Jennifer Lopez apata kiota kipya baada ya talaka

Jennifer Lopez apata kiota kipya baada ya talaka


Mwimbaji wa Marekani, Jennifer Lopez a.k.a J.Lo anaripotiwa kununua nyumba mpya yenye thamani ya Dola18 milioni ikiwa ni miezi michache baada ya kukamilika kwa mchakato wa talaka kutoka kwa aliyekuwa mumewe Ben Affleck.

Kwa mujibu wa People, mkali huyo wa kibao, On The Floor (2011) alianza kutafuta nyumba mpya kufuatia ndoa yake na Affleck kuanza kuyumba hapo Aprili 2024 na sasa amepata makazi mapya huko Los Angeles.

Lopez na Affleck, muigizaji aliyeshinda tuzo Oscar mara mbili, mchakato wa talaka yao ulikamilika Januari mwaka huu ikiwa ni takribani miezi minne tangu kuwasilisha hati ya kuivunja ndoa yao iliyodumu kwa miaka miwili.

Taarifa za Lopez kununua nyumba mpya zinakuja wakati jumba lao la kifahari la Beverly Hills bado lipo sokoni tangu Juni 2024 kwa bei ya Dola68 milioni lakini hadi sasa hakuna mteja alijitokeza kununua mali hiyo.

Mei 2024 ilielezwa kuwa Affleck alikuwa akiishi katika nyumba ya kupanga maili chache kutoka kwenye jumba lao la kifahari huku akitengeneza filamu yake ya The Accountant 2, wakati huo Lopez akiishi pekee yake katika nyumba hiyo.

Chanzo kimoja kilidokeza kuwa Affleck hakuipenda nyumba hiyo kutokana ipo mbali na watoto wake watatu aliowapata katika ndoa na aliyekuwa mkewe, Jennifer Garner ambaye walidumu tangu mwaka 2005 hadi 2018.

Kulingana na Wall Street Journal, jumba hilo lenye futi za mraba 38,000, lina ukumbi wa sinema, saluni, bwawa la kuogelea, viwanja vya michezo, vyumba 12 vya kulala, bafu 24, majiko 15, eneo la kuogesha magari 15 n.k.

Wawili hao walinunua jumba hilo kwa Dola60 milioni hapo Juni 2023 baada ya kufunga pingu za maisha huko Las Vegas Julai 2022 ikiwa ni miaka 18 tangu walipoachana kwa mara ya kwanza.

Ikumbukwe uhusiano wao ulianza mwaka 2002 hadi 2004 walipotengana, na kwa asilimia kubwa uliandamwa sana na magazeti ya udaku kitu ambacho Lopez alikuja kusema hakukipenda kwa jinsi mambo yao yalivyokuwa yakiwekwa hadhani.

Kutokana na kuandamwa na vyombo vya habari, waliamua kuaishirisha harusi yao iliyopangwa kufanyika Septemba 14, 2003 huko Santa Barbara na ndoa hiyo haikufungwa tena hadi walipoachana.

Hata hivyo, baada ya miaka 18 wakarudiana, hiyo ilikuwa ni Julai 2021, kisha wakachumbiana kwa mara ya pili hapo Aprili 8, 2022 na kufunga ndoa Julai 16, 2022 ikiwa ni ndoa ya nne kwa Lopez ambaye awali aliolewa na Ojani Noa, Cris Judd na Marc Anthony.

Wawili hao waliocheza pamoja filamu, Gigli (2003) na Jersey Girl (2004), walionekana pamoja mara ya mwisho walipohudhuria mchezo wa mpira wa vikapu pamoja na mtoto wa Affleck, Samuel, 12, huko Santa Monica, California hapo Juni 2 mwaka uliopita.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags