Vijana Pwani kuwezeshwa kiuchumi

Vijana Pwani kuwezeshwa kiuchumi

Tatizo la vijana wengi nchini kuchagua kazi na kukaa vijiwani limekuwa likigonga vichwa vya habari licha ya serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo kupambana ili kutokomeza hali hiyo.

Unaweza kukuta kijana amemaliza chuo na amepata maarifa ya kutosha lakini anashinda kijiweni na kusubiria chakula kinachotafutwa na wazazi wake.

Katika kukomesha dhana hiyo, makala hii itajikita zaidi kuangazia fursa muhimu wanayopatiwa vijana wilayani Mkuranga mkoani Pwani na Asasi ya Kiraia ya Ushirikiano wa Vijana Mwandege (USHIVIMWA) ambapo inaweza kuwa chachu ya kuwabadilisha wengine.

Ushivimwa kupitia mradi wake maalum wa utawala bora, uzalendo na maadili kwa vijana ambao unafadhiliwa na Shirika la The Foundation For Civil Society (FCS) la jijini Dar es salaam, wamejizatiti katika kuwaondoa vijana hasa wa vyuoni kuachana na mawazo hasi na badala yake kujitambua na kutafuta fursa za kiuchumi.

Mradi huo ambao ni wa miezi sita umelenga pia kuwawezesha vijana wilayani humo kutambua sera ya taifa ya vijana, pamoja na kuunda majukwaa na vikundi vidogo vidogo vya ujasiriamali ili kuunganisha nguvu pamoja na kupata urahisi wa kukopesheka na serikali ya wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Asasi hiyo ya Ushivimwa, Mohamed Mbonde, anasema kuwa dhamira yao ya dhati ni kuwasaidia vijana kimawazo, kuondokana na dhana ya kukaa vijiweni kisha kuinuka na kujikomboa kiuchumi.

Ifahamike kuwa mradi huo wenye thamani ya Sh. Milioni 59.9, unatazamiwa kuwafikia takriban vijana zaidi ya 500 kwenye kata tano za wilaya hiyo ya Mkuranga mkoani Pwani ambazo ni Kata za Mwandege, Mkuranga, Vikindu, Kimanzichana na Mwalusembe.

Tayari mafunzo yamekwishafanyika ya kuwajengea uwezo vijana hao, pia ukaguzi wa kutambua miradi ya vijana hao tayari imeonekana kwenye vikundi vidogo vidogo katika kata hizo, ambapo miongoni mwake kuna ufugaji wa kuku, kilimo cha mbogamboga, utengenezaji na uuzaji wa sabuni na kadhalika.

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi huo kutoka asasi ya Ushivimwa, Hassan Ndengu anasema kuwa, mradi huo umewalenga vijana zaidi kwa kuwa ndiyo kundi kubwa katika taifa , hivyo iwapo kundi hilo lisipoangaliwa, uwezekano wa kuifikisha nchi katika uchumi wa viwanda 2025, itakuwa ni ndoto.

Anasema kwa upande wa changamoto ambazo zimeonekana kwa vijana hao wanaopatiwa mafunzo hayo ni kwamba, wako ambao licha ya kumnaliza chuo na kupata maarifa wamekata tamaa na maisha, kana kwamba wakihisi hawawezi kufanikiwa.

“Mtazamo huu unapingwa vikali na Ushivimwa na inafanya kila liwezekanalo ili kuondosha fikra hizo hasi kwa vijana hao, na hatimaye kujikomboa kifikra na maarifa katika maisha.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Peter Nambunga, akizungumzia mradi huo wilayani kwake anasema kuwa mafunzo wanayopatiwa vijana hao yana tija kubwa kwa manufaa yao pamoja na taifa kwa ujumla ikizingatiwa ya kwamba hivi sasa suala la kujiajiri limepewa kipaumbele kuliko kuajiriwa. 

Ofisa huyo anasema kuwa tayari Sh.Milioni 108, zimeanza kutolewa mwezi huu kama sehemu ya mkopo kwa vijana na wanawake, na hiyo yote imeelezwa kuwa ni katika harakati za kutegua kitendawili cha vijana wengi eti ya kwamba hawafahamu ni wapi watakopeshwa.

Fedha hizo zimeanza kutolewa baada ya kamati maalum inayohusika na mikopo kukutana na kufanya uhakiki wa vikundi vya ujasirimali ambavyo vyenye sifa stahiki kama utaratibu unavyoeleza katika utoaji wa mikopo hiyo isiyo na riba.

Nambunga anasema kuwa dhana ya vijana kukaa mitaani na kufanya mambo ya hovyo, iondoke mara moja na badala yake waunde vikundi na kuanzisha miradi midogo midogo, huku serikali ikijizatiti kuwasaidia katika kuwakopesha fedha ili kuongeza mitaji yao na kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

Naye Meneja Miradi wa Ushivimwa, Nurdin Kiswamba, ameeleza kuwa mradi huo pia una lengo la kuongeza idadi ya vijana wenye maarifa juu ya sera ya taifa ya vijana ili waweze kuwa na sauti ya pamoja katika kujiletea maendeleo.

Anasema kuwa fursa zipo, tatizo la vijana wengi wamekuwa hawako tayari kujitoa kwa hali na mali na badala yake kubeza mambo ya msingi wakidhani hayawezi kufanikiwa, jambo ambalo kwa nyakati za hivi sasa, halina mashiko.

“Kinachotakiwa ni kuthubutu, mawazo mgando kwa sasa hayana nafasi tena, vijana embu amkeni, wakati ndiyo huu sasa wa kupata unachotaka walau kwa wastani,”anasema kiswamba.

Aidha katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2018/2019, imeelezwa kuwa walemavu pia wamejumuishwa katika suala zima la kupatiwa mikopo, hivyo cha muhimu zaidi ni kujiunga katika vikundi, huku wakibuni miradi ya kiuchumi ili iwe alama tosha pindi maofisa wanapotaka kujiridhisha kwamba fedha zitakazotolewa, zitasogeza biashara badala ya kaunzisha.

“Pia iko shida kwa baadhi ya vijanam wamekuwa hawakopesheki baadhi ya maeneo kutokana na kusuasua katika ulipaji wao kwa wakati, na hiyo inatokana na mtazamo hasi ya kwamba eti ni fedha za serikali hutolewa bure kwa vijana,”anasema Kiswamba.

Hata hivyo, Ushivimwa inauliza vijana ya kwamba, ikiwa fedha hizo za mikopo hazitarudishwa kwa wakati, je wengine wakizihitaji, zitatoka wapi?.

Kitu cha umuhimu kwa vijana ni kwam ba, wakati huu si wa kuvunja watu moyo, wanapokopeshwa, wafanya jitihada za kuzirudisha kwa wakati, kwani wafahamu ya kwamba, mikopo kama hiyo isiyo na riba ni rafiki kwa vijana katika kuwainua kiuchumi.  

Akiwa kwenye ziara ya kutembelea majukwaa pamoja na vikundi vya vijana hao ili kujionea kazi walizozibuni ili waweze kupata mikopo, Ofisa maendeleo ya jamii wilayani Mkuranga, Salum Ngawile, anasema kuwa vijana hao wameonyesha njia kwa kuwa miradi yao inaonekana hivyo wachangamkie fursa za mikopo.

Aidha Ngawile aliongeza kuwa, katika mwaka wa fedha wa 2018/2019, kiasi cha Sh Milioni 400 kinatarajiwa kutolewa kwa vikundi hivyo vya ujasirimali vya vijana, wanawake na walemavu ambapo mkopo huo hauna riba.

Wilayani Mkuranga kuna zaidi ya vikundi 400 vya ujasiorimalia, hivyo ni wakati muafaka sasa kwa wao kukaa na kuratibu vizuri shughuli zao, ili waweze kukopesheka na kujikwamua na umasikini.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post