CCM yampongeza Rais Samia kutunukiwa Uchifu

CCM yampongeza Rais Samia kutunukiwa Uchifu

Chama  Cha  Mapinduzi  (CCM) kimesema kitaendelea kupiga vita  sera za udini, ukanda  na  ukabila lakini hakitaacha kutowatambua machifu na watemi hivyo kinawapongeza umoja wa machifu Tanzania kwa kumsimika Rais  Samia Suluhu  Hassan uchifu mkuu wa machifu wote nchini.

Pia Chama hicho  kimesema pamoja na kwamba  sera za TANU na baadae CCM kutoruhusu tawala za kichifu na kitemi  hiyo  haina maana koo za kichifu na mchango wao kwa nchi yetu zisitambuliwe.

Ufafanuzi huo umetolewa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi  na Uenezi, Shaka  Hamdu  Shaka  aliyetakiwa kutoa maelezo iwapo Rais Samia kusimikwa uchifu mkuu ni kushabikia ukabila na kueleza wanaokosoa kitendo  hicho wanatakiwa wafanye rejea ya historia kabla ya kusema hayo.

Shaka alisema hata Rais wa kwanza Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye ndiye aliyekuwa  mstari wa mbele kupiga vita himaya za kichifu na kukomesha ukabila ili kujenga misingi imara ya umoja wa kitaifa alikuwa akivikwa mavazi ya kimila na kupewa hadhi za uchifu kwenye makabila yote alipokuwa Rais wa nchi yetu.

Alisema  wanaodai kitendo cha Rais Samia kupewa hadhi ya uchifu mkuu wa machifu  wote nchini ni kushabikia ukabila waelewe kuwa hiyo ni hadhi inayotolewa kwa watu muhimu na waliotoa mchango mkubwa kwenye jamii zao kama ile itolewayo na vyuo vikuu duniani kote ikiwemo udaktari wa heshima.

"Hatutashabikia ukabila, udini wala ukanda lakini muhimu ikafahamika CCM hakitabeza utamaduni, mila na desturi zetu ambazo ni chanya ikiwemo kuutambua utemi, uchifu na viongozi wa mila kwani kufanya hivyo sio kuendeleza ukabila" Alisema Shaka

Aidha  katibu huyo mwenezi alisema hata baada ya mwalimu Nyerere kukomesha ukabila alionekana akivikwa mavazi  ya kitamaduni na kiasili katika makabila mbalimbali,  mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati mzee Benjamin Mkapa, Dkt Jakaya Kikwete na hayatI Dkt John Magufuli wote walitunukiwa heshima hizo.

"Kwa kuwa wapo washindani wetu wa kisiasa na wamekosa hoja basi watakosoa kila kitu ambacho CCM na viongozi wake itafanya. Hata mwanasiasa Theresa Ntare wa kabila la Waha huko kigoma alitambuliwa kwa heshima yake na akaitwa Mwami Ntare hata baada ya uhuru." Alisema Shaka

Shaka alisisitiza kuwa CCM wakati wote itatambua, itathamini na itaenzi mchango wa machifu na watemi kama vile kina Mangi Meli, Chifu Kimweri wa Usambara, Mtemi Mirambo wa unyanyembe, Makunganya, Kinjikitile Ngwake na  kina chifu Songea, Nkossy na Mkwawa ambao walikuwa mstari wa mbele kupigania uhuru na ukombozi wa Mwafrika dhidi ya wakoloni.

Pia katibu huyo alisema machifu na watemi wameshiriki juhudi za mapambano kupinga tawala za kijerumani na kiingereza kwa kuwaeleza kinagaubaga waondoke ili wajitawale wenyewe.

"Hatuwezi kuzungumzia uhuru wa Tanganyika au mapinduzi ya  Zanzibar bila kutambua na kuthamini mchango wa machifu, watemi, viongozi wa kijadi na kimila.

Ndiyo maana katika kuenzi mchango wao yapo maeneo mengi ya umma yaliyopewa majina yao kama vile kuna mitaa imeitwa Kimweri, Makunganya; shule zinazoitwa Mkwawa, Mirambo nk" alieleza Shaka

Hata hivyo CCM wamesifu uamuzi wa machifu na watemi kuamua kumsimika uchifu mkuu Rais Samia mkoani mwanza kutokana na umahiri wa uongozi wake katika kutetea maslahi ya Taifa.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post