Baada ya mwigizaji Salim Ahmedy ‘Gabo Zigamba’ kutembelea ubalozi wa Tanzania nchini Comoro, amefunguka kuwa ni muda wa watengenezaji filamu kujitoa ili kazi zao ziweze kupenya nje ya nchi.
Akizungumza na Mwananchi Scoop Gabo ambaye kwa sasa yupo nchini Comoro kwa ajili ya kurekodi muendelezo wa Tamthilia ya ‘Mawio’ inayoonesha katika kisimbuzi cha Azam ameeleza kuwa Balozi Said Yakub amemshauri kufanya kazi na watu wa nchi hiyo ili kuendeleza mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Comoro.
“Yapo mengi tumezungumza. Mafunzo ni makubwa hasa utamaduni na siku ya Kicomoro lakini kubwa zaidi alilonisisitizia ni kuboresha mahusiano yetu na Comoro kupitia sekta ya sanaa kwani kufanya hivyo kunaongeza ushirikiano na undugu wa kihistoria wa Tanzania na Comoro,” amesema Gabo
Hata hivyo, aliongeza kwa kuweka wazi kuwa ili kuifanyia kazi kauli ya Balozi Yakub amepanga kumuweka msanii mkubwa wa muziki kutoka Comoro kwenye tamthilia hiyo inayotazamwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania, Kenya pamoja na Comoro.
Aidha mwigizaji huyo ambaye amewahi kutamba na filamu ya ‘Safari ya Gwalu’ amewataka watengenezaji filamu wenzake kuendelea kujitoa kwa ajili ya tasnia ili filamu ziweze kupenya katika mataifa mengine.
Gabo katika safari hiyo ameungana na wasanii baadhi katika tamthilia ya Mawio akiwemo mwanamuziki Barnaba na Sarah kwa ajili ya kurekodi baadhi ya vipande vya tamthilia hiyo katika Kisiwa cha Ngazidja
Leave a Reply