Masanja: Ugawaji Vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada waiingizia Serikali Bilioni 19.2

Masanja: Ugawaji Vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada waiingizia Serikali Bilioni 19.2

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema ugawaji vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada ulioanza mwaka 2019, umesaidia kuingiza Serikali kiasi cha Sh.19.2 bilioni kutoka bilioni 5.24 zilizokuwa zikipatikana kabla ya kuwepo kwa mfumo huo.

Masanja ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada wa sita uliofanyika Januari 12 hadi 18, 2022.

Masanja amesema tangu mwaka 2019 mfumo huo ulipoanza rasmi hadi sasa jumla ya minada sita ya vitalu vya uwindaji wa kitalii imefanyika kwa njia ya mtandao na imeingiza kiasi cha Bilioni 19.2.

“Katika mnada wa sita ambao ulifanyika Januari 12 hadi 18 mwaka huu ulihusisha jumla ya vitalu 75 vya uwindaji wa kitalii, vitalu 49 umiliki wake unamalizika Desemba 31, 2022, vitalu 26 ni vile ambavyo vilikuwa wazi, jumla ya kampuni 39 zilishiriki mnada huo na kati ya hizo 26 sawa na asilimia 54.2 zilishinda vitalu vya uwindaji wa kitalii 45.

“Mnada huu wa sita jumla ya kiasi cha Sh. 14.32 bilioni zilikusanywa ambapo Sh. 392.7 Milioni zilitokana na ada ya maombi ya ushiriki na Sh. 13.86 bilioni zilitokana na ada ya vitalu,” amesema Masanja

Hata hivyo amesema Serikali iliamua kugawa vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada kwa lengo la kuongeza uwazi na kuruhusu nguvu ya soko kuonesha thamani halisi ya rasilimali muhimu ya nchi ya vitalu hivyo.

“Kwa mfano kitalu kimoja daraja la tatu ambacho kilikuwa kiuzwe kwa njia ya zabuni wa Sh. 41.58 milioni kimeuzwa kwa Sh. 462 Milioni ambayo ni mara 11 ya bei ya zabuni. Daraja ya pili kilikuwa kiuzwe Sh. 69.3 Milioni kwa njia ya zabuni ila kimeuzwa zaidi ya Sh. 577Milioni,” amesema Masanja.

Aidha alisema minada ya vitalu vingine vilivyobakia utafanyika Machi mwaka huu hivyo amewaomba wadau wa utalii wanaopenda masuala ya uwindaji wa kitalii kujitokeza kwa wingi kushiriki.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post