Mwimbaji wa Afrika Kusini, Tyla, 22, hivi karibuni ameshinda tuzo ya MTV Video Music Awards (VMAs) 2024, mafanikio haya ni somo lingine kwa staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz, 34, baada ya tambo zake kwenda kwa washindani wake Afrika.
Tuzo hizo zilizofanyika katika ukumbi wa UBS Arena huko New York, Marekani hapo Septemba 11, Tyla alishinda kipengele cha ‘Best Afrobeat’ kufuatia kufanya vizuri na wimbo wake, Water (2023).
Ikumbukwe Tyla anayetamba na kibao chake, Truth or Dare (2024), alizaliwa Januari 30, 2002 huko Johannesburg, Afrika Kusini na kusoma sekondari ya Edenglen walipohitimu mwaka 2019, kisha kujiunga na chuo kusomea uandisi madini.
Hata hivyo, alikatisha masomo na kujikita katika muziki baada ya kujifunza mengi kwa Rihanna na Aaliyah, aliachia wimbo wake, Getting Late (2021) akimshirikisha Kooldrink na punde tu Epic Records walimsaini na ukawa mwanzo wa mafanikio yake makubwa.
Ushindi wa Tyla katika MTV VMAs 2024 unamfanya kuzidi kuwa msanii tishio Afrika na aliyepata mafanikio makubwa zaidi mwaka huu, hivyo kupata fursa ya kumketisha chini Diamond na kumfunda jinsi huu mchezo unavyochezwa.
Diamond anafundwa baada ya kujigamba kuwa amefanikiwa kuwaingiza kwenye mfumo wasanii wa Nigeria, yaani kuwashinda kufuatia kufanya vizuri na wimbo wake, Komasava (2024) aliowashirikisha Khalil Harisson na Chley kutoka Afrika Kusini.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba kwa mwaka huu Tyla ndiye amewaingiza kwenye mfumo wasanii wa Nigeria maana ameshinda tuzo tatu kubwa duniani mbele yao, tuzo hizo ni Grammy, BET na MTV VMAs.
Tyla alishinda tuzo ya Grammy 2024 katika kipengele cha ‘Best African Music Performance’ baada ya kuwabwaga wasanii wa Nigeria ambao ni Arya Starr, Asake, Burna Boy na Davido.
Ushindi huu ni kama aliwapiga na kitu kizito maana walilalamika sana katika mitandao wakidai Davido ndiye alistahili baada ya kubamba na wimbo wake, Unavailable (2023), huku wengine wakisema waandaaji wa Grammy walimtumia kisha kumtelekeza.
Wakati maumivu bado hayajapoa, Tyla akapiga tena kama Miso Misondo, ni kufuatia kushinda tuzo mbili za BET 2024 mbele ya hao hao Wanigeria na kuandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika kufanya hivyo ndani ya msimu mmoja.
Tyla alishinda kipengele cha ‘Best International Act’ akiwabwaga Asake (Nigeria), Aya Nakamura (Ufaransa), Ayra Starr (Nigeria), Bk’ (Brazil), Cleo Sol (Uingeza), Focalistic (Afrika Kusini) na Karol Conka (Brazil).
Pia akashinda kile cha ‘Best New Comer’ ambacho alikuwepo Ayra Starr wa Nigeria ambaye alivuma zaidi Afrika na kibao chake, Rush (2022) chini ya Mavins Records.
Utakumbuka hadi sasa wasanii wa Afrika walioshinda tuzo nyingi za BET kwa muda wote ni Burna Boy na Wizkid kutoka Nigeria ambao kila mmoja ana nne, hivyo Tyla ametuma salamu kwao kuwa anakuja kama Squeezer na Juma Nature.
Miezi michache mbele Tyla anashinda MTV MVAs 2024 akiwabwaga tena Wanigeria kibao akiwemo Ayra Starr ft. Giveon (Last Heartbreak Song), Burna Boy (City Boys), Chris Brown ft. Davido & Lojay (Sensational) na Tems (Love Me JeJe).
Ushindi huo huo umepelekea Tyla kuandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika kushinda tuzo tatu kubwa duniani (Grammy, BET na MTV MVAs) ndani ya miezi nane pekee!.
Je, hadi hapo kati ya Diamond na Tyla nani kawaingiza Wanigeria katika mfumo kwa mwaka huu?, kumbuka tuzo zote hizo alizoshinda Tyla, Diamond hajawahi kushinda hata moja!, hivyo hana budi kutulia na kufundwa na mtoto huyo wa 2000.
Kuna mashabiki husema tuzo sio kipimo cha ukubwa wa msanii au kukubalika kwa kazi zake maana tuzo zinaandaliwa na binadamu hivyo makosa yanaweza kuwepo kama upendeleo lakini mimi nasema kwa dunia ya sasa tuzo ni lazima.
Mathalani, ukiachana na vipaji vyao uwanjani, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wanatajwa kuwa wachezaji bora kuwahi kutokea kutokana na makombe na tuzo kubwa kama Ballon d’Or walizoshinda, bila hivyo hata Romelu Lukaku naye ni mchezaji bora.
Mbali na tuzo, eneo lingine Tyla analompa somo Diamond ni katika chati kubwa za muziki duniani, ni wiki chache zimepita tangu mashabiki wa Diamond kushingilia sana baada ya wimbo ‘Komasava’ kuingia Billboard U.S Afrobeats Songs.
Wakati Diamond akiingia kwa mara ya kwanza katika chati hizo na kushika namba 39, yeye Tyla kupitia wimbo ‘Water’ alikuwa namba moja kwa wiki 43, na wimbo huo ulishaingia Billboard Hot 100, chati ambayo Diamond hajawahi kuingia.
Tyla kawa namba moja Billboard U.S Afrobeats Songs kwa wiki zaidi ya 40 mbele ya wasanii wa Nigeria ila hajawahi kusema amewaingiza kwenye mfumo, zaidi anawapongeza kwa kufungua milango ya muziki wa Afrika na hata juzi katika MTV VMAs alirudia tena hilo.
Leave a Reply