Mfahamu mwanamke wa kwanza kuwa waziri wa ulinzi Tanzania

Mfahamu mwanamke wa kwanza kuwa waziri wa ulinzi Tanzania

September mwaka jana Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri.

Miongoni mwa sura mpya katika baraza hilo la mawaziri, ni mbunge aliyemteua Dk. Stergomena Tax ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa nchini Tanzania.

Dokta Stergomena Tax ni nani?

Dk Stergomena ambaye alizaliwa mwaka 1960, ni mwanamke mwenye heshima kubwa kwenye uga wa kidiplomasia.

Kabla ya kushika nafasi hiyo, Dk Stergomena alikuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini ya Afrika (SADC), nafasi aliyoanza kuishikilia tangu mwaka 2013.

Kwa mujibu wa wasifu wa Dk Stergomena, kabla hajaitumikia SADC kwa miaka minane akiwa Mtendaji mkuu, alikuwa mtumishi wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Aliteuliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2008 na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Uteuzi wa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afrika Mashariki ulikuwa kupanda cheo, kwani kabla ya hapo, alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji.

Stergomena, ambaye ni mama wa watoto wawili, aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango mwaka 2006, akitoka kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Ubora (BRU), katika Mpango wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Biashara Tanzania (BEST), chini ya Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji.

Aliwahi pia kufanya kazi katika Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) kama mratibu na mshauri. Kuanzia Mei 1991 mpaka Aprili 2002, alikuwa mfanyakazi wa Wizara ya Fedha, akiwa mhusika mkuu wa usimamizi wa misaada na uratibu (AMC).

Akiwa Wizara ya Fedha, Dk Stergomena alikuwa Ofisa wa usimamizi wa fedha kabla ya mwaka 1993, alipokuwa ofisa mkuu wa dawati la Benki ya Dunia. Mwaka 1995, alikuwa msimamizi mkuu wa dawati la Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Wizara ya Ulinzi haikuwahi kushikwa na mwanamke tangu uhuru kutoka kwa mkoloni.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post