FCC yakamata Bidhaa feki soko la Kariakoo

FCC yakamata Bidhaa feki soko la Kariakoo

Tume ya Ushindani (FCC) kwa kushiriki na Jeshi la Polisi nchini imekamata bidhaa feki zikiwemo za rungu max zenye thamani ya zaidi ya Milioni mbili, katika operesheni ya kushtukiza iliyofanyika katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Kazi hiyo ya ukamataji imefanyika baada ya kuwepo kwa taarifa ya bidhaa feki aina ya viwembe ambavyo vimeingizwa nchini na kuwekewa nembo ya ‘rungu max’ kinyume na taratibu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika mtaa wa mchikikuchini mara baada ya kumaliza operesheni hiyo, Meneja Mauzo Kampuni ya Rungu, Noel Lema alisema watafanya uchunguzi nchi nzima kuhakikisha wanapata bidhaa zote ambazo ni feki na zinatumia jina la kampuni hiyo.

Alisema duka walilofanya ukaguzi walibaini bidhaa feki aina ya viwembe vilivyokuwa na lebo ya kampuni yao vikiwa na thamani ya zaidi ya milioni mbili.

“Bidhaa wanazotengeneza hususani za rungu max wamekopi vizuri nembo yetu na rangi tunayotumia, wembe asilia imetengenezwa kwa ubora na kudhibitishwa na TBS (Shirika la Viwango Tanzania) hizi za kwao ni hatari kwa afya ya watumiaji hivyo ni muhimu kuzikamata na kuziteketeza,” alisema

Akifafanua bei ya katoni moja ya Rungu iliyothibitishwa na TBS ni Sh.590,000  huku bidhaa feki ikiuzwa Sh.350,000.

Naye mfanyabiashara wa duka lililokamatwa na bidhaa feki, Stephen Njira alisema kuwa bidhaa hizo alizokamatwa nazo amekuwa akiznunua kutoka kwa wamachinga huku nyingine akidai kuwa anaagiza.

“Bidhaa za rungu mimi nanunua kutoka kwa wamachinga lakini nyingine nimekuwa nikiagiza sehemu mbalimbali hapa nchini,” alisema

Kazi ya ukamataji wa bidhaa hizo umefanywa na maofisa wa FCC na askari polisi Kituo cha Msimbazi, hata hivyo maofisa hao wa tume hawakuweza kuzungumza na vyombo vya habari kwa madai kuwa msemaji wao aliyepaswa kuzungumza amepata dharura.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post