Na Aisha Lungato
Maendeleo makubwa katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) imeenda kubadilisha nyanja mbalimbali ya maisha yetu ikiwemo namna tunavyowasiliana na marafiki, tunavyopata taarifa, pamoja na tunavyofanya uuzaji na ununuaji wa bidhaa.
Awali kabla ya maendeleo hayo watu walikuwa wakiwasiliana kupitia barua, kupata taarifa mbalimbali kupitia redio na televisheni na hata kununua bidhaa kwa kutembelea katika maduka yanayoziuza.
Lakini kupitia mapinduzi hayo ya Tehama mambo yamebadilika sasa kupitia vifaa vya kielektroniki vilivyounganishwa na intaneti kama vile simu na komputa sasa watu wanaweza kuwasiliana, kupata taarifa mbalimbali na hata kufanya biashara.
Wengine hutumia mitandao ya kijamii haswa Instagram, Facebook na Whatsapp kutangaza bidhaa zao.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na maendeleo (UNCTAD) zinaonyesha kuwa wakati wa mlipuko wa janga la Uviko-19 biashara ya mtandaoni ilishamiri zaidi huku wanawake na watu wenye elimu ya juu wakionyesha kuongoza.
Pia watu wenye umri wa kati ya miaka 25 na 44 ndio kundi lililoongeza zaidi manunuzi mtandaoni ikilinganishwa na makundi yenye umri mdogo.
Biashara hizo zimekuwa zikisifiwa kwa kuzalisha ajira kwa vijana wengi pamoja na kurahisisha ununuaji wa bidhaa lakini pia imekuwa ikilalamikiwa kwa mambo mbalimbali ikiwemo wizi na utapeli.
Mwananchi Scoop ilizungumza na baadhi ya wafanyabiashara na wanununuzi ili kufahamu tamu na chungu ya bishara hizo za mtandaoni.
Aziza Ignas mkazi wa Kimara ambaye ni mmoja wa watu wanaotumia sana njia ya mtandao kununua mahitaji yake alisema aina hiyo ya manunuzi inamsaidia sana katika kuokoa muda mwingi pamoja na gharama ambayo angeutumia kufuata bidhaa anazozihitaji.
“Mfano katika maandalizi yangu ya sikukuu ya Eid ya juzi niliweza kununua nguo za wadogo zangu, mapazia pamoja na mahitaji mengine kupitia simu yangu huku nikiendelea na pirikapirika za kutafuta riziki, pengine isingekuwa mfumo huo ingenilazimu kuvunja ratiba zangu nyingine kwa siku hiyo”
“Pia tangu nimeanza kufanya manunuzi yangu na hata malipo mbalimbali kwa njia ya mtandao nimesahau hata madhila ya kukaa kwenye foleni, na hata msongamano watu kipindi cha kufanya maandalizi ya sikukuu,”alisema.
Aziza alisema kuwa kupitia ununuaji kwa njia ya mtandao inakuwezesha kupata bidhaa ambayo inapatikana hata nje ya nchi au mkoa ulipo mfano Uturuki na China.
Manufaa mengine aliyoyabainisha ni kupata bidhaa hata nyakati za usiku pia siyo lazima uwe na pesa taslimu, unaweza kufanya malipo hata kwa njia ya mtandao.
Nae, Jackline Maneno mkazi wa Kigamboni alisema mbali na manufaa hayo vilevile pia mfumo huo wa manunuzi una changamoto kadhaa ikiwemo kupata kile kisichoendana na uhalisia wa picha ya bidhaa.
“Unatumiwa picha na mfanyabiashara au umeiona kupitia mtandao wake wa instagram, whatsapp au facebook ambayo inaonyesha picha ya nguo, vyombo, au bidhaa nyingine lakini huwa inatokea mara kadhaa unapokea bidhaa ambayo kiuhalisia haifanani na ile iliyokuvutia kwenye picha hadi ukashawishika kununua”
“Au kinaweza pia kuwa hakiko katika ubora au ukubwa uliotarajia kama ulivyoona katika picha” aliongeza Jackline Maneno
Pia alieleza kuwa kumekuwa na baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakifanya utapeli hali inayojenga hofu kwao kama wanunuzi wa bidhaa hizo.
“Imewahi kutokea kwa marafiki zangu wawili, unakuta picha za bidhaa mfano katika ukurasa wa mfanyabiashara fulani kwenye mitandao unaipenda na kuasiliana nae ili ujue ni kwa namna gani utaipata bidhaa hiyo, unailipia lakini baada ya muda unapiga simu hiyo inakuwa haipatikani au kutopokelewa kabisa.
Aliongeza kuwa ununuaji wa bidhaa mtandaoni kunakunyima uwezo wa kujaribu bidhaa kabla ya kuinunua hali inayoweza kukupelekea kupata bidhaa isiyoendana na wewe.
“Changamoto nyingine ni hofu ya malipo ya ulaghai, utapeli na wizi wa habari za kibinafsi, unapokuwa katika eneo lenye changamoto za kimtandao, gharama za kuletewa bidhaa’delivery kwa baadhi ya wafanyabiashara wa mitandaoni huwa ni kubwa”. amesema Jackline Maneno
Akizungumza kwa upande wa wafanyabiashara wa nguo za wanawake na urembo wa wanawake, Sumaiya Abdallah Mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alieleza kuwa kwa upande wake huwa anapata faida kubwa inayoweza kukizi mahitaji yake pale Boom linapo muishia.
“Biashara hizi mara nyingi si mkubwa sana inategemea na kile unachokiuza hali inayotufanya hata sisi wanafunzi wa vyuo tumudu kujiajiri kupitia biashara hizo, na kupata maokoto ya maana si wanafunzi pekee hata baadhi ya wahitimu nao wamekuwa wakijiajiri kupitia biashara za mtandaoni”
Faida nyingine alizozibainisha Sumaiya ni pamoja na urahisi wa kuhifadhi miamala iliyofanywa na wateja na kupelekea urahisi wa kudhibiti mahesabu, urahisi wa mawasiliano kati ya mfanyabishara na mteja, inakujengea uhusiano wa karibu na watu mbalimbali.
Kwa upande wa changamoto Sumaiya alieleza kuwa kuanza biashara hadi kufikiwa kuaminiwa na wateja ni ngumu kutokana na baadhi yao kukubwa na utapeli.
“Ni vigumu sana mteja kukuamini kutokana baadhi ya watu wanaofanya utapeli mtandaoni, inatulazimu hadi kubuni mbinu mbalimbali za kumuaminisha mteja ikiwemo ya kumwambia afanye malipo baada ya kupokea mzigo wake na kuridhika nao”alisema.
Alisema pia kuna tabia za baadhi ya wateja ambazo huwapelekea wao kupata hasara ikiwemo, mteja kulazimisha kulipa ela kamili bila ya kutolea na wengine kugomea kulipa gharama za ufikishaji wa bidhaa zao.
Alibainisha kuwa uchelewaji wa kuwasili kwa bidhaa wanazoagiza nje ya nchi, kuja kwa bidhaa chini ya kiwango kilichotarajiwa ni baadhi ya sababu zinazowapelekea kuingia katika mgogoro na wateja wao.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi
Leave a Reply