Ukweli kuhusu mayai ya kware

Ukweli kuhusu mayai ya kware

KUMEKUWA na misuguano kutoka kwa madaktari, wafugaji na watumiaji wa mayai ya kware kwamba huenda yanaweza kutibu magonjwa mbalimbali na wakati mwingine yasitibu magonjwa hayo.

Wapo baadhi ya madaktari ambao wanasema huenda mayai hayo yanatibu lakini kutokana na aina ya ufugaji wa ndege hao hivi sasa, unatia mashaka na kwamba inawezekana wakawa wanaongeza magonjwa na sio kutibu.

Awali, watafiti wa Uingereza wamesema yai la kware liitwe "Super- Food" kutokana na kuwa na faida nyingi sana katika afya ya binadamu na hata kusaidia kuushinda utapiamlo.

Pia wanadai kuwa yai la kware ni moja kati ya vyakula vyenye virutubisho vingi muhimu na kwamba kila mtu anatakiwa ale moja kwa siku.

Kwa mujibu wa wataalamu wa tiba za asili, walidai kuwa mayai ya kware yanaweza kuimarisha kinga ya mwili na kuongeza ubora wa damu na magonjwa ya shinikizo la damu.

Wanadai kuwa ili kuboresha kinga ya mwili, utumiaji wa mayai 60 unahitajika ambapo mwanzo mtumiaji anatakiwa kutumia mayai matatu na baadaye mayai matano kwa siku.

Hata hivyo, Daktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha maabara, Matandala Luhongedzo anasema kuwa mayai ya kware hayana tofauti na mayai ya kuku na kwamba kinachojitokeza sasa ni biashara tu.

Anasema mayai ya kware huenda yanaweza kutibu magonjwa mbalimbali lakini endapo mgonjwa hata fuata ushauri wa daktari anaweza asipone magonjwa yanayomsumbua.

Dk Luhongedzo anasema mara nyingi magonjwa waliyonayo binadamu husababishwa na tabia na kwamba hata kama watatumia mayai hayo kwa kiasi gani, hawezi kutibu endapo hata acha tabia zake.

“Kwa mfano, magonjwa ya shinikizo la damu mara nyingi husababishwa na msongo wa mawazo ambao unatokana na tabia ya mtu, hivyo kama hata acha tabia yake ya kuwaza mambo ambayo sio sahihi, hata akila mayai 500 hawezi kupona,’’ anafafanua.

Pia anasema kuwa kwa upande wa kinga ya mwili ni kwamba binadamu mara nyingi anazaliwa akiwa na kinga ya mwili na kueleza kuwa inaweza kupungua kutokana na sababu mbalimbali hivyo suala la kula mayai pekee halisaidii kuongeza kinga hiyo.

Anaongeza kuwa ni vyema kwa mgonjwa ambaye anataka kutumia mayai ya kware kama tiba, kuhakikisha anaacha tabia zote zinazoashiria magonjwa.

Anasema kwa mgonjwa wa Virusi vya Ukimwi anatakiwa kufuata ushauri wa daktari kwani mayai ya kware pekee hayawezi kuongeza CD 4 za mwili wake.

“Hii ni biashara tu kwani kila mtu anatakiwa kupata soko kulingana na bidhaa anayoiuza. Ni lazima wawashawishi watu kwamba wakila mayai ya kwale wanaweza kupona magonjwa yao,’’ anasema na kuongeza

“Hatumzuii mtu yeyote kula mayai hayo lakini wanatakiwa kufuata ushauri wa madaktari pamoja na kuacha tabia ambazo zinachangia magonjwa hayo,’’

Anasisitiza kuwa wagonjwa wote ambao wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali wanatakiwa kula mayai kuboresha afya zao na sio kwamba mayai pekee ndio yatawasaidia wagonjwa kupona magonjwa yanayowakabili.

Kwa upande wake, Ofisa mahusiano wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Gaudencia Simwanza anafafanua kuwa kwa mujibu wa masuala mbalimbali ya kiafya, kila binadamu anatakiwa kula mayai mawili kwa siku.

Anasema mwili wa binadamu unahitaji mayai kuongeza protini na Vitamin lakini sio kwa kula mayai mengi kwa siku moja ama kwa wiki.

Simwanza anasema mayai ya kware hayana tofauti na mayai ya kuku wa kisasa kutokana na tabia za ufugaji wake.

Anasema wafugaji wengi wanatumia vyakula ambavyo wanawapa kuku wa kisasa kitendo ambacho kinasababisha mayai hayo kutoka kwenye ubora kama yalivyo mayai ya kwae ya asili.

‘’Mtu mzima hatakiwi kula mayai zaidi ya mawili hivyo ratiba zinazotolewa na wafanyabiashara hao ni upotoshaji na kwamba wanatakiwa wasipotoshe umma,’’ anasema Simwanza.

Pia anaongeza kuwa ulaji kwa wingi wa mayai hayo, utasababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo moyo kufeli kutokana na wingi wa lehemu zilizopo katika mayai hayo.

Anasema pamoja na mambo mengine, mwanadamu anayekula mayai kwa wingi wanaweza kupata shinikizo la damu hivyo ni tofauti na wanayoyasema wafanyabiashara.

Anafafanua kuwa ni vyema kwa wananchi kufuata kanuni bora za kula ili kuwa na afya bora na kwamba kufuata wafanyabiashara wasemayo, yatasababisha kuwa na wagonjwa wengi.

Hata hivyo, katika baadhi ya taarifa zinaeleza kuwa kula mayai ya kware kwa afya njema, inashauriwa kuyala yakiwa mabichi.

"Watu wengi hawapendi kuyala yakiwa mabichi lakini kuyafanya yawe matamu ni kuchanganya na maziwa na asali.

Mayai ya Kware yanachukuliwa kama ni tiba namba moja ya asili.

Madaktari wakichina wajadi wamekuwa wakitumia mayai ya kware katika miaka iliyopita na yamewapa matokeo mazuri kwa muda wote huo.

Wataalamu hao wa tiba za asili wanathibitisha yai hilo kuwa na faida kimatibabu kwa wagonjwa wa msongo wa mawazo, wanaosumbuliwa na kuchelewa kwa mzunguko wa chakula tumboni, vidonda vya tumbo, matatizo ya maini, pumu,  aina za matatizo ya moyona mapafu.

Kwa mfano, Gazeti la Lishe na Sayansi ya Chakula liliandika namna watafiti wanasisitiza umuhimu wa nafasi ya yai la kware katika kinga nzuri ya mwili, kupunguza unene na kutunza mwili wa binadamu.

Dokta Carriel Ruxton ambaye ni  Kiongozi wa utafiti anasema yai la kuku lina nafasi ya kiafya kwa mwili wa binadamu, utafiti huo uliainisha kwamba yai la kuku halina kalori za kutosha, bali yana protini na vitamini nyingine muhimu sana kwa binadamu kama Vitamini D na B12.

Inadaiwa kuwa mayai ya kware yamethibitishwa kuwa ni chanzo kikuu cha vitamin A, B1, B2, B6, B12 na Vitamin D pamoja na kuwa na madini ya chuma, zinki, shaba na virutubisho vingine.

Pia inaelezwa kuwa mayai hayo yana amino asidi ambayo yanaliwezesha yai hilo kuwa chakula muhimu kwa lishe ya binadamu.

Aidha, mayai hayo yanaelezwa kuwa na faida wakati wa ujauzito na unyonyeshaji wa mtoto. 

Inadaiwa kuwa matumizi ya mayai ya kware huimarisha mwili wa mama kabla na baada ya kujifungua pamoja na baada ya kufanyiwa upasuaji na matibabu yanayohusisha mashine za mionzi kama X-Ray.

Pia huimarisha akili na mwili wa mtoto pamoja na kumsaidia mama kuimarika baada ya kujifungua. 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post