MAHUSIANO: Mpenzi mpya akikuonyesha upendo uliopitiliza, stuka

MAHUSIANO: Mpenzi mpya akikuonyesha upendo uliopitiliza, stuka

Ni wazi wengi wetu tumeashawahi kusikia malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanawake wakisema, ‘kabla hatujaoana alikuwa malaika kabisa, yaani alikuwa ananifanyia kila kitu hadi siamini, lakini leo hii anavyonipiga na kunikashifu, huwezi hata kuamini.’

Wataalamu wa mapenzi na uhusiano wanasema, mwanaume kuonyesha upendo ambao unamfanya hata yule anayependwa kushindwa kuamini na pengine hata wanaomzunguka, hiyo ni dalili kwamba, mwanaume huyo sivyo alivyo. Anaigiza tu, na ana lake jambo.

Hebu jiulize kama kwa mfano, kila wakati mwanaume anapiga simu akitaka kusikia sauti yako. Ni kweli kwa mujibu wa maelezo yake anataka tu kusikia sauti yako, yaani anaipenda sana. Halafu anakupitia kwenye shughuli zako au kazini kwako ili kukurudisha nyumbani. Wakati mwingine anakusubiri hadi utoke, hata kama ni kwa kukaa nje kwa saa mbili au tatu. Halafu anakupeleka nyumbani kwako au kwenu, hata kama itamlazimu kurudi kwake usiku wa manane, lakini yeye yumo tu, na anafanya hivyo akiwa na bashasha.

Inawezekana pia kwamba, anafanya shughuli zote ambazo ulikuwa unazifanya, ambazo yeye anazimudu. Anaweza kupita dukani kununua kitu ambacho labda huwa unanunua kila siku ukitoka kazini au chuoni au shuleni. Ili mradi anaweza kufanya kila ulichokuwa unafanya na mwisho anakuwa amechukua maisha yako yote. Unaweza kabisa kuamini kwamba, huyo mwanaume na wewe ni kama mwili mmoja. Yaani huyo ndiye yule anayeitwa mwanaume mwenye muafaka (husband material)

Lakini bado wataalamu wa mapenzi na mahusiano wanatahadharisha kwamba, hapo hakuna mapenzi na hayo kamwe siyo mapenzi. Wao wanasema, wanachokiona hapo ni mwanaume mfujaji ambaye anaingia na dalili kubwa kabisa ya ufujaji, ambayo ni kudhibiti maisha ya mtu, kutompa nafasi anayedaiwa anapendwa.

Lakini kwa nje na kabla mwanaume huyu hajaonyesha kucha zake halisi, hiyo inahesabika kama upendo. Ni vigumu kumtoa mtoto wa kike kwa mfano kwa mwanaume kama huyo. Hii ni kwa sababu, anaamini kabisa kuwa huyo jamaa anajua kupenda kuliko mwanaume mwingine yoyote.

Kwa bahati mbaya kinachomzubaisha mwanamke hapo ni pamoja na zawadi au kupewa kila anachohitaji. Kinachomzuzua ni ile hali ya mtu kutaka kukuona muda wote na kutaka kusikia sauti yako, kinachosababisha ni ile hali ya mtu kufanya kila kitu ambacho ulikuwa ukifanya mwenyewe hapo awali.

Lakini kitu kingine ambacho msichana au mwanamke anatakiwa kukikagua kwa mtu ambaye ni mfujaji, ambacho bila shaka yeye anaweza kudhani ni kupendwa ni huyu jamaa kumtukana au kumkashifu mke au mpenzi wake wa zamani, ili kumwonyesha huyu wa sasa kwamba, yeye ndiye anayefaa.

Wataalamu hao wanabainisha, hiyo ni dalili kwamba, huyo jamaa ni mfujaji. Msichana au mwanamke anaweza kudhani kwamba, huyu jamaa anamtukana mke au mpenzi wake wa zamani kwa sababu amempata mwanamke mwenye sifa zote, ambaye ni yeye. Hilo ni kosa kubwa ajabu. Kumkashifu mke au mpenzi wake wa zamani siyo dalili kwamba, amempata mwanamke wa maana zaidi, hapana. Hiyo ni dalili kwamba huyo mwanaume ni mfujaji.

Ni vyema wanawake na hasa wale ambao ndiyo kwanza wanaingia kwenye uhusiano kukagua dalili hizi. Kuna kujidanganya kwingi kwamba, hata kama mwanamume ni mfujaji, mwanamke ataweza kumbadili. Hiyo ni karibu na uongo na kujaribu ni sawa na kucheza tombola. Kumbuka maisha hayachezewi tombola…






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post