Kama unakitambi vaa hivi kuboresha muonekano wako

Kama unakitambi vaa hivi kuboresha muonekano wako

Kitambi ni moja ya kitu ambacho hukosesha raha baadhi ya watu hasa wanawake, na ndiyo maana baadhi yao hutumia njia mbalimbali kukiondoa, ikiwemo kufanya mazoezi, diet na njia zinginezo.

Baadhi ya wanawake hulalamika na kudai kutokana na kitambi wanashindwa kuvaa aina mbalimbali za mavazi.
Magdalena Singano mkazi wa Chamazi jijini Dar es Salaam anasema anapata wakati mgumu kuchagua nguo ya kuvaa, itakayomsaidia kuficha kitambi alichonacho ili awe huru anapokuwa katika mizunguko yake.

"Hii ndiyo moja ya sababu inayonifanya nipambane sana kupunguza uzito na kitambi ili niweze kuwa huru kuvaa nguo niitakayo,”anasema
Hafsa Kiswaga mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam anasema kwa upande wake anavaa nguo yoyote ambayo anajisikia kuivaa bila ya kujali kitambi alichonacho.
"Nikisema nisubiri kitambi kiishe ndiyo nidamshi nitashindwa kuvaa kulingana na wakati, mimi navaa kile ninachojisikia ikiwa hakiko nje ya maadili", alisema.

Aidha akizungumza na Mwananchi mfanyabiashara wa nguo za kike katika eneo la Chanika, Warda Rashid anasema kitambi au tumbo kubwa isiwe sababu ya kumfanya mwanamke kuwa na mawazo na kushindwa kupendeza kwani kuna aina ya mavazi ambayo anaweza kuvaa yakamsaidia kuficha tumbo na bado akaonekana wa kisasa.

Anasema moja kati ya mavazi ambayo watu wenye kitambi huwapendeza kuvaa ni pamoja na loose dress huku akitoa angalizo kuwa ni vyema isiwe kubwa sana bali iendane na mwili wa muhusika.
"Loosedress ikiwa kubwa sana inafanya mtu aonekana mnene zaidi na pengine kusababisha kupunguza ubora wa muonekano wake," amesema.

Pia amesema mavazi yenye peplum ni mazuri kwa mtu mwenye umbo na tumbo, kwani husaidia kulificha kutokana na mtindo wake wa kuchanua kidogo na kumfanya awe na muonekano wa kawaida.
"Kama unatumbo kubwa na huna vazi la aina hii ya kumwaga kwenye kabati lako tunakushauri ukalitafute," aliongezea.

Vilevile amesema sketi zenye marinda zinapendeza zaidi ikiwa katika mtindo wa high waist na ikavaliwa juu ya tumbo.

"Pia koti au blazer huwapendeza watu wenye umbo na tumbo kubwa, unaweza kuvaa sketi au suruali ya mtindo wa high waist na ukatupia blazer au koti juu yake,"anasema
Mbali na hayo amesema mtu mwenye umbo la aina hiyo kama hatozingatia kuvaa nguo za ndani zinazoendana na umbo lake itamfanya tumbo au mwili wake kuonekana mkubwa zaidi.

"Kwa mtu mwenye umbo au tumbo kubwa anapendeza kama atavaa nguo ya ndani ambayo itamsaidia kulibana tumbo lake,”anasema






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post