Wachekeshaji Oscar Martin 'Oka Martin' na Edward 'Carpoza' ni watu wanaotokea dunia tofauti, lakini hadi sasa wanachukuliana kama makaka wa damu, kutokana na ukaribu waliojijengea.
OKA MARTIN
Oka Martin ni mpole kwa asili. Alikuwa na ndoto za kuwa mwalimu, endapo asingeingia katika shughuli za uchekeshaji. Ingawa alijulikana na mtu mcheshi toka alipokuwa nyumbani, ila hakuwahi kudhania kama kuna siku angefanya uchekeshaji kama kazi ya kudumu. Alizaliwa katika familia ya watoto wa 4, mnamo tarehe 2o, Julai.
Mwenzake (Carpoza) anamuelezea Oka Martin kama mtu 'genius', kwani ubunifu mwingi wanaoufanya kwa pamoja, huwa umetoka kwake.
CARPOZA
Katika watu waliosumbua wazazi wao angali wadogo, basi Carpoza ni mmoja wapo. Alizaliwa tarehe 24, Aprili, akiwa ni Mkazi wa Arusha. Alipitia mkasa wa kufukuzwa kazi siku ya kwanza kabisa ya ajira kutokana na misimamo yake. Baada ya kuja Dar es Salaam, Carpoza aliingia studio ambapo alifanya kazi za muziki na ndipo alipokutana na Oka Martin. Ndoto yake kubwa ilikuwa kuwa mhandisi, fani ambayo aliisomea na hakudhani kabisa kama ipo siku atakuwa mchekeshaji.
WANYABI NA UCHEKESHAJI
Nilipo wauliza kama Wanyabi ni jina lao la kundi, wote wawili walikataa, ingawa watu wengi huwaita wanyabi wakiwa pamoja. Neno Wanyabi lina maana ya mtu asiyejua na hajui kama hajui, na hivyo ndivyo wao wanavyojitizamia.
Wawili hao walikutana katika studio, ambapo wote wawili walikuwa wanafanya muziki. Hii ni takribani miaka 6 iliyipita.
Siku ya kwanza kuingia studio pamoja, Carpoza asema, "Jamaa nilimvunjia kifaa cha kurekodia. Alinimind sana ila hakusema." Kutokana na historia yao kujengwa siku hiyo, Carpoza aliamua kukitunza kifaa hicho hadi sasa.
Rafiki yao pale studio, aliwashauri kutengeneza video za uchekeshaji pamoja, baada ya kuona kuwa Carpoza nae anauwezo wa kuchekesha. Kipindi hicho Oka Martin alikuwa tayari amekwisha anza shughuli za uchekeshaji, na hapo ndipo uhuasiano wao ulipoanzia.
Katika safari yao walikumbwa na changamoto nyingi sana, hadi kuna wakati walihisi kukata tamaa kutokana na kazi zao kutozaa matunda kama walivyotegemea.
"Tumefanya shughuli za uchekeshaji kwa takribani miaka 6 sasa, ila tumeanza kujulikana na kuonja matunda ya tunachokifanya toka miaka mitano nyuma. Kuna kipindi tulikaa hatuna pesa kabisa, hadi tunakata tamaa, ila kwa sababu ni kitu ambacho tunakipenda, tukipata 'idea' kichwani, tunataka kufanya, na hivyo ndivyo tulivyoweza kuendelea na sanaa yetu kwa muda mrefu'" asema Oka Martin.
Wao wenyewe wanachukulia kukutana kwao kama kitu kilichopangwa, kwasababu kila mmoja anakitu ambacho anakileta mezani. Oka Martin akiwa yupo zaidi katika ubunifu na Carpoza alijazilizia zaidi katika utendaji.
Ukiwaona wawili hawa, bila shaka utadhani kuwa hata maisha yao ni ya kimasihara, lakini jambo la kushangaza ni kwamba, wawili hawa katika maisha ni wapambanaji na watu wenye misingi na misimamo.
Waliamua kuelekeza matunda ya mafanikio yao katika kuwekeza zaidi kuliko utumiaji, ili waweze kukuza zaidi sanaa yao, jambo ambalo wasanii wengi hushindwa kwani wanahitaji ku'maintain status' kama wazungu wanavyopendelea kusema.
Carpoza aliiambia MWANANCHI SCOOP kuwa, "Kati ya jambo ambalo tungetamani watu kujua ni kwamba sisi tupo 'serious' makini na maisha yetu. Wengi wakituona mitandaoni tukifanya vitu vya kuchekesha hutuchukulia poa, ila hii sanaa inatuwezesha kupata mahitaji yetu, lakini pia kusuluhisha changamoto za hapa na pale zinapojitokeza, kuliko hapo zamani."
Aliongeza pia Oka Martin kwa kusema kuwa waliwahi kukataa dili la milioni ili hali hawana chochote mfukoni, kwasababu kazi walitakiwa kufanya haikuendana na malengo na maudhui yao.
Wawili hao walieleza zaidi kuwa huwa hawakai kupanga au kutafuta 'idea' ya nini wafanye, kazi zao nyingi huwa wanatoa mawazo kutokana na maongezi yao au na watu wengi, hii inachangia kwa sanaa yao kuwa na uhalisia zaidi na masuala ya kijamii.
Wamewataja Joti na Mpoki, kama watu ambao wametoka mbali kwenye tasnia, na wanakula matunda ya kazi zao, hivyo huwa wako 'inspired' nao.
Oka Martin na Carpoza wanakiu ya kuisukuma gurudumu la sanaa ya uchekeshaji nchini Tanzania kwa kuweza kwanza kuongeza ubunifu na ufanisi katika kazi zao, ili pale watakapofikia mahala stahiki, waweze pia kuinua wasanii wengine chipukizi.
"Ninachoamini ni kwamba kila uzao una watu wao, mfano sisi tuna nafasi zaidi ya kuleta mabadiliko kwa watu wa sasa, ila kwa hapo baadae kuna haja wakuandaa wengine wataochukua usukani pia kwaajili ya watu wao," aseme Carpoza.
"Chochote tukipatacho sasa, tunajitahidi kuwekeza katika vitu ambavyo vitakuza sanaa yetu. Asilimia kubwa ya kipato chetu kinaenda huku, na kinachobakia ndiocho tunafanyia mengine," aliongeza Oka Martin.
Hata hivyo, nilipo uliza kuhusu masuala ya mahusiano na ndoa, wote walikiri kuwa na wenza, na Oka Martin kugusia kuwa panapo majaliwa, basi anaweza akafunga ndoa mwakani, huku mwenzake Carpoza akitumia msemo wa Mwana FA 'bado yupo yupo sana'.
Pamoja na kujitosa kuwa mabalozi wa kampuni mbalimbali kama vile Cowbell na Parimatch, wawili hao huwa waangalifu sana katika kuchagua ni aina gani ya kazi wanaweza kufanya, kwani kuna vingine haviendani na wao na ni mwiko kufanya.
"Mimi siwezi nikaja kuigiza kama mwanamke. Pamoja na kwamba ni kazi na wapo wanaofanya, ila hili ni mwiko kwangu, hata familia yangu walinisihi sana nisifanye sanaa ya aina hiyo na nina heshimu zaidi mawazo hao. Hata mwenzangu (Carpoza) hawezi kuniruhusu nifanye hivyo," aliongeza Oka Martin.
Pamoja na kupiga hatua kadhaa mbele katika sanaa yao, wawili hao bado wanajiona kama ndio kwanza wanaanza, kwani wana kiu ya kufika mbali zaidi, huku wakiwashauri wasanii wenzao kuwa makini na kuwa na malengo katika kazi zao.
"Tunawashauri tu wenzetu ambao wapo kwenye sanaa na wanaotaka kuingia, wajue wanachokifanya, wakithamini na wajue pia malengo yao, kwani malengo ndio yatakaowafanya wasitoke katika mtari," alisema Oka Martin.
Ni malengo na mategemeo makubwa ambayo wamejiwekea wenyewe, yanayowasukuma kufanya kazi zaidi siku hadi siku. Wana ndoto wa kwamba ipo siku watakaa na kuhadithia mambo ambayo sanaa imewafanyia, ili watu waweze kujua kuwa sanaa pia ni ajira tosha.
Kuona kazi zao mbalimbali, wafuatilie kupitia YouTube, Instagram, TikTok au Twitter: @OkaMartin na @MwalimuCarpoza
Leave a Reply