Huyu ndiye  Denzel Washington usiyemfahamu

Huyu ndiye Denzel Washington usiyemfahamu

Mwigizaji wa Marekani Denzel Washington ametangaza kustaafu kuigiza huku akiweka wazi kuwa Black Panther 3 itakuwa moja ya filamu za mwisho kucheza.

Pia kabla ya kustaafu kwake mwigizaji huyo amesema atafanya filamu nyingine kama Gladiator 2, na Othello. Kwa miaka zaidi ya thelathini Denzel amekuwa na ushawishi mkubwa katika tasnia ya filamu, akifanya kazi kama mwigizaji, mwelekezi, na mtayarishaji. Amekuwa akionesha umahiri wake, akicheza uhusika mbalimbali kuanzia uhusika wa kihistoria hadi wa kisasa

Denzel alizaliwa Desemba 28, 1954, katika jiji la Mount Vernon, New York, Marekani. Ni mtoto wa pili kati ya watoto watatu. Baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari, alienda kusoma kwenye Chuo cha Fordham, kilichozalisha waigizaji wengi maarufu. Huko alijifunza sanaa ya uigizaji, na alipohitimu mwaka 1977, alianza kufanya kazi katika tamthilia za jukwaani kabla ya kuhamia Hollywood.

Alijulikana kwa mara ya kwanza miaka ya 1980 katika vipindi vya televisheni. Filamu yake ya kwanza kubwa ilikuwa 'Cry Freedom' (1987), ambapo alicheza kama Steve Biko, kiongozi wa kupigania haki za raia nchini Afrika Kusini. Hata hivyo, filamu ya Glory (1989) ndiyo ilifanya dunia ilijue jina lake alicheza kama Private Silas Tripp katika filamu hiyo ya kivita, ambapo alishinda Tuzo ya Academy ya Mwigizaji Bora Mdogo.

Mafanikio yake yaliendelea kuongezeka katika miaka ya 1990. Kwenye filamu kama 'The Hurricane' (1999), ambapo alicheza kama Rubin 'Hurricane' Carter, mchezaji wa ngumi aliyetiwa jela kwa kosa ambalo hakulifanya, ilimfanya kuwa mmoja wa waigizaji maarufu duniani. Pia 'Malcolm X' (1992), ambapo alicheza kama kiongozi wa harakati za haki za kiraia. Malcolm X, ni moja ya kazi bora ya uigizaji katika historia ya filamu na kumfanya atunukie tuzo nyingi

Katika miaka ya 2000, Denzel aliigiza katika filamu kama 'Training Day' (2001), ambapo alicheza kama mwendesha mashitaka, Alonzo Harris. Kutokana na uhusika huo alishinda Tuzo ya Academy ya Mwigizaji Bora. Aidha filamu nyingine ni 'Inside Man' (2006) na 'American Gangster' (2007), ambapo alicheza kama mfanyabiashara wa dawa za kulevya, Frank Lucas.

Mbali na filamu hizo ambazo alicheza, ameongoza baadhi ya filamu kama 'Antwone Fisher' (2002) na 'Fences' (2016), ambapo pia alicheza na kushinda Tuzo ya Golden Globe kwa uigizaji wake.

Aidha anajulikana kwa kuunga mkono miradi ya kijamii na kisiasa, hasa kuhusu haki za kiraia na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi. Washington amekuwa mfano wa kuigwa na wengi kutokana na mafanikio yake na mchango wake katika tasnia ya filamu, huku akiwa na hadhi kubwa ndani na nje ya Marekani.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags