Fanya haya kukabiliana na mazingira magumu kazini

Fanya haya kukabiliana na mazingira magumu kazini

Na Aisha Lungato

 

Kauli mbiu inasema ‘Kazi iendelee’ hakuna kuchoka, leo sasa kwenye segment yako pendwa kabisa ya Kazi tutajuzani ni kwa vipi unaweza kukabiliana na mazungira magumu kazini haijalishi ni yakimazingira au watu waliokuzunguka.

 Nadhani wote tunafahamu kuwa hata watu wanaokuzunguka wanaweza kukufanya ukapata ugumu katika kazi yako, so unatakiwa kujua unaishi nao vipi basi ungana nami mwanzo mpaka mwisho kujua hili kwa undani zaidi.

 

Siyo kitu cha ajabu kuchukia kazi yako lakini, mara nyingine chuki yako ya kazi haisababishwi na kazi yenyewe, bali watu unaofanya nao kazi na mazingira kiujumla.

Pia, kuacha kazi hapo siyo solution ambayo inaweza kukusaidia kuepukana na tatizo hilo, unaweza kwenda katika kampuni nyingine ukakuta hali ni ileile na ndiyo maana waswahili wanasema ‘umeruka mjivu ukakanyaga mato’ maana hauna ambacho umekikwepa.
 

       Weka rekodi ya kila kitu

Kama unafanya kazi na boss au mfanyakazi mwenza msumbufu, hakikisha mawasiliano yote kati yenu yanafanyika kwa njia ya maandishi kama barua pepe.

Hakikisha unatumia lugha safi, na pale mnapo kwazana usijaribu kumtolea maneno makali hii itakusaidia hasa, mfano wakati mfanyakazi mwenzako atakapo kutusi basi itachukuliwa kama ushahidi hapo baadaye.

       Achana na umbea

Usiongeze ukubwa wa matatizo kwa kusambaza habari kuhusu boss wako au mfanyakazi mwingine ofisini, hata kama wanamakosa basi jitahidi kuwa na kifua watoto wa mjini wanasema ‘friji lako ligandishe’ sometime ugumu unauanzisha wewe kutokana na maneno ya chini chini unayozusha na kupelekea wenzako kukuchukia.

       Omba ushauri kutoka kwa Afisa Rasilimali Watu (HR).

 

Kama tatizo limekuwa kubwa kiasi kwamba mahala pakazi si sehemu salama basi wasiliana na HR. Usiogope kutoa taarifa hata kama tatizo linamhusisha boss wako. Ni wajibu wa HR kuhakikisha kuwa mahala pa kazi ni sehemu salama kwako. Pia, hii ni namna moja wapo ya kuweka rekodi ya tatizo kwa ajili ya kujilinda kama itatokea kesi ya kisheria.

 

      Zingatia malengo yako

Mahala pa kazi pagumu panaweza kukufanya usahau kwa nini ulikubali kazi hapo mwanzoni. Kama unapenda kazi unayoifanya lakini unakerwa na watu unaofanya nao kazi, elekeza nguvu zako kwenye kufikia malengo yako ya kikazi. Jitihada zako zitakuwezesha kupita vikwazo vyote.

 

      Tafuta kitu cha ziada cha kufanya

Wakati mwingine kuwa na jambo la kufanya nje ya kazi unalolipenda kunaweza kuongeza uwiano kati ya maisha yako binafsi na maisha yako ya kazi, hivyo kukuwezesha kuendelea na kazi, tafuta hata biashara ufanye hii itakusaidia kutoweka kichwani mambo magumu unayopitia kazini kwa sababu utakuwa unawaza tuu kuhusiana na biashara yako imeendaje.

       Tafuta mtu wa kuongea naye nje ya kazi

Ni vizuri kuzungumza kuhusu matatizo yako na mtu anae kujali, ambaye anaweza kukupa ushauri mzuri, lakini jitahidi mtu huyo awe wa nje ya kazini kwako ili kuepuka umbea na maneno yasiyo ya msingi.

       Tumia muda wako kutafakari

Kama unapata matatizo mara kwa mara na watu tofauti kazini, inabidi ujitathmini kama wewe ndiyo mwenye tatizo. Angalia matukio ambayo yalisababisha mgogoro, na wewe ulihusika vipi. Kama huoni makosa yako, jaribu kushirikisha mtu mwingine usikie mtazamo wake.

      Tengeneza mkakati wa kuondoka

Kama yote haya yameshindikana na huoni njia ya kutatua matatizo yako basi ni bora upange mkakati wa kuondoka. Jipangie muda wa kutafuta kazi na kuacha kazi uliyonayo, Pia unaweza kuhifadhi sehemu ya kipato chako kikusaidie pale utakapoacha kazi kabla hujapata nyingine. Kawaida ukishapanga mkakati wa kuondoka utapata ahueni sababu unajua unaondoka lini, hivyo unajua mwisho wa matatizo yako.

Unapofanya kazi na watu wasumbufu au sehemu yenye sera zinazobana, inatakiwa ujue ni nini kipo kwenye uwezo wako kubadilisha au kudhibiti. Lakini hauwezi kudhibiti tabia za wafanyakazi wenzako, huwezi kuwafanya wawe watu wakarimu, hivyo usijaribu kufanya hivyo, maana utakuwa unajisumbua.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post