Simulizi 08

Simulizi 08

 

N a Innocent Ndayanse

MWEZI MMOJA BAADAYE 

DHAMIRA ya Panja alikuwa palepale; kumsaka Kipanga kwa udi na uvumba, kazi aliyoamini kuwa lazima ingefanikiwa. Ndiyo, aliamini kuwa lazima angefanikiwa kumpata, japo hakuyajua matokeo ya kukutana naye. 

Hata hivyo, kuhusu hilo hakupenda kukisumbua kichwa chake kulifikiria. Hii ilikuwa ni siku ya thelathini na tatu baada ya kuzidiwa kete na Kipanga. Na tangu aliporudi nyumbani hakuthubutu kutembea  mitaani mara kwa mara nyakati za mchana kwa kuhofia kukamatwa. 

Asubuhi hii, akiwa kitandani, alijaribu kupanga hili na lile katika kutekeleza kazi ya kumsaka Kipanga. Takriban kila alilolifikiria aliuona ugumu katika kulitekeleza. Hatimaye akaanza kukata tamaa. Na alikuwa na sababu ya kuanza kukata tamaa.

Jiji la Dar es Salaam ni kubwa na lina zaidi ya wakazi milioni tano. Ilikuwa ni ndoto ya mwendawazimu kujenga imani  ya mafanikio ya kumpata Kipanga kwa kupita hapa na pale, kitongoji hiki na kile, uchochoro huu na ule, gesti hii na ile na hata baa moja hadi nyingine kwa matumaini ya kufanikisha lengo hilo.

Na alitambua fika kuwa, hata kama angetumia njia nyingine katika msako huo, bado angehitaji kutumia fedha zisizo haba. Isitoshe, alijua kuwa Kipanga ana bastola, hivyo hata kama wangekutana uso kwa uso, Kipanga asingehitaji kutumia hata dakika moja kuamua afanye nini kama angesumbuliwa tena kuhusu mgawo wa pato la Kibaha. Angemlipua!

Bastola aliyoachiwa na Kipanga haikuwa na risasi hata moja na kwa hali hiyo, haikuwa na faida yoyote kwake kwa kipindi hicho. Alihitaji risasi walao tatu tu ili ajione yu mkamilifu. Azipate wapi risasi hizo? Hili lilikuwa jambo jingine gumu, jambo lililompasa kukisumbua tena kichwa katika kulipatia ufumbuzi.

Hata hivyo, kama aliyeoteshwa ndoto, wazo likamjia, wazo ambalo aliamini kuwa ni la kumtatulia tatizo hilo la upatikanaji wa risasi. Alimkumbuka mtu mmoja, askari wa Jeshi la Wananchi, aliyeitwa Masumbuko Kambi. Masumbuko alikuwa katika kambi moja kubwa jijini Dar es Salaam akiwa ni mtunza silaha.

Askari huyo alikuwa ni mtu wa matumizi makubwa na ya kifahari. Hakuwa radhi kuwa na upungufu wa pesa za starehe. Alizipenda bia, aliwapenda wanawake. Kila jioni alipotoka kazini,  aliripoti nyumbani na kuyavua magwanda ya kazi kisha akatinga nguo za ‘kutokea’ na kwenda katika baa maarufu zenye wateja wa kike ambao walikuwa tayari kwa yeyote na kwa wakati wote. Gari lake dogo aina ya Toyota lilikuwa likimrahisishia kazi ya kufika popote alipotaka kwenda.

Lakini ili azipate bia kila alipozihitaji, na kuwanasa wanawake wa aina yoyote na kwa wakati wowote, alilazimika kutumia pesa zisizo haba, tena  za ziada; siyo mshahara halali anaoutumikia kwa mwezi mzima! Alikuwa na mke mmoja na watoto watatu, wakiishi katika nyumba ya kupanga huko Mwenge. Je, kwa kutegemea mshahara huo angeweza kuihudumia familia yake mahitaji yote muhimu sanjari na kutanua mitaani kwa kugida bia na kubeba vimwana?

Isingewezekana. Hivyo alitumia mbinu zake za siri ili aweze kupata pesa za kutanulia mitaani. Kuuza risasi kwa siri kubwa na kupata pesa za harakaharaka, ilikuwa ni mbinu pekee iliyomrahisishia upatikanaji wa pesa, asilimia kubwa ya wateja wake wakiwa ni majambazi.

Panja alikumbuka kuwa siku moja aliwahi kwenda na Kipanga kwa Masumbuko na wakapata risasi kumi baada ya Kipanga kuongea naye faragha.

Kipanga na Masumbuko walifahamiana sana, tofauti na Panja ambaye japo siku ile walionana lakini hawakuwa na ukaribu kibiashara. Lakini hilo hakuliona kuwa ni kikwazo. Aliamini kuwa mbele ya pesa Masumbuko hatakuwa na kipingamizi chochote.

Ndipo alipokurupuka kitandani na kujifunga taulo kiunoni kisha akatwaa sabuni tayari kwenda bafuni.

Hilda aliyekuwa bado kitandani, alimtazama kwa mshangao na kumuuliza, “Wewe vipi?”

“Poa tu,” Panja alimjibu bila ya kumtazama.

“Imekuwaje? Mbona unakurupuka mapema ivo?”

“Nakwenda kuoga.”

“Njoo kwanza…”

Panja hakutii wito huo. Alijua alichoitiwa. Ni kilekile walichokwishafanya kabla ya alfajiri. Na kwa kawaida walikuwa na tabia ya kuikaribisha siku kwa kukifanya kitu hichohicho muda mfupi kabla ya kukiacha kitanda. Hata hivyo, hiyo ilikuwa ni kawaida, haikuwa sheria, kwa hali hiyo Panja aliendelea na safari yake ya bafuni.

Alipomaliza kuoga alivaa harakaharaka na kisha akaifungua saraka ya kabati ambako alihifadhi akiba ya pesa zake alizopata kutokana na kazi walizofanya na Kipanga siku chache zilizopita. Alipozihesabu akagundua kuwa mambo yanazidi kuwa mabaya. Akiba pekee iliyokuwamo zilikuwa ni shilingi 250,000 tu.

Hazikuwa ni pesa za kujivunia hata kidogo, ni wazi zingeteketea siku chache zijazo. Na ni katika akiba hiyohiyo alipaswa kutoa fungu la kwenda kumpa Masumbuko ili aweze kupata walao risasi tatu!

Hata hivyo, hakujali kupungua kwa kiwango hicho, alijali kupata risasi. Hivyo,  bila ya kuwaza zaidi alichomoa noti zenye thamani ya shilingi 60,000 na kuzipachika mfukoni. Akamtupia macho Hilda ambaye bado alikuwa amejilaza kitandani kihasarahasara.

“Natoka kidogo,” alimwambia. “Kuna tatizo lolote? Naweza kuchelewa kurudi.”

Hilda alijinyonganyonga, akijifunika shuka vizuri kisha akatupa swali, “Kwani unatarajia kurudi saa ngapi?” 

“Haitakuwa kabla ya saa sita.”

“Hujaniachia pesa ya kulipia umeme.”

“Shi’ngapi?”

“Elfu tano.”

“Chukua elfu kumi kwenye droo. Jingine? 

“Hakuna.”

Mwanamume alitoka. Saa 1.45 alikuwa akiteremka kwenye daladala katika kituo cha Mwenge. Akachepuka mtaa huu na ule hatimaye akafika kwa Masumbuko Kambi. Wakazungumza kibiashara, mazungumzo ambayo japo yalikumbana na kipingamizi kutoka kwa Masumbuko hata hivyo mwafaka ulipatikana.

Awali Masumbuko alitaka malipo ya shilingi 20,000 kwa risasi moja, lakini Panja alimbembeleza hadi akakubali kuchukua 50,000 kwa risasi tatu.

Itaendeleaaa……………………………………






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post