Kabla ya Bongo Fleva Linah aliimba kwaya

Kabla ya Bongo Fleva Linah aliimba kwaya

Staa wa Bongofleva, Linah Sanga alianza kutamba baada ya kipaji chake kunolewa na Tanzania House of Talents (THT). Kwa sasa takriban miaka 15 bado anaendelea kutoa burudani kwa mashabiki ingawa sio kwa kasi ile ya mwanzo.

Kama ilivyo kwa wanamuziki maarufu duniani akiwemo Celine Dion na Whitney Houston, naye Linah alianza kuimba kanisani kisha akaibukia katika muziki wa kidunia (secular artist). Kwa Bongo ikiwa ni sawa na Ruby, Vanessa Mdee, Lady Jaydee na kadhalika.

Linah a.k.a Ndege Mnana ameshinda tuzo moja ya muziki ya Tanzania (TMA) kati ya mara tano alizochaguliwa kuwania na sasa ni miongoni mwa wanamuziki wakali wa kike waliowahi kutokea Bongo. Fahamu zaidi.

Pale THT Recho ndiye alitakiwa kuwa wa kwanza kutoka kimuziki, ila ikashindikana baada ya kuumia mkono, hivyo THT wakaanza kumtoa Linah ambaye alikuja kushinda TMA 2011 kama Msanii Bora Chipukizi. Na baada ya Linah waliofuata kushinda kipengele hicho katika TMA ni Ommy Dimpoz (2012), Ally Nipishe (2013), Young Killer (2014), Barakah The Prince (2015), Rapcha & Phina (2021) na Kontawa & Gachi (2022).

Kufuatia Linah kufanya vizuri ndipo Recho akatoka na nyimbo zake kama Kizunguzungu (2011), Upepo (2012) na Nashukuru Umerudi (2013), kisha kushinda TMA 2013 kama Msanii Bora wa Kike.

Wakiwa wanapambana kutoka kimuziki, Recho aliondoka kwa shangazi yake na kwenda kupanga. Baadaye akahamia gheto kwa Linah ambaye walikuja kushirikiana katika wimbo wao, Same Boy (2018).

Linah ndiye msanii wa kwanza wa kike kutoka Tanzania kufanya kazi na Director wa Afrika Kusini, Godfather, huku AY akiwa ndiye msanii kwanza kwa ujumla kisha wakafuata wengine kama Diamond Platnumz, Shetta na Rayvanny.

Godfather ndiye amefanya video ya wimbo wa Linah, Ole Themba (2014) kwa gharama ya Dola30,000, wastani wa Sh81 milioni kwa sasa ikiwa ni video ya kwanza ya Linah kuwekeza fedha nyingi.

Ukichana na Linah, msanii mwingine Bongo aliyefanya video kwa Godfather kwa gharama kubwa ni Diamond Platunmz ambaye alilipa Dola40,000 ili kufanya video ya wimbo wake, Nana (2015) akimshirikisha Mr Flavour kutoka Nigeria.

Wimbo wa Linah, Ole Themba (2014) ambao umetengenezwa na Uhuru kutoka Afrika Kusini ulipaswa kuwa sehemu ya wimbo wa Davido na Mafikizolo, Tchelete (2014) ila ikashindikana hivyo kila mmoja ukatoka kivyake.

Kwa mujibu wa Linah, nyimbo tatu ambazo zilibadilisha kabisa maisha yake ya muziki kwa kumpatia umaarufu, ni Atatamani (2010), Bora Nikimbie (2010) na Lonely (2011).

Linah anashika nafasi ya tano kati ya wasanii wa kike wa Bongofleva wenye wafuasi (followers) wengi katika mtandao wa Instagram akiwa ametanguliwa na Hamisa Mobetto, Shilole, Nandy na Vanessa Mdee.

Kipande anachoimba Linah katika wimbo wa Mwana FA, Yalaiti (2011) ni kutoka katika wimbo wa Siti Binti Saad wa Zanzibar unaokwenda kwa jina hilo hilo ambao pia Bi Kidude naye aliurudia.

Hata hivyo, Mwana FA ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo aliamua kuurudia wimbo huo baada ya kusikia toleo (version) la Malika wa Mombasa, Kenya na kukoshwa nalo hadi kufikia hatua ya kumpa mtoto wake wa kwanza jina la Malika.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags