“Sijawahi kutamani kuwa maarufu (star), wala sifurahishwi sana na maisha ya kuwa mtu maarufu katika jamii kwani sio maisha bora kwangu nayakumbuka maisha yangu ya kawaida kabla sijawa maarufu”.
Hiyo ni kauli ya Hakika Ruben, mchekeshaji aliyejizolea umaarufu hivi karibuni kupitia mtandao wake wa kijamii wa “Tiktok” ambapo hadi sasa amefikisha wafuasi zaidi ya elfu arobaini na tatu.
Hakika ameeleza wazi licha yakuwa na umaarufu mkubwa wa kuburudisha anayatamani maisha yake ya hapo awali kabla hajawa maarufu.
“Nayatamani sana maisha yangu ya awali mimi ni mkimya sana sijazoea maisha ya kujichanganya na watu tofauti tofauti kitendo cha kuwa maarufu kinanipa wakati mgumu sana".
"Sikuwahi kufikiria kama nitakuja kuwa mchekeshaji ila hii staili yangu ya kuishi watu wameipenda ndo imenifikisha hapa nilipo kwa sasa"anasema.
Vile vile Hakika ruben ni mchekeshaji ambaye mara nyingi hupenda kuwasilisha ujumbe kwa hadhira akionyesha maisha yake halisi jambo ambalo limeweza kuwavutia watu wengi.
“Nina miezi kadhaa sasa tangu nianze kutambulika kikubwa nashukuru jamii imenipokea vizuri jambo ambalo sijategemea kwani nilikua nafanya vichekesho kama sehemu ya maisha yangu”.
Aidha aliongeza kuwa kitu kilichobadilika baada ya kutambulika katika jamii kwa sasa ameweza kupanua wigo wa mawasiliano.
"Mimi nilikuwa naishi maisha yangu mazuri tu kikubwa nimepata faida ya kuwa na watu wengi wanaonifahamu kwa sasa, kama kuhusu suala la maisha mazuri nilikuwa nayo tangu hapo awali."
Huku akiongeza kuwa watu wanaomzunguka kwa sasa ni tofauti na hapo awali alivyokuwa japo imekua changamoto kwake kuyakabili mazingira mapya ya kikazi.
"Mwanzoni nilikua nagombana na watu wa kawaida kama majirani zangu lakni sasa hivi najikuta napambana na waigizaji wenzangu nimepanua wigo wa marafiki na Maadui pia".
Hakika ameweka wazi kuwa anavipaji vingi licha ya kuwa mchekeshaji yeye ni Muigizaji wa sinema za mfululizo (series movie) na muimbaji wa nyimbo za injili (gospel).
Vile vile ameongeza kuwa ukiachana na uwezo aliokuwa nao yeye kama kijana anajishughulisha na shughuli nyengine wanazozifanya vijana wa kitanzania.
"Kama kijana hajawa dereva bodaboda au bajaji basi atakuwa
anauza duka aidha languo, kibanda cha uwakala au masuala ya IT hizo ndo kazi zetu hata mimi niko ndani ya shughuli hizo".
Hata hivyo hakika amefafanua suala la yeye kuwa anashirikiana na kampuni ya asasi akidai kuwa yeye anafanyakazi kwenye asasi hiyo.
Wasifu wake
Hakika Rubeni ni mzaliwa wa mkoa wa Iringa kabila lake ni Muhehe na ameloweya nchini kenya kikuyu kwa wakamba ambapo alifanikiwa kusoma elimu yake ya awali hadi sekondari.
Aidha Hakika amezaliwa mnamo mwaka 1993 na anasherehekea siku yake ya kuzaliwa kila ifakapo tarehe 25 mwezi 4 ya kila mwaka.
Pia Hakika ni mtoto wa kwanza Kati ya watoto watatu katika familia yao akiwa na wadogo zake wawili akiwemo Twilu Reuben na Moab Reuben.
Changamoto
Akizungumzia kuhusu changamoto ambayo anaipata tangu alipoanza kutambulika kwa jamii Hakika anaeleza kuwa mvutano baina ya watu ndiyo tatizo kubwa kwake (tension).
"kiukweli mimi ni mkimya sana sasa kitendo cha kujichanganya na watu kinanipa ugumu sana kwani hapo awali sikuzoea kuishi maisha ya namna hiyo."
Ndoto yake
Ndoto yake anatamani sana kukutana na mchekeshaji mkubwa hapa bongo ambaye anatambulika kwa jina la Idris Sultan kwani anamkubali sana kutokana na namna anavyofanya kazi zake za uchekeshaji.
"Kiukweli mastaa ni wengi hapa bongo lakini natamani sana kukutana nae kwa sababu namna anavyofanya kazi zake naona kabisa anashabihiana na mimi kwani mimi napenda mtu anichekeshe kama ninavyofanya kazi zangu lakini sio mtu adhamirie kunichekesha."anasema
Akizungumzia aina mbalimbali ya uchekeshaji ambao unafanywa na baadhi ya wasanii wa kiume kupenda kuchekesha kwa staili ya kuvaa uhusika wa kike yeye anaeleza kuwa bado hajawahi kufikiria kufanya aina hiyo ya uchekeshaji.
"Kila msanii na staili yake ya kuchekesha wengine ili wanoge zaidi inawalazimu kuvaa uhusika wa kike ila binafsi yangu bado sijafikiria kufanya hivyo kwa sababu hakuna kitu kitakachoashiria nifanye aina hiyo lakini ikitokea ntaangalia na uzito wa jambo lenyewe kama litanilazimu sana ila mimi sipendelei aina hii"
Maisha na Mahusiano
Hakika ameeleza wazi kuwa hajawahi kuoa ila alifanikiwa kuishi na mwanamke na kubahatika kupata watoto watatu na wawili wakiwa bahati mbaya walifariki.
Hakika aliongezea kuwa kwa sasa nimebakiwa na mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka saba(7)ambaye tayari ameanza kupata elimu yake ya Msingi.
Vile vile amebainisha kuwa kwa sasa hayupo kwenye mahusiano na mwanamke yoyote yule na endapo ataingia basi mashabiki na watu wake wakaribu watagundua hilo.
"Kiukweli sijawahi kudeti na wanawake watatu kwa wakati mmoja na nikisema niingie kwenye mahusiano basi wote mtajua kwani nikiwa kwenye mahusiano hua siwi na mambo mengi hata kuposti hamtaona mara kwa mara".
Aidha alielezea kuwa changamoto ambayo anaipitia na anashindwa kuingia kwenye mahusiano ni kutokana na watu ambao anakuanao huwa wanamzungumzia kuwa yeye ni mtu wa kulalamika sana.
" wanawake wengi wanasema mimi nina malalamiko yani nina wivu sana na ukweli mimi nikimganda mtu na mng'ang'ania haswa" anasema.
Usichokijua kuhusu hakika
Hakika amewahi kubeba uhusika wa kaka kwa aliyekuwa mzazi mwenzake kwenye msiba wa mtoto wao baada ya kutambulishwa yeye kama kaka na mwanamke ambaye alizaa nae.
“Sitaweza kusahau jambo hili mzazi mwenzangu alinitambulisha mimi kama kaka yake baada ya kuolewa na mwanaume mwengine wakati wa msiba wa mtoto wetu”.
“Niliumia sana lakini nilitumia ubinaadamu huwezi kuleta fujo msbini lakini baada ya tukio hilo sikuruhusu tena mtoto wangu aliyebaki kuendelea kukaa kwa mama yake niliamua kumchukua mwanangu”.
Ili kupata habari zinahusu wasanii wakongwe na chipukizi hapa bongo, endelea kufuatilia jarida la Mwananchi Scoop ili ufahamu mengi zaidi.
Leave a Reply