Kumekuwa na maoni kadhaa kutoka kwa wadau wa muziki kuhusu migogoro katika kazi hiyo. Wapo wanasema bifu zinakuza muziki kwa sababu zinasababisha ushindani katika gemu, lakini pia wapo wanaopinga wakisema bifu hazina mchango wowote kwenye muziki wasanii wakae meza moja na kuijenga nyumba moja ya muziki wa Bongo fleva.
Katika safari ya muziki wa Bongo Fleva zimetokea bifu nyingi kati ya wasanii mpaka kupelekea kutoleana ngoma 'Diss' na kurushiana maneno. Je ipi ilikuwa bifu tishio kati ya hizi.
Diamond Platnumz na Alikiba, bifu ya mastaa hawa lilianza tangu 2010 baada ya Diamond kuingia kwenye muziki na kukiwasha akaanza kushindanishwa na Alikiba ambaye alimtangulia kwenye muziki kwa zaidi ya miaka 5
Bifu hilo lilipelekea mpaka wawili hao kutokuwa na maelewano kwa mujibu wa Alikiba alipokuwa akifanya mahijiano kwenye kipindi cha The Sporah Show alisema kuwa Diamond alifuta verse yake kwenye wimbo wa ‘Lala Salama’ ambao ilibidi washirikiane.
"Nilienda kumtembelea producers wangu nikamkuta Diamond nikakuta amesha rekodi wimbo wa ‘Lala Salama’ akaniambia imba chochote nikaimba wimbo nikaja kusikia wimbo umeshatoka kile kipande changu ameimba yeye," alisema Kiba
Dizasta na Rapcha, bifu kati ya wakali hawa wa Hiphop lilianzia kwenye ngoma ya Rapcha ' Stori Nyingine' iliyotoka Desemba 31, 2022, aliyowa-diss rappers kama Lunya, Dizasta na wadau kama Babu Tale. Kwenye wimbo huo Rapcha alimpitia Dizasta akisema rapa huyo alilike post inayom-diss Twitter.
"All My life I keep it 99 rasta kama kuna love hauwezi tia like kwenye twitt inayonidiss rasta nilidhani tuko peace mpaka siku nilipokuta kwenye twitt inayo ni diss nikakuta like ya Diszasta," aliimba Rapcha kwenye Stori Nyingine.
Dizasta naye hakupoa akaibuka na kujibu kupitia ngoma ya Best Friend ngoma yenye takribani dakika nane lakini alisema sio diss alichojaribu ni kumuelewesha Rapcha kwa kile kilicho tokea.
Rapcha alirudi na ngoma nyingine ya 'Nuclear Story' ambayo ilikuwa ni Direct Diss kwa rapa Dizasta. Naye Dizasta hakupoa akaachia diss ya takribani dakika 11 'Tribulation', Rapcha hakujibu tena na amekuwa akikana kutoulizwa tena kuzungumzia swala hilo.
Young Killer na Young Lunya, miamba hii mingine ya hiphop ilikwaruzana sana kwenye bifu lililoanza rasmi 2019 baada ya Lunya kuachia ngoma yake ya Free Style Session 2 ambapo moja ya mstari wake alimpitia Young Killer akisema kwa kejeli "Youngkiller ni Rapa fulani noma kiroho safi"
Lakini pia, bifu hilo lilipamba moto baada Lunya kuachia Freestyle Session 5 ambapo Killer aliona mazoea yamezidi na kujibu kwa diss ya Free Style Session 6. Ambapo humo ndani alimralua Lunya kwa moja ya mstari wake aliimba "Hapa labda zikuokoe dua Country kakupika kabla hujaiva kakupakua mimi wa kitaa muulize babuu anajua".
Diamond Platnumz na Harmonize, bifu hii ilihusisha zaidi masuala ya kikazi kati ya wawili hao ambapo maelewano yao mabovu yalianza baada ya Konde kuhitaji kuondoka kwenye lebo ya WCB ili ajitegemee.
Bifu hilo liliendelea mpaka kuanza kutoleana ngoma za vijembe kati ya wasanii hao. Japo kwa hivi karibuni wamekuwa wakikutana wanagonga tano.
Mr. Nice na Dudu Baya, wawili hao walionesha kuwa na bifu zito baada ya Dudu Baya kumtwanga makonde Mr Nice mbele ya mashabiki wake na kufikishana mahakamani.
Ambapo Dudu baya aliswekwa rumande. Hata hivyo, wawili hao katikati ya mwaka 2015 walimaliza tofauti zao huku picha yao wakiwa pamoja ikizua gumzo kwenye mitandao ya kijamii.
Nay Wamitego na Madee, bifu la wakali hawa lilianza kama utani kwa kugombania hadhi ya nani Rais wa Manzese ambapo kila mmoja alidai kuwa na haki hiyo. Kiasi cha wawili hao kutajwa kufanyiana fujo hata kwenye shoo.
Hata hivyo, walipatana mwaka 2014 na kuwashangaza watu kwa kupeana lifti na kupiga picha wakiwa kwenye gari moja. Lakini miaka ya mbele bado kila mmoja aliendelea kujiita Rais wa Manzese kiasi cha kuacha maswali mengi kuwa wawili hao bado haziivi.
"Mi ndo Rais wa Manzese yule tozi kasanda Manzese mikono juu naiongoza kamanda" aliimba Nay na Tozi aliyetajwa hapo ni Madee akiambiwa amesanda.
Matonya na Tunda Man, bifu hili lilikuwa ghafla wakati huo Matonya ndiyo alikuwa anawika ambapo Tunda Man aliibuka na madai ya kuwa yeye ndiye mtunzi wa nyimbo kibao za Matonya ikiwa ni pamoja na Hitsong ya 'Vaileti' jambo ambalo Matonya alilipinga na kusababisha bifu zito baina yao.
Hata hivyo, bifu hilo lilisuluhishwa kwenye vyombo vya habari na kuisha mwishoni mwa mwaka 2015 baada ya wawili hao kufanya wimbo wa pamoja unaokwenda kwa jina la Ugomvi.
Bob Junior na Diamond Platnumz, Bob Junior ambaye ni mtayarishaji wa muziki na msanii aliyemtambulisha Diamond kwenye gemu, aliingia bifu na msanii huyo kiasi cha kuacha kufanya naye kazi.
Bifu hilo likikolezwa na vita ya nani Rais wa Sharobaro. Hata hivyo, wawili hao walionesha kumaliza tofauti zao katika shoo ya Zari All White Party iliyofanyika Mei mwaka 2015 ambapo Bob Junior alijumuika nao na kufurahi pamoja na kuonesha kuwa hawana bifu tena.
Bifu jingine ambazo nazo zilitikisa na kuacha historia lakini zilikuja kusuluhisha ni pamoja na Nasma Kadogo na Khadija Kopa, Inspector Haroun na Juma Nature, O’Ten vs Afande Sele, Solo Thang na Afande Sele na nyingine nyingi.

Leave a Reply