So you wanna be a salesperson. Ijue Kazi hii kiundani zaidi!

So you wanna be a salesperson. Ijue Kazi hii kiundani zaidi!

 Eh bwana eh! Unatamani kuwa mtanashati, na kufanya kazi zenye kuleta matokeo positive kwenye kampuni? Hii ni kati ya kazi ambazo ukizifanya fresh, kutoboa ni rahisi, na sababu kuu ya hili ni kwamba watu wanaoleta mchongo wa pesa kwenye kampuni, hutambulika zaidi kuliko wengine.

Kama unataka kupiga hela, huku ukijitengenezea jina na connection mbalimbali, kazi ya masoko na mauzo inakuhusu sana tu!

 

 Kazi ya hii tunaiita ni kazi ambayo ni kama uti wa mgongo wa kila kampuni au taasisi.

 

Maarifa muhimu katika tasnia

  

Unataka kutoboa? Hakikisha unazingatia maarifa haya! Wanasema kuwa waajiri wengi hawapendelei watu waliotoka chuoni kwani hawana maarifa sahihi, hivyo basi, kuwa tofauti!

 

  1. Soma masomo ya biashara

 

Unasoma masomo ya biashara? Hii kazi ni yako! Fanya ufanyavyo, uweze kusoma biashara chuoni, ili kujiongezea nafasi ya kufanya kazi ya masoko na mauzo. Ukipiga degree yako ya Business in Marketing au Bcom, utakuwa umetisha!

 

  1. Fahamu Lugha

 

Oya, ikiwezekana hata jifunze lugha za kigeni kama kifaransa na kachina. Utashangaa ni milango mingapi inafunguka kwa wewe kuwa na uelewa wa lugha mbalimbali.

 

Lugha ya muhimu zaidi kuijua kwa ufasaha ni Kiingereza. Ukipiga ngeli vizuri, anza kujifunza na lugha zingine. Mtu wa masoko anatakiwa afahamu lugha kwa ufasaha, kwani ndiyo msingi mkubwa katika kazi hiyo.

 

  1. Hesabu

 

Kama uliikimbia hii, usingekuwa unasoma biashara, ila kama kweli una mpango wa kuhamia huku, hesabu muhimu sana!

 

Watu wengi ambao wanajihusisha na masoko hufikiri kwamba hesabu haihusiki, lakini ili uwe mfanyakazi mzuri katika kitengo hicho hakikisha uko vizuri katika sekta ya hesabu.

 

Kama hesabu zinakupiga chenga, hii ngoma sio ya kwako!

 

  1. Ubunifu

 

 Ubunifu wa ufanyaji kazi na mbinu mpya za kupiku wapinzani na muhimu sana. Unatakiwa ukubali kujifunza kupitia wengine, bila creativity utafeli. Huwezi kutumia mbinu za zamani kila siku, kupata wateja wapya! Weka akili freshi, tafuta maoni ya watu, search kwenye Google njia mpya za kuuza bidhaa na kupata wateja, ukifaulu katika hilo, na kwenda extra mile kuliko wengine, wateja watakupenda, na watakupa tenda wewe kila siku.

 

Mfano hai wa kijana katika Kazi ya Masoko na Mauzo

 

Kama unajihisi hii kazi ni ya kwako kabisa, mtazame kijana mwenzako anaefanya maajabu katika tasnia.

Selina Julius Otacho, ni Meneja Masoko na Mauzo, katika kiwanda cha nguo cha Urafiki, kilichopo Mabibo, jijini Dar es salaam, ambaye amedumu kwenye kazi hiyo takribani miaka kumi, ingawa awali ndoto yake ilikuwa ni kuwa mwanasheria.

 

 “Wakati nasoma nilikuwa napenda kuwa mwanasheria, lakini baadae akili yangu ikanipeleka kwenye biashara, na hapo ndipo nilipoanza kujitathmini mwenyewe kwanza, hiyo ilinifanya kuamua kusomea kazi ya masoko na mauzo,” alisema.

 

Selina ametueleza kuwa kazi ya masoko na mauzo haihitaji hasira, kwani inahitaji kujua namna ya kuwasiliana na kuwasilisha huduma au bidhaa kwa wateja.

 

“Ukifikiria masoko ni kuuza utafeli, kwani masoko sio kuuza, kuuza ni sehemu ndogo tu! kuna vitu ambavyo vinasababisha wewe kuuza, na hivyo vitu ndiyo masoko yenyewe,” aliongeza.

 

 

Ufanyaje ukitaka kufanya kazi kwenye tasnia ya masoko?

 

Kama unataka kusomea kazi ya masoko, unapaswa kutambua kuwa soko kwa sasa limebadilika, hivyo unatakiwa kuwa na uwezo wa kubadilika mara kwa mara kulingana na uhitaji wa wakati huo.

 

Pia mtu wa masoko unatakiwa kufuatilia ile huduma au bidhaa unayoitoa kwa mteja kama imekidhi viwango, ukiweza kufanya hivyo itakusaidia zaidi kwenye uzalishaji na utagundua namna utakavyoweza kufanya kazi zako.

 

Hata hivyo, watu wanatakiwa kutambua tofauti kati ya masoko na mauzo kwani siku zote mauzo ni sehemu moja wapo tu ya masoko, na si vinginevyo!

 

 Changamoto

 

Selina anatubainisha uzito wa kazi hii;

 

 “Kiukweli changamoto ambayo nimekumbana nayo katika kazi hii ni kutokuaminika. Mara nyingi unapoleta wazo kwa ajili ya maendeleo ya taasisi, unaonekana kama unafanya kwa ajili ya matakwa yako binafsi.”

 

Mtu wa masoko siku zote anakuwa anasimama kwa niaba ya mteja, hata kwenye masuala ya mawasiliano, yeye ndiye anayewasilisha hoja ya taasisi yoyote ile kwa mteja.

 

Wakati mwingine mteja anaweza akataka huduma au bidhaa ya kitu fulani, na wakati huo unakuta kile ambacho anakihitaji hakipo, unapaswa kupambana kuhakikisha mteja anapata ile huduma.

 

Elimu

 

Mwaka 2007, Selina alijiunga kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), na kutunukiwa shahada ya Biashara, mwaka 2010.

  

ANGALIZO

 

Ukiwa unajiandaa kusomea kazi hiyo, unapaswa kutambua kuwa hakuna watu wenye fitina kama watu wa masoko na mauzo, lakini tambua kuwa hiyo ndiyo kazi yenyewe.

 

Kazi ya masoko na mauzo ni kazi nzuri ambayo ukiifanya vizuri itakujengea mahusiano mazuri kati yako wewe na wateja wako, pia hakikisha unakuwa na ubunifu kila wakati.

 

Hakikisha pia una uwezo wa kuzingatia muda, kuendana na muda katika kazi yako ndiyo msingi mkuu wa mafanikio katika tasnia hii: Mfano ukiwa unafanya kazi kwenye kitengo cha kusambaza bidhaa fulani, basi hakikisha unajitahidi kuangalia fursa inayopatikana kutokana na ile bidhaa kwa wakati huo.

 

 

Zingatia kuwa ili ufanikiwe kwenye kazi yoyote ile, hakikisha unakuwa na mambo haya matatu muhimu - uvumilivu, kuzingatia muda, na kubali kukosolewa na kujifunza pia. Hizi ndizo nguzo za mafanikio katika sekta ya masoko na mauzo.

 

Baada ya madini yote haya, kazi ni kwako!

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post