Mawazo ya biashara mwaka 2023

Mawazo ya biashara mwaka 2023

Oooooooh! Ni week nyingine tena katika segment yetu ya biashara, sisi bwana mwendo wetu ni ule ule mpaka mkubali kufanya biashara na kutokuwa tegemezi, yaani ni jinsi gani ninavyowapenda, nataka mchakalike, kuna kamsemo bwana kanasema kuwa, “pesa ya kutafuta kwa jasho lako ni tamu mno kuliko ya kupewa.”

Bwana katika nchi hii kuna fursa za biashara nyingi za kufanya sema ni vile tu tumechagua uvivu na kufanya mambo yasiofaa. Haya ungana nasi kujua mawazo mengine ya biashara ambayo watu wengi wamekuwa wakiyadharau.

 

  • Kilimo

Kutokana na hali nzuri ya hewa na mvua ya kutosha, baadhi ya maeneo unaweza kufanya biashara ya mazao mbalimbali kama vile mboga mboga nk.

Kama tunavyoelewa, kilimo sio lazima mazao bali pia unaweza kuwekeza katika ufugaji wa kuku na kuuza mayai katika sehemu mbalimbali haswa katika maeneo ya miji.

Hapa bongo watu wengi wanajishughulisha na kilimo cha mboga mboga na hiki sio lazima uwe na eneo kubwa na mvua, hapana unaweza kutumia eneo dogo lililoko nyuma ya nyumba yako na kuwezesha kupanda mboga na kuwauzia watu walio mtaani kwako na kwenye magenge yaliyo karibu na nyumbani kwako.

  • Uagizaji bidhaa na huduma za usafirishaji

Baadhi ya sehemu hakuna huduma za kuaminika za uagizaji na usafirishaji. Kampuni nyingi za uagizaji bidhaa na huduma za usafirishaji zinamilikiwa na wawekezaji walioko nje ya nchi.

Hali hii inaibua fursa kubwa kwa wafanyabiashara wa ndani wenye nia ya kujiingiza kwenye aina hii ya biashara. Sekta hii inatoa nafasi ambapo mwekezaji atahitajika kuliziba pengo hili kwa kutoa bidhaa na huduma zinazostahili.

Baadhi ya wateja katika biashara hii ni pamoja na taasisi za kiserikali za nchi pamoja na mashirika yatakayohitaji huduma hizi. Ili uwe na mafanikio katika biashara hii, unahitaji mtandao mpana (wa wateja na usambazaji) na pia uwe na ubunifu.

  • Biashara za mtandaoni

Kutoa huduma za kibiashara kwenye mtandao ni mojawapo ya biashara ambayo haiaminiki kabisa na changamoto kubwa ni ulaghai na utapeli. Hivyo basi, ili uwe mwenye mafanikio katika biashara hii, unahitaji kuwa na njia za kuondoa udanganyifu.

Cha muhimu kabisa ni kuweka mazingira ya kirafiki kwa wateja na matangazo ya kutosha yanahitajika kwa ajili ya biashara hii ili uweze kuwavutia watu zaidi na waweze kukuamini, pia inabidi uwe na ofisi maalumu ili wateja wajenge uaminifu na wewe muda na wakati wowote.

Biashara za mtandaoni zinaeleweka ni zile zile, mfano nguo, vyombo, na bidhaa za kawaida ambazo kila mwanadamu anauhitaji nazo.

  • Kutoa mtaji kwa biashara ndogo

Kusema ule ukweli jamani, hapa bongo kuna wajasiriamali wengi wenye ubunifu na vipaji na nia ya kuanzisha biashara ila hawana mtaji wa kuendesha biashara hiyo.

Biashara chipukizi kwa wajasiriamali wa bongo ni wazo bora lenye soko lililo tayari kwasababu benki nyingi za hapa hutoza viwango vya juu vya riba kwa mikopo ya kipindi kifupi na hivyo kukatisha tamaa wajasiriamali kukopa fedha.

Lakini sasa yeyote anayehitaji chakufanya ni kulielewa soko na hatimaye kuibua mahitaji ya soko hilo. Hata hivyo, biashara hii ina hatari ya juu ya hasara na hivyo utahitaji kuwa na njia za kuhakikisha kuwa mikopo kwa biashara chipukizi kwa wateja wako inatumika kwa madhumuni yaliyonuiwa. Pia, unahitaji kuwasiliana na mashirika ya udhibiti wa mikopo ili kuhakikisha usalama wa pesa zako.

  • Utayarishaji wa filamu na video

Mfano mkubwa ni chaneli ambayo inafanya vizuri sana ya Sinema zetu katika kisembuzi cha Azam, Chaneli hii inatoa fursa nyingi kwa vijana na watu ambao wanavipaji vya kuandika tamthilia wanapewa fursa ya kutangaza vitu walivyo navyo.

Tuseme tu ukweli, bongo waigizaji wenye vipaji na ubunifu ni wengi na idadi kubwa ya watu ni vijana, na hivyo basi watazamaji ni wengi. Ili uweze kujitosa kwenye biashara hii, unahitajika kutayarisha filamu na picha zenye ubora wa hali ya juu.

Waigizaji wengi wa Afrika husafiri sehemu mbalimbali kutafuta huduma za hali ya juu (yaani wanaangalia maslahi zaidi). Kanda za filamu zinazotayarishiwa Afrika zimepata umaarufu mkubwa duniani na vilevile huchukua tuzo mbalimbali.

  • Huduma za usafiri (Teksi, Bolt)

Hili ni wazo zuri la biashara hasa hapa bongo ambapo kuna idadi kubwa ya watu wenye kipato cha juu na wanapendelea huduma za teksi au bolt kwa safari zao ndefu au hata za muda mfupi. Vilevile, baadhi ya kampuni hukodisha huduma za teksi kwa baadhi ya wasimamizi wao wakuu, badala ya kuwapa magari.

Unaweza kupata huduma hii ukiwa barabarani au uagize teksi kwa kutumia simu. Ili kufanikiwa katika biashara hii, unapaswa kuhakikisha kiwango cha juu cha usalama wa gari, pamoja na kuwachukua wateja kwa wakati unaotakiwa.

  • Mafunzo kwa wafanyakazi

Ongezeko la mahitaji ya mafunzo kwa wafanyakazi katika sekta ya ajira ni kubwa mno. Wengi wa wahitimu kutoka vyuo vikuu vingi wanahitaji kozi nyingine ya kujiandaa kwa ajili ya ajira. Hali hii inaleta haja ya kuwepo kwa taasisi zaidi za mafunzo ya kitaalamu.

Baadhi ya maeneo unayoweza kutoa mafunzo ni pamoja na uendeshaji wa shughuli za kiofisi na jinsi ya kutumia fedha vyema. Wazo hili la kibiashara ni zuri katika sehemu zenye mifumo imara ya elimu.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post