Waziri wa Elimu nchini Ufaransa, Gabriel Attal jana Ijumaa Oktoba 6, 2023, ametangaza kuwa nchi hiyo imelazimika kufunga shule saba ambazo kwa ujumla hupokea wanafunzi 1,500 baada ya kuvamiwa na kunguni.
Kwa mujibu wa DW Swahili, wiki hii, mamlaka ya Paris ilitangaza pia kufungwa kwa shule mbili kisa kikielezwa ni uvamizi wa wadudu hao, shule hizo moja wapo ikiwa iko Marseille na nyingine Villefranche-sur-Saone nje kidogo ya mji wa kusini mashariki wa Lyon.
Kutokana na ongezeko la uvamizi huo, Serikali ya Ufaransa imekuwa ikifanya vikao kadhaa kuchunguza idadi inayoongezeka ya visa vya kunguni, kipindi amchacho nchi hiyo inaandaa michuano ya Kombe la Dunia la Rugby, lakini pia itakuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki hapo mwakani.
Serikali mjini Paris imelazimika sasa kuingilia kati kupambana na kunguni hao, ambapo Ijumaa iliyopita, Waziri Mkuu wa Ufaransa Elisabeth Borne aliitisha kikao cha Baraza la Mawaziri kujadili namna ya kupambana na wadudu.
Waziri wa Usafirishaji Clement Beaune alikutana wiki hii na makampuni ya usafirishaji kubuni mpango wa kufuatilia na kunyunyizia dawa vyombo vya usafiri wa umma na, yumkini, kujaribu kupunguza wasiwasi wa nchi nzima uliochochewa zaidi na vyombo vya habari.
Leave a Reply