Johari awacharukia wasioamini ushindi wake, Tuzo za MVAA

Johari awacharukia wasioamini ushindi wake, Tuzo za MVAA

Mwigizaji na mkurugenzi wa kampuni ya ‘Empire Lokoma’ Johari Chagula mapema wiki hii ameinua bendera ya Tanzania nchini Nigeria kwa kuondoka na tuzo mbili za The MVAA zilizokuwa zikitolewa nchini humo.

Johari ambaye ameshinda tuzo hizo katika vipengele viwili Best MVAA Actress Of The Year’ na ‘Best Series Of The Year’ kupitia series ya Wimbi alianza safari yake kwenye sanaa kupitia kundi ‘Kaole Sanaa Group’ huku akitamba na filamu kama ‘Sikitiko Langu’, ‘Johari 1&2’, ‘Mke Mchafu’ nk.

Baada ya kutua nchini na tuzo zake ameiambia Mwananchi Scoop kuwa hafurahishwi na baadhi ya mashabiki wasiokubaliana na ushindi wake

“Kwanza kabisa napenda kuwaambia kwamba mimi nimestahili kupata tuzo hizo na waliotoa tuzo wana akili zao timamu wameweza kuangalia vigezo tofauti na watu walikuwa ni wengi, lakini niliweza kushinda kwa hiyo ninaweza kusema kwamba kupata hiyo tuzo ni haki yangu.

“Nataka kuwaambia kuwa tusikae tu tukaangalia hapa, tuangalie historia kidogo ya mtu sidhani kama watoa tuzo wote wanaangalia machoni, wanaangalia huyu amefanya nini na kwa muda gani kupata hiyo tuzo ni haki yangu nimeshukuru na nimefurahi na nadhani itanipa changamoto ya kuendelea kufanya hii kazi,” amesema Johari.

Hata hivyo, amesema kigezo kikubwa kilichoangaliwa hadi kushinda tuzo ni ufanisi wake wa kazi.

“Kwanza wameangalia ufanisi wa kazi, pili wameangalia kazi mbalimbali ambazo nimeweza kuvaa uhusika unavyotakiwa kwa kila kazi ninayoifanya toka nimeanza sanaa mpaka sasa, nina takribani miaka 23 kwenye hii tasnia.

“Wanakuchunguza kuanzia mwanzo wa sanaa yako, maendeleo, safari yako ya sanaa ikoje kwa hiyo sidhani kama kuna kazi yangu hata moja ambayo sijavaa uhusika,” ameongezea Johari.

Kama wasemavyo wahenga mkaa bure si sawa na mtembea bure mwigizaji huyu hakuishia hapo ameeleza kuwa hakuna utofauti mkubwa unaofanyika katika kazi za Nigeria na Tanzania lakini changamoto kubwa hapa nchini ni soko.

Hivyo basi amewataka wawekezaji kuwekeza kwenye sanaa ya uigizaji kwani masoko yamekuwa machache na ndiyo maana wasanii na filamu hawatambuliki.

“Cha kwanza ninachowashauri wasanii wenzangu kwamba tuichukulie hii tasnia kama kazi, unajua ukikithamini kitu chako ambacho unakifanya na chenyewe kitakuthamini, wasiichukulie poa kwa sababu hii tasnia tulipoitoa ni mbali sana,” amesema Johari.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags