VISA NA MIKASA: Nikaenda kumuona Mkurugenzi, nikapigwa butwaa

VISA NA MIKASA: Nikaenda kumuona Mkurugenzi, nikapigwa butwaa

 

Nakumbuka ilikuwa ni mwaka ya 2010 ndipo nilipokutana na fedheha hii ambayo sitakuja kuisahau maishani.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000 nilikuwa nafanya kazi kwenye kampuni moja ya ujenzi ya Wajapan na nilikuwa katika kitengo cha manunuzi. Kutokana na rushwa na wizi nilijikuta nikiwa na fedha za kutosha kufanyia starehe na uasherati.

Kutokana na ujana sikuwaza kufanya maendeleo wala kuweka akiba kwa kuwa fedha zilikuwa zinaingia kila siku nikawa ni mtu wa kula bata huku nikibadilisha wanawake vile nitakavyo. Kwangu mimi kumtongoza mwanamke yeyote na kulala naye ilikuwa ni jambo la kawaida na wala sikuwahi kuwaza wala kuogopa Ukimwi ambao kwa wakati huo ulikuwa umeshika kasi.

Nilikuwa sijui kukataliwa na mwanamke, kwani mwanamke awaye yeyote nikimtongoza akaikataa natumia fedha kumnasa na kwa kweli niliwanasa wanawake wengi sana kwa sababu niliamini kwamba fedha ni mtego uwanasao wanawake kirahisi kuliko upendo.

Kila nikimpata mwanamke namuaminisha kwamba yeye ni malaika kwangu na nauahidi kwamba nitamuoa, ahadi ambayo wanawake wengi walikuwa wanaota kuolewa hasa walio katika umri wa usichana. Lakini nikishatembea naye kwa muda mfupi nikimchoka namuacha na kutafuta kipusa kingine.

Sikuona hata huruma kuwaumiza wanawake kwa sababu niliamini kwamba nimezaliwa kula starehe na si vinginevyo. Suala la kudumu na mwanamke kwa muda mrefu halikuwa akilini mwangu kabisa. Nilichukulia suala la mapenzi kama biashara kwamba wanawake wanauza na mimi nawanunua kwa fedha zangu za wizi. 

Nakumbuka nilikutana na binti mmoja mzuri sana. Alikuwa ni mwanamke mwenye asili ya Kipemba na Kimbulu, mama yake akiwa ni Mbulu na baba yake akiwa ni Mpemba. Leyla alikuwani binti mwenye rangi ya chocolate, mrefu mwenye nyonga kama ya nyigu na mahipsi yaliyobeba makalio yake makubwa barabara.

Nilikutana naye katika duka la vifaa vya ujenzi wakati huo nilienda kununua vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kampuni niliyokuwa nikifanya kazi na yeye kama mimi alikuwa ni mteja katika duka hilo alikuwa amefuatana na mafundi akinunua vifaa vya ujenzi. Kwa kuwa nilikuwa chakaramu na mwepesi kuwaingia wanawake nilianza kwa kumchokoza..

‘Hongera dada kwa umri huu tayari umeanza ujenzi, ni wanawake wachache sana wa umri wako wenye uthubutu wa kuanza ujenzi wangali vigori kama wewe.’

Kwanza alicheka kisha akanijibu huku akitabasamu, ‘Siyo nyumba yangu, bali ni nyumba ya baba anajenga kwa ajili ya kupangisha huko Tabata.’

Basi tulijikuta tumeanza mazungumzo na kuzoeana kwa muda mfupi. Katika mazungumzo yetu niligundua kwamba binti yule anaitwa Leyla Mohammed. Ni Binti wa mfanya biashara mmoja wa maduka ya jumla huko Tabata na ni binti wa kwanza kuzaliwa akifuatiwa na wadogo zake watatu, wawili wa kiume na mmoja wa kike. Alikuwa ndiyo amemaliza chuo kikuu mlimani akiwa amesomea mambo ya Biashara yaani Business Administration na kupata shahada yake ya kwanza katika masomo hayo.

Tulibadilishana namba za simu na kuanzia hapo tukawa na mamasiliano kwa karibu sana kiasi kwamba usiku tulikuwa tunaongea kwenye simu mpaka zinapata moto.

Ukweli ni kwamba Leyla alionekana kunipenda kutokanan na uchakaramu wangu ile hulka yangu ya kupenda mizaha na kuchekesha. Hili lilimfanya anipende sana wakati mimi kama Simba muwindaji wala sikuwa na mapenzi na yeye zaidi ya kutaka kumega na kusepa.

Baada ya kuwa na mawasiliano kwa muda mrefu nilimwambia tupange siku tukutane mahali tulivu kwa mazungumzo. Alikubali na nilimuelekeza tukutane maeneo ya Mwenge na yeye alikubali. Nilipanga eneo la kukutane ni karibu na Hoteli ili iwe ni rahisi kumshawishi kwenda naye hotelini ili nitimize azma yangu ya kufanya naye mapenzi.

Ni kweli alikuja majira ya mchana kama tulivyokubaliana na tukakutana kwenye mghahawa mmoja pale Mwenge. Alikuwa amevaa mavazi mazuri ya Kiislamu na kwa kweli hayakuacha kuonyesha umbo lake maridhawa japokuwa lilikuwa ni gauni refu. Leyla alikuwa ni binti mzuri ambaye kila mwanaume angetamani kuwa na mahusiano naye au hata kumuoa.

Baada ya kupata chakula cha mchana nilijaribu kumshawishi twende Hoteli kwa ajili ya mazungumzo zaidi nikitaka kwenda kufanya naye mapenzi lakini akakataa katakata akidai ni kinyume na dini yake ya Kiislamu.

Niliamua kuwa mstaarabu na kukubaliana naye. tulizungumza mengi na baada ya hapo tukaachana yeye akienda Tabata na mimi nikienda nyumbani kwangu Kijitonyama.

Tuleendelea kuwasiliana na kujenga ukaribu huku nikiamini kwamba kwa kutumia fedha nitampata Leyla kirahisi kwani nilijua tu kwamba ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu, lakini haikuwa hivyo, Pamoja na kutumia fedha zangu nyingi kwa mitoko na kumnunulia zawadi kemkem lakini Leyla alibaki na msimamo wake ule ule, hakuna kufanya mapenzi mpaka tufunge ndoa.

Baada ya kuishiwa mbinu zote niliamua kufanya maamuzi magumu. Nikajisemea kama shida ni ndoa basi ngoja nipelele posa. Nikajua nikipelelka posa nitampata kirahisi ili kutimiza azma yangu ya kukutana naye kimwili. Niliona ni kashfa kubwa sana kwangu kukataliwa na mwanamke wakati uwezo hususan ule wa kifedha kutokana na kupata marupurupu mengi kiujanjaujanja nilipokuwa  nikifanya kazi.

Nilipokutana na Leyla nilimweleza nia yangu ya kuleta posa kwao na nilitaka kujua taratibu za kimila za kwao kama zipo.

Kwanza alishangaa sana na baada ya kumhakikishia kuhusu nia na dhamira yangu akafurahi sana. Ukweli ni kwamba Leyla alikuwa anakwepa sana kuja kwangu na hata maeneo ya kukutana alikuwa anachagua yeye kwa hiyo mbinu na mitego yangu yote ya kufanya naye mapenzi ilikuwa ikipachuka kile nikitega.

Baada ya kumweleza alinishauri kwanza niache pombe na nianze kuswali. Kwani Pamoja na kuwa nilikuwa muislamu lakini nilikuwa siswali na nilikuwa mtu wa pombe na starehe na wanawake.

Nililazimika kununua kanzu na kuanza kuswali. Awali pale msikitini nilipokuwa nikienda kuswali Masheikh walinishangaa kwa sababu walikuwa wananiona pale mtaani nikiwa kwenye mabaa nikinywa pombe huku nikiwa nimezungukwa na wanawake.

Ukweli ni kwamba hawakujua kwamba mabadiliko yangu yalikuwa ni ya kimkakati ili kumnasa binti Leyla Muhammed, binti wa kiislamu mwenye msimamo na Imani yake.

Baaada ya Leyla kuona mabadiliko yangu akanikubalia nipeleke posa na baada ya kuzungumza na baadhi ya wazee niliokutana nao pale msikitini walikubali kunisaidia kupeleka posa yangu kwa wazazi wa Leyla. Mzee mmojawapo aliyekubali kusimamia zoezi hilo aliniambia kuhusu suala la kuandikwa barua na kiasi cha pesa cha kuambatanisha na na barua ile.  Nilitoa laki moja na kuwapa wale wazee ili kukamilisha mchakato haraka haraka. Wale wazee alipoona zile fedha wakachanganyikiwa na kuahidi kulifanya zoezi kwa ufanisi.

Waliomba ramani na nikawaelekeza na baada ya wiki wakanipa mrejesho kwamba posa imepokelewa  na nisubiri majibu.

Majibu yalitoka baada ya wiki mbili tangu posa kupelekwa na hiyo ilitokana na Leyla kulazimisha sana nijibiwe kwa sababu baba yake alikuwa anataka kufanya uchunguzi kuhusu familia yangu na mambo mengine lakini presha za mama na bintiye barua ikajibiwa na mahari ikapangwa na kutokana na haraka ya kutaka kumpata Leyla nililipa chapchap na kuomba ipangwe siku ya ndoa.  

Niliambiwa nivute Subira maana kuna ndugu kutoka Pemba na Arusha inabidi washirikishwe hususan mashangazi kwa sababu Leyla ni binti wa Kwanza kuzaliwa wazazi walipanga harusi yake iwe ya kukata na shoka.

Kitendo cha kulipa mahari kilinifanya niwe huru sasa na Leyla hasa uhuru wa kufika kwao na kutoka naye mara kwa mara kwa mitoko ya kawaida na wakati mwingine akija kwangu kunifanyia usafi lakini bado aliendelea na msimamo wake wa kusubiri mpaka ndoa.

Kuna siku moja nilijifanya mgonjwa na nikamtafuta Rafiki yangu mmoja daktari nikamuomba anitundikie tu drip kuonyesha naumwa kisha ampigie simu mchumbangu  amwambie naumwa na hali yangu siyo nzuri,

Leyla alikuja haraka sana na akawa akinihudumia Pamoja na yule Rafiki yangu Daktari. Majira ya jioni nikajifanya nimepata nafuu na daktari akaaga na kuondoka baada ya kuchomoa dripu tukabaki watu wawili mimi na Leyla. Nilitumia mbinu zote mpaka kulia ili Leyla anikubalie ombi langi la kukutana naye kimwili mpaka akalainika na kukubali. Nakumbuka zoezi lilikuwa maridadi maana kutokana na mavazi anayovaa nilikuwa kama vile namnyonyoa kuku manyoya. Nilimvua nguo na kukutana na mwili laini wa binti huyu ambaye alinisotesha kwa takriban mwaka mmoja nikisotea penzi. Nilihakikisha natumia ujuzi wangu wote ili kumpagawisha binti huyu. Kwa kweli alionekana kutoshiriki jambo hilo kwa muda mrefu maana nilipata tabu sana kukamilisha zoezi lakini hatimaye nikafanikisha zoezi na binti akawa hoi taaban.

Baada ya kufanya tendo binti akawa amenogewaa ikawa sasa siyo zamu yangu kuomba bali yeye akawa ndiyo anakuja mwenyewe kama vile Mbwa anavyojipeleka kwa Chatu ili amezwe.

Baada ya miezi kadhaa tangu nipeleke posa na kulipa  mahari na mimi kupata penzi la binti huyu aliyenisumbua sana nilianza sasa kurudia tabia zangu za awali. Nilianza kunywa pombe na msikitini nikawa siendi tena kama zamani. Nilianza kuwa busy na kula bata na kubadilisha wanawake lakini kwa siri sana maana nilikuwa nawapeleka Hotelini badala ya kwangu na nilikuwa namdanganya mchumba wangu Leyla kwamba nimesafiri kikazi kukagua mradi wa kampuni yetu Morogoro.

Hata hivyo mshenga wangu aliitwa kwa ajili ya kupangwa tarehe ya Ndoa ambapo aliponijulisha nikamtuma awaambie wakwe zangu kuwa  nasafiri kwa masomo nchini Japan na nitarudi baada ya miezi sita kwa hiyo nikirudi ndiyo nitafunga ndoa. 

Baada ya kutoa taarifa nilianza kuwa adimu kwa Leyla na hatimaye nikahamia Tegeta na kubadilisha namba yangu ya simu na hivyo kutokuwa na mawasiliano naye tena.

Maisha yaliendelea na sikumkumbuka yena Leyla nikasonga mbele na masiha yangu ya starehe na uasherati.

Baada ya miaka mitano mradi ukawa umeisha na tukalipwa mafao nikarudi mtaani kutafuta ajira upya. Hata hivyo nilipata wazo la kubadilisha taaluma na kusomea Mauzo na Masoko nikiamini kwamba ni rahisi kupata ajira hususan kwenye viwanda na makampuni makubwa. Nilimaliza masomo yangu baada ya miaka miwili na kuingia mtaani kutafuta ajira. 

Siku moja niliona Tangazo la nafasi za Kazi kwenye kampuni  inayouza vifaa vywa ujenzi kutoka nje ya nchi.

Niliomba kazi na baada ya mchakato wa usaili nilipata kazi na kupangiwa kazi katika tawi la Kariakoo. Nilianza kazi chini ya meneja wangu ambaye alikuwa akinipa ushirikiano tangu awali. 

Ghafla nikashangaa kila nikipeleka ripoti zangu anasema Mkurugenzi kazikataa akisema zina makosa na wakati niandae nyingine ambazo pia alikuwa anazikosoa.

Cha kushangaza huyu Meneja wangu kwenye Tawi letu alikuwa ananikubali sana na alipokuwa akipitia ripoti zangu alikuwa anazisifu sana. Iweje huyu Mkurugenzi Mkuu aone kasoro! Jambo lile lilininyima raha sana, lakini pia haikuishia hapo, hata nikifanya miadi na wateja nikienda naambiwa ilipigwa simu kutoka makao makuu ya kampuni yetu kwamba appointment yangu imekuwa cancelled

Kwa bahati mbaya huyu Mkurugenzi nilikuwa simjui na makao makuu ya kampuni niliyoajiriwa ambayo yalikuwa Masaki nilikuwa sijawahi kufika.

Baada ya kuona kila ninachofanya kina kasoro na Mkurugenzi anaingilia hata appointment zangu nilikata shauri kwenda kumuona mimi mwenyewe na kuzungumza naye ili kujua tatizo ni nini. 

Meneja wangu alinisihi sana nisiende kwani aliniambia kwamba Mkurugenzi wa kampuni ile ni Mke wa mwenye Kampuni ambaye ni Muarabu na yeye yaani huyo Mkewe anasimamia biashara zote ya vifaa vya ujenzi kati ya biashara zake nyingi sana alizo nazo hapa mjini huyo mumewe.

Aliniambia huyo mke wa Bosi ni Mkorofi sana na kumfukuza mtu kazi ni suala la sekunde tu akiamua na hakuna wa kumuingilia kwenye maamuzi yake.

Pamoja na tahadhari hiyo niliamua kwenda kama ni ajira kwisha basi kwani nilichoka kudhalilishwa.

Nilipofika nilimkuta sekretari wake na nilipomuomba kumuona mkurugenzi alinikatalia Pamoja na kumsisitiza sana alikataa kata kata. Kwa kuwa nilishakuwa na hasira niliingia bila ruhusa yake na yeye akanifuata nyuma huku akinishika kunizuia nisiingie. Nilipoingia yule Mkurugenzi ambaye alikuwa amesimama dirishani akiangalia nje akiwa ametupa mgongo alimwambia sekretari wake aniache na yeye atoke nje na kunicha pale.

Hakugeuka kuniangalia bali aliniuliza sababu ya kungia ofisini kwake bila ruhusa yake. Nikiwa nimehemkwa kwa hasira nilianza kulalamika kuhusu anavyonitendea isivyo wakati najitahidi kufanya kazi kwa weledi na bidi ili kufikia malengo ya kampuni lakini nashangaa ripoti zangu anazikataa……. Wakati wote naongea yeye bado alikuwa amesimama Dirishani amenipa mgongo.

Nilimaliza kujieleza na kumuomba anieleze kosa langu na anifundishe namna anavyotaka nifanye kazi.

Aligeuka taratibu huku akiwa ametabasamu na akiwa anapiga makofi…. Vile kuona sura yake moyo wangu ulipiga paaaaa…. Nusura nizimie… nilijikuta mwili ukinitetemeka na jasho jembamba likinitoka.

Hivi mnaweza kukisia yule Mkurugenzi alikua ni nani?

Hamuwezi kuamini alikuwa ni Leyla yule mchumba niliyemtolea posa na mahari na kumtelekeza baada ya Kukutana naye kimwili na kufanya naye mapenzi mara kadhaa.

Leyla alicheka sana tena sana Kisha akaniambia karibu sana Leynoor Company Limited na Mimi ndiye Boss wako hivi sasa ninayekulipa mshahara kwa hiyo utafanya kazi kwa maelekezo yangu….. Kisha akaniamuru niondoke ofisini kwake haraka sana.

Je mnataka kujua kilichoendelea baada ya kikao changu na boss wangu Leyla…..?

Itoshe tu kusema kwamba tukio lile lilinipa funzo kubwa sana maishani kwamba Karma inalipa hapa hapa duniani..

Ukitenda ubaya utalipwa ubaya maradufu na ukitenda wema utalipwa wema mara dufu. Ni kanuni ya maumbile. 

Tujitahidi sana kutenda wema.

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post