Tumia muda wako vizuri upate mafanikio

Tumia muda wako vizuri upate mafanikio

Eebwana mambo vipi kijana mwenzangu, najua kuwa Jumatatu tulivu ya leo uko pouaa na unaendelea vema na majukumu yako ya kila siku.

Basi leo katika karia tutajuzana namna ya kutumia muda ili kuleta mafanikio makubwa katika malengo unayoyaweka kila siku katika maisha yako.

Kijana ili uweze kustawi unatakiwa kwenda na majira na nyakati, matumizi ya muda ndio yanayomfanya mtu afanikiwe, hivyo ukishindwa kuutumia muda wako vizuri lazima ushindwe, ndio maana kuna muda wa kuzaliwa na muda wa kufa.

Kuwa na saa haimaanishi una muda na sio kila mwenye saa ana muda, (tena wenye saa wengi ni mapambo tu hata hazitembei), wengi wana saa lakini hawana muda na kuna watu wana muda lakini hawana saa.

Nikujuze tu mafanikio katika maisha maana yake ni utumiaji mzuri wa muda katika mambo yanayoleta maendeleo chanya, kushindwa kufanikiwa maana yake ni utumiaji usio sahihi wa muda katika mambo yasioleta maendeleo katika maisha yako ya kila siku.

Ukifuatilia kwa umakini juu ya historia za maisha ya watu waliofanikiwa duniani kote utagundua ya kuwa ni watu wenye kujali kila sekunde, dakika, lisaa, masaa katika maisha yao, ndiomana wakawa wamefikia kwenye kilele cha mafanikio makubwa kwa haraka kila wanapoweka malengo yao.

Kwa hiyo kwa ujumla ni watu wenye kujali muda wakijua yakuwa mafanikio yao yako katika utumiaji mzuri wa muda wao.

Watu wengi hii leo hasa vijana waliopo vyuoni wamekuwa wakishindwa kufikia malengo yao kila wanapoyaweka si kwasababu hawawezi kuyafikia lahasha bali ni kwasababu ya kushindwa kutumia muda kwa usahihi kwenye mambo yanayoweza kuleta mabadiliko katika maisha yao.

Vijana hawa wamekuwa wakitumia muda mwingi katika mambo yasioleta hata robo ya badiliko katika maisha yao na wakibaki kulalamika kuwa maisha ni magumu pasipokujua tatizo ni namna bora ya utumiaji sahihi wa muda katika mambo yenye kuleta maendeleo.

Je wataka kujua kuwa huwa hufikii malengo yako kwa kuwa hutumii kwa usahihi muda wako? Wawezajiuliza siku ya leo tangu ulipoianza ni mambo gani ulioyapanga kuwa utayafanya na hukuyafanya? Na je sababu za kutoyafanya ni kweli zinaonyesha uzito wa kushindwa kuyafanya ukiangalia?

Je katika ratiba yako ya leo kwenye mambo unayohitaji kuyafanya je mambo hayo ulioyapanga yanachangia asilimia ngapi ya kufikia malengo ulioyaweka juu ya mafanikio katika maisha yako? Je ni jambo gani ambalo si lalazima kulifanya ukalifanya likavuruga ratiba ya malengo ulioyaweka siku ya leo? Hayo ni baadhi ya maswali ambayo waweza jiuliza na kujua kuwa kila unachokifanya kinaangalia namna unavyotumia muda.

Rafiki muda ndio sehemu ya mafanikio yako pasipo kujua namna nzuri ya kutumia muda utajikuta unalalamika kuwa kwanini hufanikiwi na kuanza kumtafuta mchawi wa mafanikio yako pasipokujua kuwa mchawi ni wewe mwenyewe.

Yawezekana hujajua sasa ufanye nini ili uwezetumia muda wako vizuri hebu jifunze mambo yafuatayo ili uweze jua namna ya kutumia mda wako kwa mafanikio mazuri.

Weka malengo yenye kuleta maendeleo katika maisha yako, jifunze kusema hapana katika mambo yasiyo na tija, Sema hapana pia fanya kwa umakini na kwa mda kitu ulichopanga kukifanya.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post