Hii hapa sababu ya kifo cha King Kikii

Hii hapa sababu ya kifo cha King Kikii

Joseph Silumbe ambaye ni mtoto wa marehemu msanii mkongwe wa muziki wa dansi Tanzania, Boniface Kikumbi maarufu 'King Kikii' amesema baba yake amefariki kwa maradhi ya saratani ya ini.

Joseph amesema hayo leo Ijumaa Novemba 15, 2024 wakati akizungumza na Wasafi Radio.

"Ana miaka kama mitano, sita alikuwa anaugua, mara ya kwanza alifanyiwa upasuaji wa pingili za mgongo hapa shingoni baada ya hapo tukampeleka India na nilikuwa nae mimi mwenyewe, tulikaa mwezi mmoja. Wakamuwekea pampu moja ya kujisaidia kwa sababu alikuwa kama amepooza miguu na mikono ilikuwa haifanyi kazi baada ya hiyo oparesheni.

"Baada ya kurudi hapa (nchini) akawa amedhohofika kidogo hivi karibuni tukamrudisha hospitali walivyofanya vipimo wakagundua tezi dume imerudi tena ikawa imeongezea na saratani ya ini,"amesema Joseph

Hata hivyo mtoto huyo wa marehemu amesema baba yake alitolewa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) siku tatu zilizopita na kurudishwa nyumbani.

"Mzee alifariki usiku wa kuamkia leo ilikuwa saa 7.10 tulikuwa nyumbani mimi, mama, Jesca na ndugu wengine tumemaliza kula, ikawa ngumu yeye kula baada ya hapo hali ikabadilika ghafla. Awali alikuwa Muhimbili kwa takribani wiki mbili baada ya hapo tukaomba ruhusa kurudi nyumbani ilikuwa siku tatu zilizopita,"amesema Joseph

King Kiki ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 77, enzi za uhai wake alitamba na vibao mbalimbali kikiwemo maarufu cha ‘Kitambaa Cheupe’. Kwa mujibu wa mtoto wake msiba upo nyumbani kwake Mtoni Kwa Azizi Ally.

Kutokana na msiba huo Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa asubuhi ya leo Novemba 15 kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram alitoa salamu za pole.

“Lala salama mzee wetu Boniface Kikumbi Mwanza Mpango (King Kikii), mwanamuziki mkongwe, jabali la rhumba na mtu mwenye utumishi uliotukuka katika tasnia ya muziki Tanzania.

“Tutauenzi mchango wako mkubwa katika muziki wa dansi Tanzania. Kwa miaka mingi umeburudisha, umefundisha, umeelimisha na uliipenda sana Tanzania,” ameandika Msigwa.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags