Wakati mwanamuziki Emmanuel Elibarick 'Nay Wa Mitego' akitoa taarifa ya kuitwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kufuatia wimbo wake wa ‘Nitasema’ Katibu Mtendaji wa baraza hilo Dkt.Kedmon Mapana, anasema hata taarifa hizo.
Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 26, Dkt.Mapana amesema taarifa za kuitwa kwa msanii huyo hata yeye anaziona kwenye mitandao ya kijamii kama watu wengine.
“Na mimi naona tu kwenye Social Media lakini sifahamu chochote, mimi nipo Songea kikazi naona tu kwenye mitandao,” amesema Dkt.Mapana
Hata hivyo hayo ni baada ya Mwananchi kutaka kufahamu kuhusiana na wito huo ambao Nay alieleza kupitia ukurasa wake wa Instagram kuwa ameupokea.
“Nimepokea barua ya wito kutoka Baraza la Sanaa Taifa, Basata. kufika kwenye kikao kujadili wimbo wangu wa 'Nitasema' kikao kilipangwa kufanyika leo asubuhi but (lakini) nilikuwa safarini, so (hivyo) kesho Ijumaa saa sita mchana nitafika ofisi za Basata kuitikia wito huo.
“Mashabiki wangu na Watanzania wapenda haki wote kwa ujumla mimi na nyinyi letu ni moja na tutashinda kwenye kila jaribu coz (kwa sababu) sauti ya wengi ni sauti ya Mungu na haki huinua taifa. Nitasema ata iweje bado,” ameandika Nay.
Mpaka kufikia sasa wimbo huo wa ‘Nitasema’ wa Nay aliyomshirikisha Raydiace umefikisha zaidi ya watazamaji 598,045 kupitia mtandao wa Youtube.
Hata hivyo, ikumbukwe baada ya msanii huyo kutoa wimbo huo, alianza kuchangiwa fedha kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya wadau wa muziki wakidai kuwa ni zawadi yake kwa kuwa ameimba mambo yanayogua jamii.
Leave a Reply