Mahakama yatupa ombi la wosia mjane wa Mengi

Mahakama yatupa ombi la wosia mjane wa Mengi

Mahakama ya Rufani imetupilia mbali shauri la maombi ya marejeo lililofunguliwa na mjane wa Reginald Mengi, Jacquiline Ntuyabaliwe na wanawe wawili, ambao wamekuwa wakipambana kutetea wosia unaodaiwa kuandikwa na Mengi ambao Mahakama Kuu iliubatilisha.

Katika shauri hilo, Jacquiline na wanawe anaowasimamia, Jayden Kihoza Mengi na Ryan Saashisha Mengi walikuwa wanaiomba mahakama irejee na hatimaye itengue uamuzi uliotupilia mbali shauri la maombi ya mapitio, walilolifungua awali mahakamani hapo wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu, iliyoukataa wosia huo.

Hata hivyo, katika shauri hilo la maombi ya marejeo namba 748/01 la mwaka 2022, mahakama hiyo katika uamuzi imewakatalia maombi ya kuurejea uamuzi huo ikisema sababu zilizotolewa hazina mashiko.

Katika uamuzi huo uliotolewa na jopo la majaji watatu waliosikiliza shauri hilo, Rehema Mkuye (kiongozi wa jopo), Abraham Mwampashi na Zainabu Muruke, mahakama imesema sababu walizozitoa si miongoni mwa zile za kuomba mahakama kufanya marejeo ya hukumu yake, bali zinahusu rufaa.

Uamuzi huo ulioandikwa na Jaji Muruke kwa niaba ya jopo hilo, ulitolewa Agosti 5, 2024 na unapatikana katika tovuti ya Mahakama iitwayo Tanzlii.


Chimbuko la shauri hilo

Shauri hilo linaanzia katika lingine la msingi la mirathi ya marehemu Mengi, aliyefariki dunia Mei 2, 2019. Mengi alikuwa mfanyabiashara maarufu nchini, alifariki akiwa Dubai.

Shauri hilo la mirathi namba 39/2019 lilifunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na mtoto wa ndugu yake hayati Mengi, Benson Benjamin Mengi, kwa pamoja na watu wengine watatu; William Mushi, Zoebu Hassuji na Sylvia Mushi.

Walikuwa wakiomba kuteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi kwa mujibu wa wosia huo uliodaiwa kuachwa na Mengi.

Wosia huo ulikuwa unampa Jacquiline na wanawe pekee haki ya urithi wa mali zote za Mengi.

Hata hivyo, mtoto mkubwa wa Mengi aitwaye Abdiel na mdogo wa hayati Mengi, Benjamin Abraham waliweka pingamizi katika shauri hilo la mirathi wakipinga uhalali wake.

Mahakama Kuu katika hukumu iliyotolewa na Jaji Yose Mlyambina, Machi 18, 2021 ilikubaliana na sababu na hoja za pingamizi hilo dhidi ya wosia huo na ikaukataa ikiamuru kuwa ni batili.

Pamoja na mambo mengine, Jaji Mlyambina alisema unawanyima urithi watoto wengine wa marehemu, (Abdiel na ndugu yake Regina) bila kutoa sababu.

Sababu nyingine alisema ziliingizwa mali za mke wake wa kwanza (Mercy Anna Mengi, waliyekuwa wameshatalikiana), pia kutokana na mjane huyo (Jacquiline) ambaye wosia huo ulimtambua kama mnufaika.

Jaji Mlyambina aliwateua Abdiel na Benjamin kuwa wasimamizi wa mirathi na akaelekeza mali za marehemu zigawiwe warithi wanaostahili kwa utaratibu wa kawaida kama wa mtu ambaye hakuacha wosia.

Jacquiline na wanawe kupitia kwa wakili wao, Audax Kahendaguza, walifungua shauri la mapitio Mahakama ya Rufani wakiiomba ipitie hukumu hiyo na hatimaye iitengue amri ya kukataa wosia huo na uteuzi wa kina Abdiel, badala yake iwateue waliofungua shauri la mirathi.

Mahakama katika uamuzi uliotolewa Desemba Mosi, 2022 na jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye (kiongozi), Dk Paul Kihwelu na Panterine Kente waliosikiliza shauri hilo la mapitio ililitupilia mbali.

Mahakama iliamua hivyo, baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi lililoibuliwa na wasimamizi walioteuliwa na Mahakama Kuu, Abdiel na Benjamin, kuwa viapo vilivyokuwa vinaunga mkono maombi hayo vilikuwa na kasoro za kisheria.


Shauri la marejeo

Baada ya uamuzi huo, Jacquiline na wanawe walifungua shauri la marejeo, dhidi ya wasimamizi walioteuliwa na Mahakama Kuu, Abdiel na Benjamin pamoja na waliofungua shauri la msingi la mirathi, Benson, William, Zoeb na Sylvia Mushi.

Katika shauri hilo waliiomba Mahakama itengue uamuzi wake uliotupilia mbali shauri lao la maombi ya mapitio, wakidai ulikuwa na kasoro, huku akibainisha sababu tatu kuiomba Mahakama ifanye marejeo ya uamuzi wake wa awali, na hatimaye iutengue.

Waombaji walikilishwa na wakili Kahendaguza na wajibu maombi wa kwanza mpaka wa tatu (Abdiel, Benjamin na Benson), waliwakilishwa na wakili Roman Masumbuko, huku wajibu maombi wa nne mpaka wa sita (William, Zoeb na Sylvia mtawalia) wakiwakilishwa na Eliasa Msuya.

Sababu za maombi, uamuzi

Katika sababu za kuomba mahakama ifanye marejeo ya uamuzi wake wa kutupilia shauri lao la mapitio, kwanza walidai kulikuwa na makosa ya dhahiri katika kumbukumbu za shauri hilo yaliyosababisha haki kutotendeka.

Waliilalamikia mahakama kuwa haikukipa uzito kiapo kilichounga mkono shauri lao la maombi ya mapitio.

Baada ya kujadili sababu hiyo, huku ikirejea uamuzi wake katika mashauri mbalimbali kuhusu suala hilo, mahakama imesema kwa kuangalia kumbukumbu hizo zilizozungumziwa katika shauri hilo la marejeo, siyo sahihi kuwa kuna makosa ya dhahiri.

Imesema hoja hiyo tayari ilishaamriwa wakati wa kuamua shauri la mapitio, ikieleza alichokifanya wakili wa mwombaji ilikuwa ni njia nyingine ya kuhoji pingamizi lililowasilishwa kwenye shauri la mapitio kwa njia ya marejeo.

“Kwa maoni yetu kosa lililolalamikiwa na waombaji siyo la dhahiri, linahitaji mchakato wa uchunguzi na uchambuzi, hivyo si kosa la dhahiri kwenye kumbukumbu kiasi cha kuhitaji kufanyiwa marejeo," unaeleza uamuzi huo.

Sababu ya pili ya kuomba marejeo ilikuwa kutokupewa haki ya kusikilizwa na ubatili wa uamuzi huo (kutupilia maombi yao ya mapitio), kwamba mahakama ilikubaliana na pingamizi na kutupilia mbali shauri lao la mapitio bila kuwasikiliza.

Mahakama imesema bila kupoteza muda pande zote zilisikilizwa kuhusu pingamizi hilo.

“Lengo la marejeo si kutoa kwa wadaawa walioshindwa kwa njia ya mlango wa nyuma kujadili tena kesi yao. Kwa ujumla wake hoja hii inakosa mashiko,” imesema mahakama.

Sababu ya tatu ilihusu mamlaka ya mahakama, kuhusu uamuzi wa Oktoba 12, 2021 juu ya pingamizi la awali lililoibuliwa na wajibu maombi dhidi ya shauri la mapitio.

Mahakama imesema kumbukumbu za mwenendo wa shauri hilo zinaonyesha wadaawa wote waliridhia na kukubaliana na mamlaka ya Mahakama kusikiliza pingamizi hilo.

Hivyo baada ya kujadili sababu hiyo kwa kina imehitimisha kuwa waombaji hawalalamikii mamlaka ya mahakama kusikiliza pingamizi la awali, bali ni matokeo yake, hivyo sababu ya tatu ya marejeo pia inakosa mashiko.

Mahakama imehitimisha kuwa kwa mtizamo wake hakuna sababu yoyote kati ya sababu na hoja zilizotolewa zinazokidhi masharti ya kanuni ya 60(1) (a) mpaka (e) ya Kanuni za Mahakama hiyo na kesi rejea.

Mahakama ilisema maombi hayako sawasawa, hayana mashiko na kuyatupilia mbali.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post