Kwanini inakuwa ni shughuli pevu kumpata mwanaume muafaka

Kwanini inakuwa ni shughuli pevu kumpata mwanaume muafaka

Kwa mwanamke kumpata mwanaume mwenye muafaka, yaani mwanaume ambaye ni husband material si kazi rahisi. Inaweza kuchukua miezi kama siyo miaka ya kucheza pata potea kabla ya kumpata mwanaume halisi wa ndoto yako. Hata hivyo wakati mwingine inaweza kutokea mwanamke akafanya majaribio kadhaa ya kuwa na mitoko (dating) na wanaume tofauti tofauti na bado akajikuta anatoka kapa, yaani hakuna hata mmoja anayefikia viwango vyake alivyojiwekea na kujikuta umri unasonga na bado yuko single.


Hapa chini nitaeleza sababu zinazosababisha wanawake wengi kukwama pale wanapokuwa kwenye harakati za kutafuta waume wa ndoto zao:

1. Hujui unatafuta mwanaume wa aina gani?

Huu ni ujinga unaofanywa na wanawake wengi. Kuna idadi ya kutosha ya wanawake ambao wanakuwa na mitoko na wanaume wa aina tofauti tofauti lakini ndani ya nafsi zao hawajui wanataka kuolewa na mwanaume wa aina gani. Mbaya zaidi wanawake hawa wanajikuta wakipoteza muda wao mwingi wa kuwa na mitoko lakini hawajui wanachokitafuta, mwisho wa siku hujikuta akiwa ametoka na wanaume wengi sana lakini hakuna hata mmoja waliyemuona anafaa, na jambo hilo huwa linawachanganya na kujikuta wakiwa na msongo wa mawazo, kumbe masikini ya Mungu hawajui kwamba mwanaume wanayemtafuta anafananaje.

2. Kujihisi kutokuwa salama

Kama mwanamke anajihisi kutokuwa salama anapokuwa na mtoko na mwanaume kunamuweka katika mazingira ya kutompata mwanaume anayemtarajia kwa sababu hana uhakika anatafuta mwanaume wa aina gani. Kutojiamini kwa mwanamke kunamfanya kushindwa kufanya juhudi binafsi za kumnasa mwanaume wa ndoto zake kutokana na kujiuliza maswali mengi kwamba mwanaume aliye mbele yake ndiye au siye? Mwanamke kutokuwa na uhakika kama atataka mwanaume wa aina gani kunamuweka katika mazingira ya kushindwa kumvutia mwanaume mwenye muafaka hata kama atakuwa na mtoko naye mara kadhaa.

3. Ukosefu wa mbinu za kuwanasa wanaume wenye muafaka

Kwa kawaida kila mtu ana udhaifu wake, hivyo linapokuja suala la mtoko, kila mmoja anajaribu kuwa makini kuficha udhaifu wake. Ukweli ni kwamba jambo hilo linaweza kuwa ni kikwazo kwa mwanamke kumpata mwenza sahihi. Unakuta mwanamke anakuwa na mtoko na mwanaume na katika mazungumzo tu ya kawaida anajitahidi sana kutotofautiana na mwanaume aliyetoka naye au anajifanya ni malaika asiyekosea na kujitahidi kutoonyesha rangi yake halisi kwamba yeye ni mwanamke wa aina gani.


  1. Mwanamke anaweka nguvu nyingi kwa aina moja ya mwanaume anayemtarajia

Katika mchakato wa kuwa na mitoko, mwanamke anakuwa amejiwekea aina moja ya mwanaume anayemtaka na anaelekeza nguvu nyingi katika kumtafuta mwanaume wa aina hiyo hiyo. Si vibaya kujiwekea malengo na matarajio kwa aina ya mwanaume unayemtaka lakini iwapo vigezo vyako vitakufunga kwa aina moja tu ya mwanaume unayemtarajia, basi hilo ni tatizo. Jaribu kutoka kidogo nje ya vigezo ulivyojiwekea kwani inaweza kukusaidi kujua aina tofauti tofauti za wanaume...

5. Bado unatembea na kumbukumbu ya mwanaume/wanaume ulioachana nao
Kwa kawaida wakati mwingine ni ngumu sana kuendelea na maisha yako ya kawaida baada ya kuachana na mpenzi wako uliyempenda sana, hasa kama mlikuwa pamoja kwa kipindi kirefu kidogo na mlipendana sana. Hata hivyo kama bado moyo wako umekuwa ni mgumu kumsahau mpenzi wako mliyeachana itakuwa ni vigumu kuwa na mitoko na kumpata mwanaume wa ndoto zako. Kwa kifupi ni kwamba hutofanikiwa kwa sababu hauko tayari.

6. Unajitahidi sana kuchukua tahadhari kupita kiasi....

Baada ya kuwa mwanamke ameumizwa sana katika mahusiano yake ya nyuma mara nyingi humuwia vigumu kusahau na kusonga mbele. Lakini pia huyachukulia mahusiano kwa tahadhari kubwa. Kwa kawaida si ajabu kukuta mwanamke aliyetendwa akiwa amejiwekea ulinzi madhubuti dhidi ya wanaume akijitahidi kwa kadiri awezavyo kuwakwepa na hata kuwakataa au kuwakatisha tamaa kwa kuogopa kuumizwa tena.
7. Kazi inachukua sehemu kubwa ya maisha yako...

Mtu kuipenda kazi yake siyo kitu kibaya, lakini si vyema kazi yako ikachukua sehemu kubwa ya maisha yako na muda wako kiasi cha kukufanya ushindwe kujichanganya katika mambo ya kijamii au kuwa na mitoko itakayokukutanisha na watu mbalimbali wa kubadilishana nao uzoefu. Wakati mwingine mwanamke anaweza akajikuta hapati mwanaume wa kumuomba mtoko kwa sababu ya kuonekana kwake kuwa na udhati (serious) na mambo yake au kazi yake.

8. Kuwa na mtazamo hasi (Negative) kuhusu wanaume

Huwezi kamwe kumpata mwanaume wa ndoto zako kama una mtazamo hasi kuhusu wanaume. Kama unatawaliwa na fikra za kukata tamaa au kuna sauti ndani yako (little Voices) zinakwambia kamwe huwezi kumpata mwanaume sahihi kwa sababu wanaume wa kuoa wamekwisha au hawapo na ukaamini na kujenga hofu, ni dhahiri kwamba haitatokea kumpata mwanaume sahihi kama ulivyoamini. Kumbuka kwamba sisi ni kile tunachowaza na kuamini kwa hiyo ni kiasi tu cha kubadilisha mawimbi yako ya namna ya kufikiri kwa kuwaza mambo mazuri unayoyahitaji huku ukiamini kabisa kwamba inawezekana.

9. Kila mwanaume anayekuomba mtoko unagundua siyo sahihi kwako

Kuwavuta wanaume wasio sahihi na wasiokidhi viwango vyako kunachangiwa na mambo mengi. Hebu chunguza mawazo yako, chunguza marafiki zako unaoambatana nao, chunguza maeneo unayoishi, chunguza maeneo unayotembelea, Je wewe ni mwanamke wa aina gani, una tabia gani nk..... Ni vyema kama unajiwekea malengo ya kumpata mwanaume mwenye tabia uzitakazo, basi mchakato wa kumpata ni pamoja na kujiweka katika mazingira ya kumvutia mwanaume huyo.

10. Unawalinganisha wanaume kupita kiasi

Ni vyema kujifunza kutokana na makosa uliyowahi kuyafanya katika mahusiano yako ya nyuma, lakini makosa hayo yasigeuke na kuathiri mtazamo wako kuhusu wanaume. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba si vyema kumlinganisha kila mwanaume unayekutana naye na mwanaume uliyewahi kuwa na uhusiano naye huko nyuma. Kila unapokuwa na mtoko na mwanaume nenda huku kichwa chako kikiwa kitupu kabisa ili kupata mtazamo mpya kuhusu mwanaume huyo kutokana na mazungumzo yenu.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post