Athari za kupaka make up mara kwa mara

Athari za kupaka make up mara kwa mara

Ufanyaji wa makeup haswa kwa wanawake umejizolea umaarufu sana haswa miaka ya hivi karibuni na kupelekea mwanamke wengi kushindwa kwenda katika sherehe bila ya kufanya hivyo.

Inawezekana wewe ni mmoja wa warembo ambao haiwezi kupita siku bila kufanya makeup na inawezekana kwa kiasi fulani, makeup inakuongezea ujasiri wa muonekano wako.

Lakini inasemekana kuwa matumizi ya mara kwa mara ya makeup bila kuzingatia utunzaji wa ngozi yako huweza kupelekea athari mbalimbali ikiwemo ngozi kuzeeka na kukosa nuru.

Akizungumza na Jarida la  Mwananchi scoop Mtaalamu wa Masula ya Makeup na ngozi ambaye ana uzoefu wa takribani miaka 6 katika fani hiyo, Candynesh Fourine kutoka Candynesh Saloon and Makeup Studio ilioko Kawe Ukwamani iliyopo jirani na sheli ya Puma jijini Dar es Salaam alisema kuwa ni kweli mtu anapofanya makeup mara kwa mara bila kuzingatia utunzaji na usafi wa ngozi huweza kupelekea athari mbalimbali.

“Ngozi inahitaji kupumua na usafi, kabla ya kumpaka mtu makeup huwa kuna vitu vinatangulizwa kupakwa ili kutoa muonekano mzuri na kama ngozi ni kavu na unapaka foundation ya mafuta vitundu hivyo vya hewa katika ngozi huwa vinaziba na kushindwa kupumua,”alisema.

Nini cha kufanya kuzuia hilo

Candynesh alisema kwa mwanamke ambaye kutokana na mazingira aliyopo yanamlazimu kufanya makeup kila siku ni muhimu kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo utoaji sahihi wa makeup usoni.

“Ni muhimu kuwa makini sana haswa kipindi unapohitaji kuondoa makeup yako usoni kwani utoaji wa makeup kiholela na kuhakikisha makeup yote inaondoka usoni,”alisema.

Aliongezea kuwa ni vyema pia awe anafanya matibabu ya ngozi mara kwa mara ikiwemo scrub kila baada ya siku mbili au tatu ili kuirudisha ngozi katika uwiano unaohitajika.

Mambo ya kuzingatia wakati wa kufanya/kumfanyia mtu makeup

Candynesh alisema kabla ya kufanyiwa mtu makeup kitu cha msingi ni kuangalia na kujua aina ya ngozi ya mtu unaetaka kumfanyia makeup.

“Kuna wateja wenye ngozi zenye mafuta na kavu, wengine ngozi zao zina aleji na aina fulani ya kipodozi hivyo kuzingatia kwanza ngozi ya mteja na aina ya vifaa vinavyoendana na ngozi yake vitakusaidia kutoa muonekano ambao mteja ataufurahia,”alisema.

Pia, alieleza kuwa ni muhimu kabla ya makeup uso kufanyiwa usafi na kuhakikisha hauna uchafu wa aina yeyote .

Pia alieleza mbali na uzingatiaji wa  ngozi na vifaa kwa ajili ya kupata muonekano mzuri ni vyema kufanya makeup kwa kutumia vifaa orijino na kuhakikisha mtu anaehitaji kufanyiwa makeup afanye kwa mtaalamu wa kazi hizo.

“Ni muhimu kufanya makeup kwa mtaalamu kwa kuwa anakuwa amesomea na anafahamu vyema kila aina ya ngozi na vifaa gani atumie kukupa muonekano unaouhitaji,”alisema.

Alisema mtaalamu wa makeup anajua kila aina ya ngozi na vifaa vyake vya kufanyia makeup kwani kila aina ya ngozi ina namna yake ya ufanyaji wa makeup.

Changamoto

Alisema kuna wakati amekuwa akipokea wateja wa kufanyiwa makeup ambao hawazingatii usafi na kujali ngozi zao.

“Lakini kwa kuwa mimi ni mtaalamu wa ngozi huwasaidia kuziweka ngozi zao katika hali nzuri kabla ya kuwafanyia makeup, pia huwa ninawapa ushauri ya mambo gani wanapaswa kuzingatia ili ngozi zao ziwe safi na zenye afya,”aliongeza.

Pia alisema changamoto nyingine ni gharama kubwa ya ununuaji wa vifaa vya makeup orijino ambavyo ndivyo huhitajika katika kutoa muonekano mzuri.

 

Watu anaotamani kuwafanyia makeup

Candynesh alisema kwa siku nyingi amekuwa na ndoto siku moja aweze kuwafanyia makeup watu mashuhuri ambao jitihada zao huwa zinamuhamasisha zaidi kupambana kuzidi kuzifikia ndoto zake.

Watu hao Mashuhuri ni pamoja na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo.

“Watu hawa wananivutia kutokana na namna wanavyofanya kazi zao za uongozi kwa ufanisi na kuionyesha dunia kuwa wanawake tunaweza,”

Aliongeza: Najua ni ndoto ambayo inaonekana kama ngumu kutimia lakini nina imani ipo siku nitaweza kuwapendezesha viongozi hao

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post