Hisia za mashabiki zinavyokera wasanii

Hisia za mashabiki zinavyokera wasanii

Awali ilizoeleka kuwa wasanii ndiyo hurusha vitu vyao kama nguo, saa na hata kofia kwa mashabiki kama zawadi, lakini pia kwa upande wa mashabiki hao hutumia vitu kama vile pesa, maua na hata vitu vyao kuwarushia wasanii jukwaani wakati wakitumbuiza wakiwa na lengo la kuwapongeza na kuthamini wanachofanya.

Urushaji wa vitu hivyo huaminika kama njia ya kuonesha shukrani, kuunga mkono na wakati mwingine kugeuka na kuwa njia ya kumkataa msanii jukwaani.

Matukio kama hayo yamekuwa yakitokea duniani kote na hivi karibuni limetokea mwanamuziki wa Bongo Fleva Zuhura Othman 'Zuchu', ambaye mara kadhaa amekuwa akilia na tabia ya baadhi ya mashabiki kumrushia vitu kama mawe au chupa akiwa jukwaani anatumbuiza.

Ambapo Septemba 29,2024, wakati akitumbuiza kwenye tamasha la Wasafi Festival Mkoani Mbeya, Zuchu alionesha kukerwa na baadhi ya mashabiki waliomrushia vitu wakati akitumbuiza na kupeleke aondoke jukwaani kabla ya kumaliza kutumbuiza.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa msanii kutoka lebo ya WCB kukutana na matukio hayo akiwa jukwanii kwani katika tamasha hilohilo la Wasafi Festival mkoani Songea, mwaka 2023, alirushiwa chupa na mashabiki.

Inawezekana ikawa mzuka wa mashabiki unapelekea kufanya hivyo, lakini kwa baadhi ya wadau wa muziki wameonesha kukerwa na vitendo hivyo huku wengine akitoa namna bora ya kufanya.
Akitoa maoni kuhusiana na tukio hilo Fatma Karume kupitia ukurasa wake wa X (Twitter), amesema vitendo hivyo vinahuzunisha.

"Inahuzunisha sana. Mnakwenda kustarehe halafu mnatupa chupa kwa muimbaji. Kuna jambo kubwa sana lililo potofu kuhusu hasira katika jamii hii, (Something very wrong with the aggression in this society),"ameandika.

Mbali na ujumbe huo Mwakajoka kupitia ukurasa wake wa X amewataka waandaaji wa matamasha kufanya tafiti kuhusiana na hadhira ya baadhi ya maeneo kabla ya kuwapeleka wasanii.

"Waandaaji wa haya matamasha wanapuuza sana swala la tafiti, wangefanya tafiti ya mapendeleo ya watumiaji (consumer preferences), na kuweza kubaini hadhira (audience) ya wakazi wa Mbeya wanataka wanamuziki gani, badala yake wanafanya maamuzi kwa hisia, ameeleza",ameandika

Naye mwanamuziki wa Bongo Fleva Elias Barnabas, 'Barnaba' ameeleza kuwa haungi mkono vitendo hivyo vya mashabiki.

"Siungi mkono kabisa mashabiki kufanya fujo kwenye show kama hivi. Watu wanawekeza pesa nyingi kuwapa kinachostahili kama mashabiki, lakini mambo mnayotulipa sio poa kabisa.

"Kibaya zaidi yule ni binti binafsi siungi mkono kwa tukio la Zuchu lakini niseme direct watu wa mbeya mnafanya haya mambo zaidi ya mara 3 sio poa kabisa hata kama ndo vibes basi kuweni na nidhamu na heshima,"amechapisha Barnaba kwenye ukursa wake wa Instagram.

Mbali na matukio hayo ambayo yametokea nchini yakimgusa msanii huyo mmoja, wasanii wengine kama vile Drake na Cardi B wamewahi kukutana na majanga hayo wakiwa jukwaani.

Utakumbuka mwanamuziki Drake kutoka Canada ni kati ya wasanii ambao wamekuwa wakirushiwa vitu mbalimbali vya ajabu kutoka kwa mshabiki.

Septemba 2023, mkali huyo kupitia ukurasa wake wa Instagram alichapisha picha za sidiria alizowahi kurushiwa jukwaani na mashabiki jambo lililopelekea kuzua taharuki na kusababisha wengine wamshauri aziuze.

Siyo yeye tu katika wengi waliowahi kukumbana na madhira hayo ni mwanamuziki wa Marekani Cardi B, ambaye 2023 pia, video zake zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha akimrushia Mic mashabiki jijini Las Vegas, ikiwa ni baada ya shabiki huyo kummwagia maji Cardi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post