Nenda Kamwambie. Kwamba Mondi ndiyo bidhaa bora zaidi ya muziki kwa miaka 14. Haichuji, haipauki, haichoshi kwa macho na masikio. Huyu ndiye staa zaidi wa muziki hapa Afrika Mashariki ya sasa.
Nitarejea. Mbwana Samatta, aliingia katika soka la kimataifa Mondi akiwa staa mkubwa tayari. Dalili ziko wazi kuwa Champion Boy atarejea Bongo, huku Mondi akiwa staa vilevile. Tamati ya ustaa wake haionekani.
Mbagala. Mradi wa mwendokasi ni wazi unafuta taswira iliyojengeka kwa wengi. Kama ni eneo chovu na lenye huduma mbovu ya usafiri. Hata maudhui ya dude lake la Mbagala yalitutaka tuamini hivyo.
Mawazo. Wengi waliamini msela wa Tandale hana mbio ndefu. Atakuja na kutoweka kama upepo kwenye gemu. Kadiri siku zinavyosogea bila shaka wanabaki na mawazo. Kwamba jamaa atashuka lini?
Moyo wangu. Moyo unavyokutuma ama unavyotaka ndicho ulichopangiwa. Ni wazi Mondi aliamini katika moyo wake. Ndiyo maana hakuwahi kuingia unyonge kwenye mitikasi yake. Mikono mingi na fitina nyingi aliziishi.
Lala salama. Kama mwenzetu umeamua kulala wewe lala salama tu. Sisi wengine tupo kwenye mbio. Hakuna kulala ndiyo maana Mondi alihaha bila kulala, ili jina lake lishinde majina yote. Kuanzia katika magazeti, runingani na redioni.
Nataka kulewa. Kuna ‘taimu’ kila jambo unalogusa linageuka dhahabu. Mondi katika ubora wake wa mwanzoni. Hata uhusiano wake ulikuwa ni dhahabu kwa macho na masikio ya wengi. Kila kitu kikiwa kwenye mstari mwisho utataka kulewa tu.
Number One. Yes! Ukijengea picha ya ukubwa utakuwa mkubwa. Ukiamini wewe ni namba moja utakuwa namba moja tu. Kwa sababu utataka kila kitu unachofanya kiendane na ukubwa wako na mwisho utakuwa namba moja.
Ukimuona. Baada ya kumuona Davido, historia yake ilibadilika ‘totale’. Ghafla tukaanza kumuona kwenye ‘steji’ kubwa kila kona ya Afrika. ‘Am gonna meki yu feimasi’, ‘panchi laini’ katika ‘vesi’ ya Davido kwenye lile pini la Number 1 remix, hii ilimaanisha.
Vijana mnapaswa kuziishi ndoto zenu. Mpiganie ndoto zenu. Amini katika ndoto zetu na kila kitu kinawezekana. Mondi ni mtoto wa kitaa mwenye njaa njaa zake. Akajitafuta na kujipata, akakomaa. Leo ni mmoja wa ‘bigi bosesi’ hapa mjini.
Mwaka wa 14 huu yupo juu kwa kila kitu. Kimuziki, kimapene na kiustaa. Katika mastaa wawili awe wa kike au wa kiume kwa hapa Bongo. Hapo weka na jina la Mondi pale katikati hawezi kukosekana. Hawa ndiyo madogo wenye hasira na ‘laifu’.
Unaweza kuwa na hasira na maisha na bado ukaishia kuwa mwendawazimu tu. Kuna watu hasira za maisha huwapeleka kwenye ulevi wa pombe, bangi, unga au kamari. Mwisho wa siku huishia kuitesa jamii inayomzunguka kwa kupagawa.
Hasira za maisha ukizihamishia kwenye utafutaji lazima utoboe. Suala la muda gani utatoboa itategemea bidii, nidhamu na kasi yako. Unaweza kuingiza sana na ukatumia sana, ikawa kazi bure. Na hili ndiyo kosa la vijana walio wengi mjini nikiwepo na mimi.
Siri ya utajiri ni kuingiza sana na kutumia kidogo sana. Lakini sisi watoto wa ‘tauni’ tunaingiza kidogo sana na kutumia kingi sana. Tupo tupo tu. Na kisingizio chetu ni “Pesa yenyewe ya kutunza iko wapi?” Tunaishi na msemo huo.
Kwenye uongozi wa soka kuna Ismaily Aden Rage, kwenye siasa za upinzani kuna Freeman Mbowe, kwenye burudani kuna Joseph Kusaga, kwenye muziki kuna Naseeb Abdul. Hawa walijua na wamejua ‘kumeinteini statasi’ zao.
Huyu Mondi ameshika akili za machizi muziki Bongo. Tena katika ubora wa hali ya juu sana. Ni kama mtu aliyekuwa nje yetu sisi, akatusoma kila kitu na kujua afanyeje. Kuna siku atakaa atulie lakini siyo leo au kesho. Bado tunaye sana.
Utabiri ni mwingi sana wa atashuka tu. Lakini hadi leo ukiondoa watu kama vile Hayati King Majuto, Hayati Gurumo, Hayati Tx Moshi, Bitchuka na Khadija Koppa, Mondi atavunja rekodi za wengi katika kuhudumia watu kisanii.
Anaenda kuwa staa aliyedumu na ustaa wake kwa muda mrefu kileleni. Mpaka sasa ni miaka 14 siyo tu ni staa, bali ni staa mkubwa mbele ya wenzake. Alianza Bongo sasa ni Afrika Mashariki yote ipo kwenye uvungu wa soksi zake.
Wanamuziki wengi waliishia njiani. Hata Chameleone wa leo siyo yule wa miaka 10 nyuma. Chameleone wa leo kashuka. Ila Mondi wa leo siyo wa miaka 10 nyuma. Wa leo kapanda jina, ngoma na namba nyingi kwenye akaunti.
Kuna wakati tuliambiwa hajui kuimba. Baadaye ikaja stori kuwa anabebwa na Wema. Ikaja stori kuwa bila Davido asingefika pale alipo. Ghafla zikaanza zile stori kuwa hawezi kuandika kama zamani mara anaiga Wanaijeria.
Hapo kati tuliaminishwa kuwa Mondi kashuka sana na kwamba zile ngoma alizoimba kivyake zimebuma. Lakini zile alizoshirikishwa ndiyo zinakimbiiza. Kama Kwangwaru, Tetema na kina Zuchu hadi za juzi na Jux.
Nenda duniani mbali kote hivi sasa, mchizi anaimbisha masela na maduu kila kona. Mwendo wa Komasava, mtaa umedata. Sasa twende mitaani mwetu tukaaminishane kuwa hawezekaniki pengine ndiyo atawezekanika.
Komasava!
Leave a Reply