Serikali ipo mbioni kufanya mageuzi katika Sekta ya Utamaduni na Sanaa ili ijiendeshe kibiashara, izalishe ajira kwa wingi, iwe chanzo cha mapato ya fedha za kigeni pamoja na kuwa kinara cha uchangiaji wa pato la taifa nchini.
Katika kulifanikisha hilo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Damas Ndumbaro, leo Mei 23, wakati akitoa hutuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo 2024/25, amesema malengo yaliyopangwa ni kutekelezwa na mfuko ili Sekta ya Utamaduni na Sanaa ijiendeshe kibiashara, izalishe ajira kwa wingi, iwe chanzo cha mapato ya fedha za kigeni pamoja na kuwa kinara cha uchangiaji wa pato la taifa nchini.
Hata hivyo, amesema katika eneo hilo mfuko utaendesha programu ya mafunzo ya urasimishaji wa kazi za Utamaduni na Sanaa nchi nzima na walengwa wakiwa ni wasanii wachanga na chipukizi, huku programu hiyo ikiwa na hatua kuu nne.
“Moja, wasanii watapata mafunzo ya mada mbalimbali zitakazowasaidia kuendesha Sanaa kibiashara. Pili, wasanii waliofuzu katika hatua ya kwanza wataunganishwa na taasisi, wadau wa sanaa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya vitendo.
“Tatu, wasanii waliofuzu katika awamu ya pili wataunganishwa na wasanii waliofanikiwa katika maeneo husika kwa ajili ya kulelewa na kujifunza mbinu mbalimbali za kibiashara na nne na mwisho, wataunganishwa katika fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kupata mikopo kupitia mfuko wa Utamaduni na Sanaa,” amesema Ndumbaro.
Wanachosema wadau wa muziki
Akizungumza na Mwananchi Juma Hassani, ambaye ni mdau wa burudani kutoka Temeke jijini Dar es Salaam, amesema jambo hilo litakuwa neema kama kweli litafanyiwa utekelezaji.
“Ikiwa kama wanavyosema itakuwa jambo jema kikubwa ni utekelezaji ufanyike na siyo maneno, maana hawa wasanii wengi wachanga wanajaribu kuingia kwenye gemu ila mambo yanawashinda wanaamua kukata tamaa,” amesema.
Ismail Jumbe, mdau wa muziki kutoka Mwanza amesema hiyo inaonesha kwamba rasmi serikali imeanza kuthamini sanaa hasa ya muziki na kwa kufanya hivyo, itawezekana kuzalisha wasanii bora.
“Ubora wao utatokana na kutekeleza shughuli za sanaa kitaalamu. Programu hiyo itawawezesha wasanii chipukizi kuwa na stadi za biashara katika sanaa na hatimaye wakanufaika na shughuli wanazozifanya, tofauti na ilivyo sasa ambapo baadhi wanaimba ili wawe maarufu."
Kadhalika programu hii itazifanya ndoto za sanaa za vijana wengi ziwe hai, badala ya kupotea kama ambavyo imeshuhudiwa mara kadhaa,” amesema.
Naye Hawa Juma, mkazi wa Tabata amesema haoni kama suala hilo litaleta manufaa kwa wasanii wachanga kwani wapo ambao kwa sasa wanafanya vizuri lakini hawakuanzia kwenye mafunzo yoyote.
“Mimi naona ni kupoteza muda na kupiga pesa tu kwa sababu wapo baadhi ya wasanii leo wana majina makubwa lakini hawajapita popote, sasa hiyo programu wanayotaka kuianzisha hawaoni kama ni kupoteza muda na kupiga pesa inabidi kabla ya kuanza wafanye tafiti kwanza,” amesema.
Wanachosema wasanii chipukizi
Zulfa Mohamed Ibrahim ‘Xoul’ ambaye ni mwanamuziki wa Bongo Fleva amesema jambo hilo ni muhimu kwani litaenda kupunguza utapeli wanaofanyiwa wasanii chipukizi.
“Kwa upande wangu naona serikali imesikia kilio maana mimi kila nikiingia kwenye interview lazima nizungumzie kuhusiana na msanii ambaye ndiyo kwanza ameanza unajua msanii akikosa elimu ya mitandao anakuwa anadhulumiwa, anakosa haki zake za msingi.
“Mfano mimi mwenyewe hivyo vitu vimenikuta na siyo mara moja kwa hiyo ni jambo jema kwa kuwa wasanii tutapatiwa elimu na hao matapeli wataogopa.”
Mwanamuziki Abubakar Maulid maarufu kama Buki amesema ni jambo zuri kuwakumbuka wasanii chipukizi.
“Ni jambo zuri kuwakumbuka wasanii ambao wanakuja kwa sababu kizazi kipya ni wafalme wa baadaye watakaosimama kwa hiyo kuwakumbuka inakuwa jambo zuri,” amesema.
Aidha Peter Jovan, maarufu kama P Voice amesema jambo hilo linaongeza upendo kwa wasanii na kukuza muziki.
“Kwa upande wangu kama msanii ni jambo zuri na litatusaidia kuongeza upendo pamoja na umoja ili kuzidi kuisogeza mbele sanaa ya Tanzania.
“Pia itasaidia kutengeneza kazi ambazo zitaleta manufaa chanya kwa wasanii pamoja na kuitambulisha nchi kimataifa kitu ambacho kwa wenzetu tumeona wanafanikiwa sana kwa sababu ya umoja na mchango wa serikali kwenye kuhakikisha wanawawezesha wasanii wao kufanikiwa na kuitambulisha nchi zaidi,” anasema.
Leave a Reply