Mocco Genius anavyoifanya Bongo Fleva anavyotaka

Mocco Genius anavyoifanya Bongo Fleva anavyotaka

Wengi walianza kumtambua Idd Mohamed maarufu kwa jina la Mocco Genius kama mzalishaji muziki, lakini baadaye akaingia kwenye soko la uimbaji.

Mocco Genius aliyeanza kazi ya uzalishaji muziki mwaka 2007 kisha 2022 akaigia kwenye uimbaji, amesema alikuwa na ndoto ya kuwa mwimbaji kabla ya kufanya kazi ya uzalishaji muziki.

“Kuimba ilikuwa ‘passion’ yangu ya kwanza kabla ya kuwa mtayarishaj, ‘producertion’ ilikuja kipindi naanza masuala ya muziki, nilikuwa bado mdogo na sikuwa naweza ku-afford zile gharama za production kama kumlipa ‘producer’ na vitu vingine kama video, kwa hiyo nilijikuta naanza kwa kujitengenezea beat mwenyewe, kipindi nimeanza kufanya hivyo nikaona ni kitu ambacho nakipenda na nimekizoea,” amesema na kuongeza.

“Nikaanza kuona production inanipa pesa kwa sababu watu walikuwa wanakuja na kutaka kufanyiwa kazi na mimi, kwa hiyo muda huo nikajikita huko nikaona haina haja ya kuchanganya vitu viwili kwa wakati mmoja.”

Hata hivyo, Mocco Genius amesema mwaka 2022 aliingia kwenye muziki baada ya kutamani watu wafahamu uwezo wake kwenye kuimba na kuandika.

“Nilikuwa natamani watu wasikie nilichonacho katika uimbaji na kama ninaweza kuandika pia kwa hiyo sikuwa nimepanga moja kwa moja nikiingia kwenye uimbaji nifanye kazi na msanii gani ili kitu changu kiende.

“Lakini namshukuru Mungu kwa sababu kazi yangu ya kwanza nilifanya remix na Alikiba katika wimbo wangu wa ‘Napendwa’ kadri siku zilivyoenda nikajikuta nafanya kazi na Nandy, Marioo nikarudia wimbo na Alikiba,” amesema.

Licha ya kuwa kwa sasa amefanya muziki aina ya Kompa, mwanamuziki huyo amesema ana mpango wa kufanya muziki wa kila aina duniani.

“Mimi nawaza kufanya muziki wa kila aina, kwa mfano sasa hivi kwenye 'library' yangu nina nyimbo nyingi za miondoko ya Kihindi, Amapiano na Kompa lakini uzuri ni kwamba nilivyofanya kompa mashabiki wameipokea vizuri na siwezi kuwanyima kitu ambacho wanakipenda ndiyo maana najitahidi sana kuwa wa pekee,” amesema.

Hata hivyo hakuacha kufunguka changamoto zinazoikumba sanaa ya muziki nchini.

“Sanaa ya muziki ina changamoto na ndiyo maana kuna watu wanashindwa kuendelea sana zinawakuta watoto wa kike ambao wanaona hawawezi kusimama wao wenyewe, tofauti na sisi wanaume,” amesema Mocco.

Kati ya changamoto hizo amesema ndiyo sababu ya wasanii wa kike kuwa wachache hapa nchini.

“Baadhi ya wasanii wamekuwa wakiishia kati kwa sababu kuna tatizo la kuweka jinsia mbele badala ya kufanya kazi, kunaweza kutokea kitu cha kawaida ambacho hata mwanaume anafanyiwa ila akifanyiwa msanii wa kike anaweza kujitafsiri kwa sababu yeye mwanamke, msanii wa kiume anaweza akaingia studio akafanya vibaya tukamsema akakiri kuwa atajirekebisha lakini wa kike ukimwambia umezingua anasusa,” amesema.

Mocco mpaka sasa amefanya wimbo kama Mchuchu, Mi Nawe, Napendwa, Amenishika, Single, Nikilala, Hello na Mar Gaya.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post