Undani mchezo wa bao

Undani mchezo wa bao

BAO ni moja ya michezo migumu ulimwenguni kutokana na mahesabu yaliyosheheni wakati wa wakucheza mchezo huo, jambo ambalo linahitaji umakini na weledi wa hali ya juu katika uchezaji kwake.

Kila jambo lina utaratibu wake, Ili ufanikiwe kushinda mchezo huo lazima utambue namna ya kuanza kucheza kwa kufuata kanuni na taratibu zilizopangwa kwenye mchezo huo wa bodi ya jadi ya mankala, uliyochezwa katika sehemu nyingi za Afrika.

Asili ya mchezo huo huchezwa barani Afrika, hasa eneo kubwa la Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, Kenya, Comoro, Malawi hata maeneo mengine ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo pamoja na Burundi, ni maarufu zaidi katika jamii ya Waswahili hususani, Tanzania na Kenya.

Bao au bao la Kiswahili inamaanisha kuwa mchezo wa bodi ya Kiswahili unaohusiana na bodi ama bao la Zanzibar ni mchezo wa aina ya Mankala  unaochezwa na wachezaji wawili,  mmoja  kila upande mchezaji, mmoja anaitwa kaskazini na mwengine kusini.

Vile vile bao la kiarabu (Mchezo unaohusiana na "bodi ya waarabu", pia unajulikana kama (Hawalis) katika miaka ya 1820, Mshairi wa Kiswahili Muyaka bin Haji kutoka Mombasa alisherehekea mchezo huo katika shairi lake bao Naligwa. (4)

Aidha hapa nchini Tanzania hususani visiwani Zanzibar, wachezaji hushindana mara kawa mara na washindi huitwa mabingwa, huku aina nyingine za bao ni Sono ya kabila la Wagogo na Engesho ya Wamasai, huko nchini Malawi Mchezo huo hujulikana kama “Bawo” sawa na jina la Kiswahili la Yao.

Vilevile mashindano rasmi ya mchezo huo hufanyika nchini Tanzania, Zanzibar, Lamu (Kenya) pamoja na Malawi kwa Tanzania bara na Zanzibar huwa kuna jamii za Mchezo huo ambapo mnamo mwaka 1966, chama cha bao kilianzishwa rasmi.

Hata hivyo bao inajulikana kuwa Mankala maarufu kwa suala la ugumu na kina cha kimkakati na imeongeza hamasa kwa wasomi wa taaluma kadhaa, pamoja na nadharia ya mchezo nje ya Afrika, wataalamu wa Michezo na Wanasaikolojia huvutiwa sana na mchezo huo.

Namna ya kucheza bao

Bao linachezwa kwa kutumia kipande cha mbao ambacho huchimbwa mashimo (32) yaliyopangwa kwa mistari minne tu, mashimo mawili ya upande wa juu yanamilikiwa na mchezaji anayeitwa kaskazini, mashimo mawili ya chini yanamilikiwa na mchezaji anayeitwa kusini.

Pia mistari miwili ya mashimo ya katikati inaitwa mistari ya mbele au ya ndani, mistari miwili ya mashimo ya nje inaitwa mistari ya nyuma au ya nje.

Shimo la tano kutoka upande wa kushoto kwenda kulia kwa mchezaji la kila mstari wa ndani linaitwa nyumba na kwenye bao kadhaa mara nyingi hua lina umbo tofauti, kwenye bao kadhaa kuna mashimo mawili ya ziada ya kuhifadhia kete au namu au kombwe au vijiwe za wachezaji huitwa ghala mashimo haya yapo upande wa kulia wa kila mchezaji.

Katika bao la kiswahili, kila mchezaji hapo awali huweka mbegu 6 ndani ya nyumba, na mbegu nyingine mbili kwenye mashimo mawili mara moja kulia kwenye nyumba.

Aidha nchini Malawi mbegu zote zilizobaki huwekwa mkononi ,mbegu 8 huwekwa ndani ya nyumba hivyo basi  kila mchezaji ana mbegu 22 au 20 Mtawaliwa mwanzoni mwa mchezo ambapo  mbegu hizo zinawekwa  kwenye mchezo katika awamu ya kwanza ya uchezaji inayoitwa awamu ya namua.

Katika awamu ya namua, kila mchezaji anaanza hoja yake kwa kuanzisha moja ya mbegu alizonazo mkononi, mbegu lazima iwekwe kwenye shimo lililo tupu kwenye safu ya ndani ya mchezaji.

Historia ya Bao na Mwalimu Nyerere

Katika historia ya mchezo huo mtu muhimu ambaye hukumbukwa sana katika kuendeleza Utamaduni kupitia Michezo ya jadi ni Baba wa Taifa Hayati  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye anakumbukwa kwa kuendeleza utamaduni wa michezo ya jadi hapa nchini.

Vilevile Mwalimu alikuwa muasisi wa mchezo huo ambapo alibahatika kutunukiwa bao lililotengenezwa Ndanda mkoani Mtwara na kukabidhiwa kama zawadi yake kupitia mchezo huo. 

Miongoni mwa michezo ambayo Baba wa Taifa alikuwa akiiendeleza ni mchezo wa bao ambao alikuwa akiupenda na akiucheza vilivyo.

Mara nyingi Mwalimu alikuwa anapendelea kucheza bao akiwa nyumbani kwake Magomeni na watu mbalimbali walikuwa wakijuinga nae kwenye mchezo huo.

Sababu ambazo zilisababisha Mwalimu kuvutiwa na  kuupende mchezo huo ni kutokana na mazingira yanayoashiria urafiki na undugu zaidi  hasa kitendo cha kukaa pamoja kwenye mkeka na wachezaji wakiwa wamekaribiana huku wakitaniana na kupeana vijembe vya hapa na pale.

Bao kufananishwa na ngoma ya Ndalandala

Katika kipindi hicho cha miaka ya nyuma mchezo huo ulikuwa ukifananishwa na ngoma ya makabila ya Wazaramo na Wandengereko iliyokuwa inaitwa ‘Ndalandala’ambayo ilikuwa ikichezwa sana na watu wa Pwani.

Kwenye ngoma hizo Wazaramo na Wandengereko walikuwa wakichapana bakora hadi kufikia hatua ya baadhi ya washiriki walikuwa wanakufa kutokana na ngoma hiyo.

Kwakuwa Mwalimu alikuwa akipambana kikamilifu na mila potofu aliamua kuupiga marufu kabisa mchezo huo na kuhakikisha kuwa hauendelei katika jamii.

Mchezo wa bao ndiyo mchezo pekee wa asili ambao bado unaendelea na kuenziwa na mababu pamoja na wazee wetu hadi sasa ambapo utakuta kwenye vijiwe mbalimbali vya kahawa watuwazima wakiwa wanaendeleza kucheza mchezo huo.

Ama kwa hakika bado ule usemi wa “vyakale ni dhahabu” utaendelea kuenziwa siku hadi siku kutokana na asili pamoja na kuenzi mambo mbalimbali ambayo ni muhimu kwenye jamii.

Hivyo basi michezo ni afya na muhimu kujifunza kwani huongeza maarifa, mtazamo na fikra yakinifu.

Usikose kusoma jarida la Mwananchi Scoop, kila siku ya Ijumaa ili uweze kutambua historia za michezo mbalimbali, nakutakia wikiendi njema!

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post