Khanga ni vazi linalosifika kutokana na mtindo wake wa kuandikwa jumbe nyingi zenye maana na mafumbo mbalimbali lakini hivi sasa mambo ni tofauti kwani yamekuja mavazi mengine yaliyochukua nafasi ya khanga kama vile Kijora, Dera na Kikoi.
Kutokana na mabadiliko ya maisha yanayoletwa na utandawazi wanawake wengi hususani jiji la Dar es Salaam wamejikuta wakilitelekeza vazi hili na kuamia kwenye mavazi ya mtindo mpya na wakisasa zaidi.
Moja ya matumizi ya vazi hili adhimu kwa mwanamke wa Kiafrika ilikuwa linatumika kama sare katika sherehe mbalimbali lakini hivi sasa limepotea.
HISTORIA YA VAZI HILI
Vazi hili likiwa asili yake ni Zanzibar, lilianzishwa kutokana na ushawishi wa wareno ambapo khanga ya kwanza kuchapishwa ilikuwa khanga yenye rangi nyeusi mnamo mwaka 1860, na jina la khanga hiyo ilijulikana kama khanga ‘Zhamira’ na baadae vazi hilo likaendelea kukua katika ubunifu mbalimbali.
Mwanzoni khanga ilikuwa ikirembwa kwa vitone vidogo ambavyo vilionekana na manyoya ya ndege aina ya kanga. Ndiyo sababu ilipewa jina hili.
Kanga huwa na sehemu tatu ambazo inakuwa na pindo, mji (sehemu ya kati), na ujumbe. Ujumbe ambao mara nyingi huwa ni kitendawili au fumbo.
Hii ni mifano ya ujumbe wa kwenye kanga: Majivuno hayafai, mkipendana mambo huwa sawa, japo sipati tamaa sikati, Wazazi ni dhahabu kuwatunza ni thawabu, Sisi sote abiria dereva ni Mungu, Mwanamke mazingira, Naogopa simba na meno yake siogopi mtu kwa maneno yake.
WALIOVAA ZAMANI
Mwamvita ubeto anasema zamani ilikuwa ni heshima kwa mwanamke kuvaa na kutumia khanga kumbebea mtoto tofauti na anavyoona sasa kwa wanawake na wasichana wengi
HALI ILIVYO SASA
Jenipher Steven mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam yeye anasema anaona matumizi ya vazi hili kwa sasa yamepungua kutokana na utandawazi, wanawake wengi hivi sasa hawalitumii kama kubebea mizigo mfano ndoo za maji, kucheza ngoma za asili, kuchana nepi za watoto, kutengeneza malemba ya kuvaa kichwani au kufikisha ujumbe.
“Mama zetu na bibi zetu walikua wanavaa khanga vizuri tu tena walikuwa wanafikishiana ujumbe kupitia hizo khanga ambazo huwa na maandishi tofauti na sasa hivi ambapo mtu anakusema mubashara kwenye mtandao wa Whatsapp kwa kuweka Status” alisema Jenipher.
Nae Zulfa Abdallah kutoka Kinyerezi Dar es Salaam anasema yeye pia ni mmoja wapo ya waliopunguza matumizi ya vazi hili kutokana na kupendelea nguo za kisasa zenye muonekano mzuri zaidi ya khanga.
“Mimi sio kwamba sivai, navaa mara chache nikiwa nyumbani, mimi napenda kuvaa nguo ambazo zinanifanya niwe huru,” alisema Zulfa
Anaongeza kwamba zamani aliona dada zake ikiwa watavaa suruali basi lazima wajifunge na khanga kwa juu lakini yeye kwa sasa hivi hawezi kwa sababu huwa inambana.
Mwananchi Scoop haikuishia hapo tu moja kwa moja mpaka jiji Mwanza tuna kutana na Leah Samson anatueleza katika matumizi ya kubebea watoto, kwa sasa wanawake wanao wabeba watoto wao kwa khanga mgongoni ni wachache sana zaidi vinatumika vikoi au vibebea watoto hata wanaojifungua wengi wanatumia baby ‘shoo’.
“Mimi sina khanga hata moja. Sioni umuhimu wake kwa sababu siwezi kujifunika nikiwa natoka kwenda mijini au nimetoka outing. Huwa natumia kikoi, na hata nikishinda nyumbani bora nitinge dera langu kuliko kujifunga khanga” alisema Leah.
Naye Rebecca Mlewa kutoka Pugu jijini Dar es Salaam anasema akivaa khanga anahisi watu wanamuona kama mshamba anapokuwa anatembea barabarani hivyo bora avae mavazi ya kisasa.
Kwa uzoefu wake wa kuuzaji wa khanga wa zaidi ya miaka 10, Maria Christopher anasema kwa sasa uuzaji wa vazi hili kwa wanawake wa mjini umepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Maria anayefanya biashara yake eneo la Kitumbini, Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam anasema watu wamekimbilia kwenye vijora, madera na vikoi na kutelekeza khanga jambo ambalo hata yeye anashangaa.
Maria anasema wanawake wasilisahau vazi hili la kiafrika lenye uzuri wa kipekee lililonakshiwa na maneno mazuri yenye ujumbe.
Anasema kutokana na ujumbe ulioandikwa unaweza ukawa unatumika hata mke na mume wanapogombana mke anaweza akavaa khanga iliyoandikwa ‘Ukiniona cha nini wenzio wanasema watanipata lini,’ mume akiona hili anashituka na kujirekebisha kama alikuwa anamakosa kwa mkewe.
“Nakumbuka kipindi nasoma niliwahi kupewa khanga na rafiki yangu ikiwa imeandikwa ‘Wawili wakipendana, adui hana nafasi’, Khanga hii niliishi nayo muda mrefu kwa sababu ilikuwa nikiangalia namkumbuka rafiki yangu,” alisema Maria
Usiache mbachao kwa msala upita,vazi hili ni la heshima mwanamke anapaswa kuwa nalo na kulitumia hivyo wasikimbilie mavazi mengine wakalisahau vazi la tamaduni yao.
Leave a Reply