Jumpsuit: Vazi la kike linalobamba kwa sasa nchini

Jumpsuit: Vazi la kike linalobamba kwa sasa nchini

Habari wewe kijana ambaye umekuwa ukifuatilia dondoo hii ya masuala mbalimbali ya fashion, ni siku nyingine tena tunakutana ili  kujuzana mambo mbalimbali kuhusiana  na urembo, mitindo na mavazi.

Leo napenda kukuletea aina ya vazi ambalo linaonekana kushika kasi kwa kupendwa na wadada wengi wanaokwenda na wakati hapa nchini si lingine ni bwela suti au ovaroli kwa kingereza tunaliita jumpsuit.

Katika historia vazi ili liligundulika mwaka 1960 na hapo zamani lilikuwa likitumika sana na watu wanaoruka na parachuti kwa lengo la kuzuia hali ya baridi na upepo.

Mwaka 1987 vazi hili lilipata umaarufu katika sekta mbalimbali ambapo lilianza kuvaliwa na marubani, madereva, wanamichezo, mafundi bomba, mafundi mitambo, wasanii  pia huvaa jukwaani, huku vyuoni/mashuleni  likivaliwa kama sare katika vyuo vya ufundi.

Kwa sasa vazi hili limeendelea kushika nafasi kubwa katika suala la mitindo huku wabunifu wengi wakibuni katika mitindo tofauti tofauti.

Hata hivyo linaoneka kuvutiwa na wadada wengi wa kisasa kwani ukilivaa unapendeza muhimu ni kuzingatia rangi na aina ya viatu utakavyochagua kuvaa.

Jinsi ya kuvaa bwela suti (jumpsuit)

Kwanza, Tambua kiuno chako

Hakikisha unajua kipimo cha kiuno chako wakati wa kuchagua bwela iliyo sahihi. Lazima lastiki au mkanda uliopo katika jumpsuit ushike vema kiuno chako ili kuepusha muonekano mbaya wa umbile lako.

Pili, fanya chaguo sahihi la jumpsuit kulingana na umbo lako

Ni vema kutambua umbo lako ili kuweza kuonekana nadhifu ndani ya vazi hili. Kwanza kabisa kwa wale wenye miguu mrefu ni vema kuvaa jumpsuit ambazo ni pana miguuni, watu wafupi au wenye urefu wa wastani hutakiwa kuangalia aina ya kitambaa na urefu wa vazi hili.

Wenye maziwa madogo, mikono miyembamba lakini wamejariwa nyonga(hips) unatakiwa kuvaa jumpsuit yenye muonekano wa blauzi zaidi pia iweze kuonyesha  mikono yako vizuri, hii itazuia muonekano wa nyonga zako zaidi.

Tatu, uchaguzi wa rangi 

Jumpsuit yenye rangi moja huvutia zaidi kuliko yenye rangi moja juu na chini rangi nyingine au yenye mchanganyiko wa rangi mbalimbali chini, katika uchaguzi wa rangi wengi hutofautiana kulingana na chaguo la mvaaji.

Nne, uchaguzi wa kiatu cha kuvalia jumpsuit

Unaweza kuvaa viatu vya chini (Flat shoes) au viatu virefu na bado ukaonekana  mwanamke nadhifu na mwenye kuvutia zaidi bila kujali umri ulionao wala umbo lako.

Kwa wasio na vitambi vikubwa na vya wastani wakivaa vazi hili linapendeza sana.

Vazi hili huweza kuvaliwa nyakati zote na katika matukio tofauti, kitu cha msingi mvaaji aangalie mtindo wa jumpsuit, aina ya kitambaa na eneo analokwenda.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post