Habari msomaji wetu, ni siku nyingine tena tunakutaka ili kujuzana mambo mbalimbali kuhusiana masuala ya urembo, mitindo na mavazi ambapo leo napenda kuwajuza juu ya mambo ya kuzingatia ili kucha zako ziwe na mvuto wakati wote.
Ni wazi mikono, viganja na vidole ni kati ya sehemu muhimu katika mwili wa msichana. Mikono hutumika kufanya shughuli nyingi za nyumbani, shuleni na sehemu mbalimbali katika maisha kuanzia kupika, kufanya usafi, kuandika, kujiremba pamoja na majukumu mengine mengi.
Mikono isipotunzwa vizuri ni rahisi sana kuharibika, kupoteza mvuto wake wa asili na kuharibu afya ya kucha.
Mambo ya kuzingatia ili kucha zako ziwe na mvuto, jambo la muhimu kufahamu kuwa baadhi ya vipodozi vinavyotumika katika urembo wa kucha, vina rangi na sumu zisizofaa kwa afya.
Sumu kama vile ‘Formaldehyde na Toluene’ zinazopatikana katika baadhi ya rangi za kucha zina madhara kwa afya ya msichana.
Ni kweli rangi ya kucha huongeza urembo, mvuto na furaha ya msichana lakini pia ni busara kukumbuka kuwa afya ni muhimu kuliko urembo na uzuri hivyo ni vyema ukajiepusha na matumizi ya rangi ya kucha mara kwa mara.
Pia afya ya mwili na kucha za msichana kwa ujumla hutegemea chakula bora chenye protin, madini na vitamini na siyo rangi na vipodozi.
Kwa ajili ya afya bora ya kucha msichana anashauriwa kula mboga za majani, maharage, korosho, asali na matunda kwa wingi kila siku.
Aidha upungufu wa vitamini A, B, protin, madini ya chuma na chokaa (kalishiamu) mwilini husababisha kucha zipoteze afya yake ya asili. Kucha ambazo hazina afya zinaweza kuoza, kukauka, kupinda, kupasuka au kuwa na umbo kama kijiko.
Safisha kucha kila siku kwa kuziosha kwa maji ya uvuguvugu na sabuni laini pamoja na brashi ndogo ya mikono kwani huimarisha afya ya kucha.
Leave a Reply