Ijue biashara ya matunda

Ijue biashara ya matunda

Wanangu niaje? Karibu tena katika kona yetu ya michongo. Kama tunavyofahamu mtaani ajira ngumu na maisha yanaenda sawa na kasi ya jua linavyowaka yaani mtiti hakuna kivuli aisee! Muhimu zaidi kupambana. Basi bhana mwanao wa faida katikati ya jua kali nakusogezea kivuli kupitia fursa mbalimbali za biashara na leo tutaitizama kwa undani biashara ya uuzaji wa matunda maarufu mtaani kama “fruits” ambao ni mchanganyiko wa matunda tofauti tofauti.

Wataalamu wa lishe wanapohamasisha ulaji wa matunda japo hawamaanishi kuwa ni lazima kwa mlaji kupata kiasi kikubwa cha matunda hayo bali kiasi chochote hata kipande kidogo lakini mara kwa mara, kinasaidia kuleta faida mwilini. Katika jiji la Dar es salaam na viunga vyake hasa hospitalini, sokoni na mtaani, miongoni mwa biashara inayokua kwa kasi ni biashara ya uuzaji wa mchanganyiko wa matunda (fruits) ambapo biashara hiyo unaweza kuianza ukiwa na mtaji mdogo tu, basi twende pamoja mwanangu wa faida kwenye chimbo letu la biashara.

NAMNA YA KUANZISHA BIASHARA YA UUZAJI MATUNDA.

  • Mfanyabiashara anatakiwa kujua eneo la kufanya biashara na aina ya wateja wake ili kujua namna ya kutengeneza au kuaanda vifungashio vya matunda pamoja na ujazo.
  • Pia anatakiwa kujua wateja wake wanapendelea zaidi matunda ya aina gani katika mchanganyiko huo wa matunda.
  • Vilevile mfanyabiashara anatakiwa kuwa msafi na kuipenda kazi yake katika utayarishaji wa matunda. 

MTAJI WA BIASHARA YA UUZAJI MATUNDA

Mtaji ni Tshs50,000/=

Mfanyabiashara ataamua kuanza na aina gani ya matunda kulingana na uhitaji wa wateja wake lakini kwa bei ya sokoni ndizi moja Tsh.30-Tsh.50/=, tikiti Th.700/=, parachichi Tsh.200-300/=, papai Tshs800/=, tango Tsh.250/=, embe na nanasi.

Mfanyabiashara atamua kutumia sahani au mifuko laini kama vifungashio vya matunda hayo na bei ya sahani au mfuko wenye matunda huuzwa Tsh.1000/=

Pia mfanyabiashara anatakiwa kuwa na meza au kabati ambapo atahifadhia au kuandalia matunda yake ambapo mteja ataweza kuyaona.

FAIDA YA KULA MATUNDA

  • Kula matunda kwa wingi hupunguza hatari ya kupata magonjwa.

Kula matunda kila siku hupunguza hatari ya magonjwa mengi, ni vigumu kuorodhesha yote ila kwa utafiti wa 2003 chuo cha afya cha Harvard uligundua kuwa kula matunda (na mboga mboga) hupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo. 

Matunda pia yanaweza kusaidia kudhibiti shinikizo la damu, kupunguza hatari yako ya kupata saratani hivyo ulaji wa matunda ni muhimu kwa afya.

  • Matunda husaidia mifupa kuwa na nguvu

Matunda ni sehemu ya lishe yenye afya kwa ujumla, matunda yanaweza kusaidia sana kufanya mifupa na misuli yako kuwa na nguvu. Mfano tunda la parachichi ni nzuri kwa mifupa, hufanya kuwa na nguvu na matunda mengine yenye vitamin C husaidia katika afya ya mifupa.

  • Matunda yana antioxidants ambayo hupambana na ‘radicals’ bure.

Radicals bure ni atomi mbaya zisizo imara ambazo hutufanya kuzeeka haraka, kuharibu seli zetu zenye afya na hata kusababisha saratani. Antioxidants ni vitu vinavyosaidia kupigana nao. Ingawa matunda yote yako na kiwango kidogo lakini kwa matunda yaliyoiva yamejazwa na antioxidants. 

  • Matunda yana nyuzinyuzi nyingi ambayo husaidia kukuweka sawa na kuwa na afya njema

Moja ya faida kuu za matunda ni nyuzinyuzi zenye afya ndani yake ambazo husaidia kupunguza viwango vya cholesterol ya damu na kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo. Pia ni muhimu sana kwa matumbo yenye afya, inaweza kuzuia matatizo kama vile kuvimbiwa, hemorrhoids na diverticulosis.

Vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi vinaweza kukusaidia kupunguza uzito kwasababu hukufanya ujisikie umeshiba kwa muda mrefu vilevile hudhibiti sukari katika damu.

  • Matunda husaidia miili kupata vitamin na madini.

Miili yetu inahitaji vitamini na madini tofauti tofauti ili kuwa na afya na baadhi ya matunda yana virutubishi hivyo kama vile calcium na potasiamu ambavyo ni muhimu katika miili yetu kwa mfano moyo unahitaji zaidi madini ya sodiamu na potasiamu ili kuendelea kusukuma maji na matunda kama parachichi yana potasiamu.

  • Matunda hukufanya ngozi kung'aa

Wataalamu wa afya wanasema ulaji wa matunda unasaidia ngozi kung’aa kutokana na virutubisho na madini yanayopatikana kwenye matunda. Antioxidants katika matunda husaidia kukabiliana na hali hiyo, wakati maji huweka ngozi yetu kutoka ndani hadi nje.

Vilevile matunda yenye mafuta kama parachichi yanasaidia kuzuia ngozi dhidi ya mionzi ya jua pia matunda yenye vitamini C mazuri kwa ngozi kwani husaidia mwili wako kutoa collagen zaidi.

CHANGAMOTO YA BIASHARA YA MATUNDA

Kila biashara haikosi changamoto na wafanyabiashara wenyewe wanasema changamoto hazikwepeki ila unatakiwa kuwa mbunifu zaidi katika biashara yako ili kuwapatia huduma nzuri wateja pia waliweza kufunguka baadhi ya changamoto wanazokutana nazo katika biashara ya uuzaji wa matunda nazo;-

Wateja kuwa wasumbufu hasa katika uchaguzi wa matunda. Mteja anaweza kufika anaona kabisa matunda yako tayari katika sahani ataanza kuchagua mara tunda fluani toa au ongeza, kwahiyo inakuwa hasara kwa muuzaji.

Pia baadhi ya matunda yanakua kwa msimu hivyo husababisha kupunguza ujazo au mpangilio wa matunda katika aina tofauti tofauti na kusababisha kujaza aina moja tu ya matunda ambacho ni kitu wateja hawapendi.

Vilevile katika ununuzi wa matunda muda mwingine unaamua kununua mzigo mwingi ili kuepusha safari kwenda sokoni kila siku na kupunguza gharama ya usafiri lakini unakuta matunda yanaharibika kabla ya wakati au muda mwingine unakuta matunda yana uchachu au uchungu na husababisha mivutano na wateja.

Ebwana kivuli ndo hicho cha kupumzika kutoka kwenye jua kali la mtaani la kutokuwa na ajira au vipi mwanangu? Mchongo ndo huo kazi kwako kubadili kuwa pesa na waswahili wanasema sio kila fursa inakuja na ndege, fursa zingine ni wewe amka mwanangu!! 

Tukutane week ijayo kwenye kona hii ya biashara ndani ya Mwananchi Scoop. Byee Byee.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Habiba Mohamed

A digital journalist and writer for mwananchi scoop My stories around entertainment,fashion, Artist profile, relationship, lifestyle and career.


Latest Post