sehemu 12: simulizi

sehemu 12: simulizi

Innocent Ndayanse

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani lililivalia njuga suala la mauaji ya Waarabu watatu, Nassor Khalfan na wenzake. Jambo la kwanza baada ya kupata taarifa ya tukio hilo, walimchukua mtoto Abdul hadi kituo cha Polisi. Huko, askari wa kitengo cha upelelezi, Maftah na Chopa wakachukua maelezo yake.

“Unaitwa nani?” Maftah alimhoji.

“Abdul.”

Umri wako?”

Abdul alifikiri kidogo kisha akasema, “Sijui.”

Maftah na Chopa walitazamana. Hatimaye  Maftah akayarejesha macho kwa mtoto Abdul na kuendelea, “Unasoma?”

“Ndiyo.”

“Uko darasa la ngapi?”

“La nne.”

Chopa na Maftah walitazamana tena. Chopa akasema, “Hatazidi miaka kumi na miwili.”

“Yeah. Ni kati ya kumi na kumi na miwili,” Maftah aliongeza.

Maftah akamgeukia tena mtoto Abdul. “Leo ulikuwepo nyumbani tangu asubuhi?”

“Ndiyo.”

“Hukwenda shuleni?”

“Sikwenda.”

“Kwa nini?”

Abdul hakujibu.

“Tangu asubuhi marehemu baba yako hakuwa ametoka nyumbani?”

“Hakutoka.”

“Alikuwa na shughuli gani tangu alipoamka?”

“Alikuwa akiangalia tivii.”

“Mama yako alikuwa wapi?”

“Mama hayupo.”

“Yuko wapi?”

“S’jui.”

“Hayupo kwa siku nyingi?”

“Ndiyo.”

“Wakati baba yako anaangalia tivii unaweza kuwakumbuka wageni wa kwanza waliokuja nyumbani?”

“Ndiyo.”

“Walikuwa ni akina nani?”

Abdul alifikiri kidogo kisha akasema, “Ni wale rafiki zake wawili.”

“Wale waliokuwa pamoja naye wakati walipovamiwa?”

“Ndiyo.”

“Na wale unaosema kuwa ndio waliowavamia walikuja saa ngapi?”

Abdul alitulia kidogo, akatazama sakafuni kisha akasema, “S’jui.”

Chopa akasema, “Hilo si tatizo. Hebu tuambie, hao wavamizi walipokuja ni nani aliyewapokea mlangoni?”

 

“Mimi.”

“Walikwambiaje?”

“Eti wao ni wageni wa baba, wametoka Dar.”

“Halafu?”

“Halafu baba akatokea na kuwakaribisha.”

“Baba yako alikuwa akiwafahamu?”

“Ndiyo.”

“Na walipoingia walipiga risasi moja kwa moja au waliongea kwanza na baba yako?”

“Waliongea kwanza na baba.”

“Wakati wanaongea wewe ulikuwa wapi?”

“Chumbani.”

“Kwa hiyo hukuyasikia maongezi yao, eti Abdul?”

“Niliyasikia. Mlango wa chumba ulikuwa wazi.”

Chopa na Maftah wakatazamana tena kisha wakamkazia macho mtoto Abdul.

“Walikuwa wakizungumza kuhusu nini?” Chopa aliendelea kumwaga maswali.

“Gari. Walikuwa wakitaka baba awape pesa ili wamwachie gari.”

“Yaani walikuwa wakiuza gari?”

“Ndiyo.”

“Hilo gari walikuwa wamekuja nalo? 

“Ndiyo.” 

“Uliliona?”

“Ndiyo, nililiona.”

“Hebu njoo,” afande Chopa alimtoa nje Abdul. Huko kulikuwa na magari ya aina mbalimbali. “Kuna gari lolote hapa ambalo unaweza kulifananisha na lile gari walilokujanalo hao wageni?” alimuuliza.

Abdul alitazama huku na kule kisha akasema, “Ni kama lile, na lile… na lile… na lile…” Alimwonyesha magari manne, meupe aina ya Toyota Mark 11 ambayo yalikuwa yameegeshwa, yakiwa yamechanganyika na magari mengine.

Wakarudi ndani.

“Nadhani kuna haja ya kumwonyesha picha za wahalifu sugu tulizonazo,” Chopa alimwambia Maftah.

Dakika chache baadaye majalada kadhaa ya wahalifu sugu yalikuwa mbele yao sanjari na picha zao. Baadhi ya wahalifu hao walikuwa wakitumikia vifungo magerezani, baadhi walikwishakufa, baadhi walikuwa rumande kesi zao zikiunguruma na wengine walikwishamaliza vifungo.

Hawakutaka kubagua picha za kumwonyesha Abdul, waliamua kumwachia kazi ya kuzitazama na kuzipambanua mwenyewe kabla ya hatua itakayofuata.

“Abdul, ni wewe uliyewakaribisha hao wageni ndani,” Chopa alimwambia. “Kwa hali hiyo kwa vyovyote ulipata muda mzuri wa kuweza kuwatazama. Kama ikitokea ghafla mmojawao au wote wakitokea hapa unaweza kuwakumbuka?”

“Ndiyo.”

“Una hakika?” Maftah alimtazama Abdul kwa makini.

“Ndiyo! Nitawakumbuka vizuri!” Abdul alijibu kwa msisitizo.

Ni hapo rundo la picha kumi na tatu lilipomwagwa mbele yake.

“Kazi kwako,” Chopa alimwambia. “ Zitazame kwa makini picha hizi

Kama utaiona picha yoyote ambayo unaitilia shaka kuwa inafanana na mmoja wa wale wavamizi, iweke pembeni.”

Mtoto Abdul aliingia kazini. Akaitazama picha moja baada ya nyingine kwa utulivu. Mara macho yakaganda kwenye picha moja. Akaikodolea macho picha hiyo bila ya kupepesa. Hatimaye akaiweka kando na kuendelea kuzichunguza picha nyingine.

Alipozimaliza, akairudia picha ile aliyoiweka pembeni. Kwa mara nyingine akaikodolea macho kwa makini. Kisha akampatia Chopa.

Ilikuwa ni picha ya mmoja wa majambazi sugu wenye rekodi mbaya katika Jeshi la Polisi. Aliitwa Kipanga Sukasuka. Rekodi yake ilionesha kuwa kiasi cha miaka  kumi iliyopita, Kipanga alihukumiwa jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu. Lakini rekodi hizohizo hazikuweka bayana kuwa Kipanga alikwishamaliza kifungo hicho.

Picha hiyo ilimwonesha Kipanga akiwa amevaa suruali aina ya jeans, raba miguuni na fulana kubwa yenye picha ya mcheza sinema maarufu wa Marekani. Macho yake yalikuwa makali, yaking’ara ukatili ilhali kichwani upara ukitawala.

“Kwa nini umeichagua picha hii?” Chopa alimhoji mtoto Abdul.

Abdul alikumbwa na kigugumizi.

Maftah akamwahi, “Vipi, Abdul, huyu mtu ni mmoja wa wale uliowafungulia?”

“Ndiyo.”

“Ni huyu pekee? Si umesema uliwafungulia wawili?”

“Ndiyo, niliwafungulia wawili.”

“Sasa mbona umeichagua picha moja tu?” Chopa alimuuliza.

 

Itaendelea……………….

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post