilianza kuitumia mwenyewe na ikaleta matokeo mazuri kwani vipele na makovu yaliyokuwepo usoni mwangu yaliondoka,” anasema na kuongeza

“Nashukuru Mungu kwani hadi mama yangu aliponiona nipo vizuri usoni akawa ananisifia na kuomba na yeye nimpatie ili aweze kuitumia,” anasema.

Jinsi anavyotenga muda wa masomo, biashara

Anasema amekuwa akitenga muda wa kujisomea na kutengeneza scrabu hizo ambazo akimaliza utakiwa kuziuza mtaani na kwa wanafunzi wenzake.

“Kila kitu ni mipango ili nisije kufeli darasani nimehakikisha kuwa nina ratiba maalum ya utengenezaji wa scrabu zangu ambayo haiingiliani kabisa na ratiba ya masomo chuoni,” anasema.

Matarajio

Anasema matarajio yake ya baadaye ni kuja kuwa na kampuni kubwa ya urembo itakayotoa mafunzo na ajira kwa vijana mbalimbali.

“Nataka kuwa na kampuni itakayojulikana kwa jina la Pinky, najua itakuwa kuwa moja ya kampuni kubwa ambayo itaweza kutengeneza vitu mbalimbali vya urembo vya asili vitakavyowasaidia watu kutibu matatizo yao ya ngozi,” anasema.

Kaijage ametoa wito kwa vijana hasa waliopo chuoni kufikiria kufanya biashara mtaani pindi watakapomaliza masomo yao.

“Wanafikiri watapataje fedha za kufanya biashara hiyo maana natambua kuwa wapo wanaosoma kwa mikopo hivyo wanapaswa kuzitumia fedha hizo kwa uaminifu mkubwa maana wakifanya hivyo wanaweza kujikuta wanamaliza chuo wakiwa wamepata mtaji,” anasema.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post