Kayumba: wasanii wengi hawana nidhamu, niliambiwa sitafika popote

Kayumba: wasanii wengi hawana nidhamu, niliambiwa sitafika popote

Miongoni mwa wasanii wa kizazi kipya, walioanza kuonekana, kujulikana kupitia mashindano ya kusaka vipaji, Bongo Star Search (BSS), ni Kayumba Juma 'Kayumba' ambaye mtaani anatamba na ngoma kama vile ‘mama’.

Mwanamuziki huyo wakati akizungumza na Mwananchi Scoop amesema kwa sasa nchini muziki umekua jambo linalopelekea wasanii kutotegemea shoo kuendesha maisha yao.

"Sasa hivi unakuta msanii hafanyi show ndani ya miezi hata mitatu na bado anapiga mkwanja kupitia vyanzo vyake vya mitandao ya kijamii. Kwa mwenendo huu naona miaka mitano ijayo tutakuja kuwa na wasanii wenye mikwanja mirefu na kushindana na baadhi ya nchi za Afrika,"amesema

Kuhusu ushindani wa muziki anasema "Kitu ambacho mashabiki hawakifahamu sisi hatupati changamoto kwa wasanii wa Tanzania tu, kuna Afrika na Dunia kwahiyo tunaweza kufanya kitu

Bongo Fleva damu

Licha ya kuwa wasanii Bongo ni wengi na kila mmoja kachagua aina ya muziki wa kupita nao, kwa upande  wake Kayumba amesema Bongo Fleva ipo kwenye damu.

"Mimi ni Bongo Fleva halisi na ndiyo muziki ulionilea hata kama nikifanya amapiano nitauweka kwenye ladha ya nyumbani siwezi kuikimbia mfano wimbo kama Mama, Wasiwasi, Chunga na Bomba ambazo zilifanya vizuri ukizisikiliza utagundua ni ladha ya nyumbani”,amesema

Nidhamu kipengele kwa wasanii

Amesema sababu kubwa inayowafanya wasanii wengi kusikika na kisha kupotea kwenye gemu ni kutokana na kuwa na nidhamu mbovu.

"Kuhusu kuja na kupoteza nadhani msanii ili ukamilike lazima uwe na nidhamu ufanye kazi kwa bidii, japokuwa kuna kushuka na kupanda ingawa unaposhuka wapo watakusaidia kupanda na wasanii wengi hawana nidhamu hicho ndiyo kinawaangusha, wengi wanavipaji,"amesema

Watatu wanamkosha

Mkongwe wa muziki wa Bongo fleva, Dully Sykes, Ali Kiba na Mr Blue ni miongoni mwa orodha ya wasanii watatu anaowakubali Kayumba.

 

 

"Ni wakongwe ninao wakubali sana na ukiangalia hadi sasa bado wanafanya vizuri na hiyo inatokana na kuwashirikisha wasanii wa sasa kwenye ngoma za pamoja na mambo yakaenda,"amesema

Changamoto

Anasema wasanii wachanga wanakumbana na changamoto nyingi ikiwemo fedha jambo linalowarudisha nyuma na kuwakatisha tamaa.

"Kikubwa wasanii tufanye kazi changamoto zipo na za kawaida hata mimi nilizipitia, watu wanaweka pesa ndefu kwenye muziki hivyo muda mwingine pesa inakuwa mbele." amesema Kayumba

"Niliwahi hadi kukataliwa, nikaambiwa ngoma zako haziwezi kuuza, wasanii kama ninyi hamfiki popote hivyo kama hauko imara na hautafanya kazi kwa bidii basi unakata tamaa kabisa."






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post