Mambo niaje fashionista na mpenda mitindo mwenzangu? Karibu kwenye uwanja wetu wa kujidai bwana wa suala ya mitupio na muonekano aisee.
Wiki hii moja kwa moja tumekuletea rangi ya nguo iliyoenda mjini kwa mwaka huu 2023 bwana unaijua Viva Magenta? Aloooh fanya kusoma dondoo hii hapa kwanza karibu.
Kila mwaka mamlaka ya kimataifa ya rangi - Pantone huchagua rangi ya mwaka na kwa mwaka 2023 rangi ya 'Viva Magenta' imechaguliwa kuwa rangi ya mwaka baada ya mwaka uliopita rangi ya Very Pery.
Pantone imekuwa na utaratibu wa kuteua rangi ya mwaka kwa takribani miaka 24 sasa ambayo husaidia kuongoza watu katika shughuli mbalimbali haswa za masuala ya mitindo.
Kwa mujibu wa tovuti mbalimbali za mitindo, zinaeleza kuwa ili kufikia uamuzi wa kuteua rangi fulani kuwa ndiyo rangi ya mwaka wataalamu kutoka Pantone hufanya uchunguzi kwa muda fulani juu athari za rangi duniani na katika tasnia mbalimbali kama vile mitindo, burudani, filamu, uchoraji, upambaji, maeneo ya kumbi za sherehe, michezo, maeneo maarufu ya kusafiri pamoja na hali ya kiuchumi kwa wakati huo.
Pia inaelezwa kuwa huzingatiwa teknolojia mpya zinazogunduliwa nyenzo, yanayoathiri rangi, mifumo husika ya mitandao ya kijamii na hata matukio yajayo ya michezo yanayovutia watu duniani kote.
Inaelezwa kuwa uteuzi wa rangi huo unaofanyika kila mwaka imekuwa ina athari katika maamuzi ya mtu kununua vitu mbalimbali ikiwemo mavazi, vifaa vya majumbani, muundo wa picha, ufungaji na mambo mengineyo yanayohusisha rangi.
Viva Magenta
Viva Magenta kwa mujibu wa tovuti ya webflow ni moja kati ya rangi zinazotokana na familia ya rangi nyekundu lakini yenyewe inataka kuelekea kuwa rangi ya waridi (pink) huku Pantone wakieleza kuwa rangi hiyo ipo katikati si rangi ya kuwaka sana wala si ya kupoa.
Inaeleza kuwa katika saikolojia ya rangi inaziainisha rangi hizo zilizotokana na rangi nyekundu kuwa zinaashiria upendo, nguvu, kujali pamoja na mamlaka.
Kila mwaka rangi hizi hubeba ujumbe fulani kwa mwaka husika hivyo kwa mujibu wa tovuti ya Pantone rangi ya mwaka huu imebeba ujumbe wa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya mitindo wanaeleza kuwa kuteuliwa kwa rangi fulani kuwa rangi ya mwaka kunasaidia watu kutotumia muda mrefu kutafuta rangi ambayo itatumika katika sherehe katika upande wa mavazi na mapambo.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Grace Miller watu wanapokuwa na sherehe haswa kwa upande wa wanawake wamekuwa wakiumiza kichwa ni rangi ipi wanaweza kuvaa lakini inapoteuliwa rangi fulani kuwa rangi ya mwaka inakuwa msaada kwao na kuwasaidia kuendana na wakati.
Grace anasema kuwa rangi iliyoteuliwa mwaka huu ni nzuri na inavutia haswa kwa wanawake.
"Kwa ninavyofahamu wanawake wengi wanapendelea kuvaa nguo zinazoendana na rangi ya pink hivyo naimani rangi iliyoteuliwa mwaka huu wataipenda na tutaona ikitawala katika sherehe nyingi"
Kwa upande wake Abduni Masud mkazi wa Kimara anasema masuala ya rangi ni ya wanawake kwa sababu huwa wana utaratibu wa kuwa na sare katika sherehe."Wanaume kwa asilimia kubwa hatunaga desturi ya kuwa na sare katika shughuli hivyo masuala ya rangi ya mwaka yanawahusu zaidi wanawake.
Nae, Mwanaisha Juma anasema yeye huwa anazingatia kupendeza zaidi kuliko suala la rangi ya mwaka.
Akizungumza na Jarida La Mwananchi scoop fundi wa nguo za kiume na kike kutoka Kilumbi Fashion, Abdul Kilumbi anasema kuwa iliyoteuliwa mwaka huu ya Viva Magenta ni rangi nzuri na kama itavaliwa kwa kuchanganya na rangi nyingine ni vyema kuchagua rangi iliyopoa.
Amesema rangi hiyo ina ‘match’na nguo, accessories, pochi au viatu vyenye rangi nyeusi, nyeupe, dark blue, njano, kijani, kijivu, brown, silver.
Leave a Reply