Kansa ya matiti

Kansa ya matiti

Katika kuelekea kilele cha kutoa elimu Kwa jamii juu ya ugonjwa wa kansa ya matiti tarehe 31 oktoba, jarida lako pendwa la Mwananchi scoop linakuletea nakala likifafanua Kwa kina kuhusu ugonjwa huu.

Kansa ya matiti ni uvimbe wenye madhara (mkusanyiko wa seli za kansa) unaotokana na seli za matiti. Pamoja na kuwa saratani ya matiti huwaathiri zaidi wanawake, huweza pia kuwapata wanaume. Kansa ya  matiti kwa wanaume hutokea kwa nadra, lakini pale itokeapo huleta madhara makubwa zaidi.

 Moja ya sababu ni kuchelewa kufanyiwa uchunguzi kwa sababu inapotokea wanafanyiwa uchunguzi kansa hii huwa imefikia hatua ya kusambaa. Dalili za saratani ya matiti kwa wanaume zinalingana na zile za wanawake, dalili kuu ikiwa ni uvimbe ndani ya  matiti au kubadilika kwa rangi kulizunguka titi au kutoa majimaji. Kansa ya matiti kwa wanaume huweza kutokea kwenye umri wo wote, lakini hujitokeza zaidi kwa wanaume wenye umri wa miaka 60 au zaidi. Katika mada yetu ya leo, tutazungumzia saratani ya  matiti kwa wanawake.

VISABABISHI VYA SARATANI

Kuna mambo kadhaa ambayo yameonekana kuwa na uhusiano, ama wa moja kwa moja au kwa kupitia vitu vingine, wa kusababisha saratani ya matiti, au kumfanya mtu au kundi la watu kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa huu kuliko wengine. Mambo hayo ni pamoja na

 

Jinsia: Ingawa, saratani ya matiti huweza kutokea kwa wote wanawake na wanaume, imeonekana kuwa wanawake ni waathirika wakubwa zaidi wa saratani hii ikilinganishwa na wanaume.

Umri: Uwezekano wa kupata saratani hii huendana na umri wa mtu. Kadiri umri wa mtu unavyoongezeka ndivyo pia uwezekano wa kupata saratani hii unavyozidi kuwa mkubwa. Wanawake walio na umri wa kuanzia miaka 50 wapo kwenye hatari kubwa (mara 2 au 3 zaidi) kuliko walio na umri wa miaka 45.

Uasili wa mtu: Saratani ya matiti hutokea zaidi kwa wanawake wazungu kuliko wanawake wa kiafrika au wenye asili ya afrika (weusi)

Uzazi: Wanawake ambao hawajazaa au kunyonyesha wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti. Wanawake wanaopata ujauzito kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 nao pia wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani hii.

Historia ya ugonjwa huu katika familia: Wanawake walio katika familia zenye historia ya ugonjwa huu wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti ukilinganisha na wale ambao hawana historia ya ugonjwa huu katika familia zao. Kwa mwanamke aliye na ndugu (mama, dada au mtoto) ambaye aliwahi kupata saratani hii kabla ya umri wa miaka 50, uwezekano wa mwanamke huyu kupata ugonjwa huu ni mara mbili ya yule ambaye hana historia hii.



Umri wa kuvunja ungo: Wanawake wanaovunja ungo (kupata hedhi) kabla ya umri wa miaka 12 wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.

Kuacha kupata hedhi: Kwa kawaida wanawake huacha kupata hedhi wafikapo miaka 45, hali ambayo kitaalamu hujulikana kama menopause. Wanawake wanaochelewa kuacha kupata hedhi, kwa mfano wale wanaoendelea kupata hedhi wakiwa na zaidi ya miaka 45, wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya matiti.

Historia ya saratani ya matiti: Wanawake ambao wamewahi kupata ugonjwa huu kwenye titi la upande mmoja hapo kabla, wana uwezekano mkubwa wa kupata tena saratani kwenye titi la upande mwingine hapo siku za usoni.

Ulaji wa vyakula venye mafuta mengi: Tafiti zinaonesha kuwa, wanawake wanaopendelea kula vyakula vyenye mafuta mengi wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.

Kuongezeka uzito: Tafiti nyingine zimeonesha kuwa, wanawake wanene wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti ukilinganisha na wale wa uzito mdogo au wa kati.

Uvutaji sigara: Kuna matokeo yenye kukinzana kuhusu uhusiano wa uvutaji sigara na hatari ya kupata saratani ya matiti. Wakati baadhi ya tafiti zinaonesha uhusiano wa karibu kati ya uvutaji sigara na uwezekano wa kupata saratani ya matiti, tafiti nyingine zinaonesha majibu yenye kutofautiana kuhusu uhusiano wa uvutaji wa sigara na saratani ya matiti. Hata hivyo, kwa ujumla, wanawake wanaojizuia kuvuta sigara wanakuwa na afya njema zaidi kuliko wale wanaovuta sigara.

Unywaji pombe: Imeonekana kuwa wanawake wanaokunywa pombe zaidi ya chupa moja kwa siku wana uwezekano wa kupata saratani ya matiti kwa asilimia zaidi ya ishirini.

Historia ya tiba ya mionzi: Wanawake ambao wamewahi kupata tiba ya mionzi hususani wakati wa ukuaji wa matiti, wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu. Hali hii husababishwa na ukweli kuwa mojawapo ya madhara ya mionzi ni kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya aina yoyote.

Matumizi ya dawa za kupanga uzazi: Kuna ushahidi kuwa saratani ya matiti ina uhusiano na matumizi ya muda mrefu ya vidonge vya kupanga uzazi.

Kuwepo kwa kiwango kikubwa cha homoni mwilini: Kwa wale wanaotumia tiba ya homoni inayojulikana kama hormone replacement therapy, kwa sababu nyingine yeyote ile, au wale wenye kiwango kikubwa cha homoni kama vile oestrogen na progesterone mwilini mwao wapo kwenye hatari zaidi ya kuugua saratani ya matiti.

Kuwa na matiti makubwa: Wanawake wenye matiti makubwa (dense breast tissue) wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti. Hali hii hutokana na ukweli kuwa wakati mwingine ni vigumu sana kwa madaktari kutambua kama wana saratani au la kutokana na ukubwa wa matiti yao.

DALILI ZA KANSA YA MATITI.

Dalili zinaweza kujumuisha uvimbe ndani ya titi, mabadiliko ya ukubwa au umbo la titi na chuchu kutoa majimaji.

Kuvimba kwa sehemu ya titi au titi lote (hata kama hakuna bonge unaloligusa)

Kuchubuka na kubonyea kwa ngozi ya titi

Maumivu ya titi au chuchu

Kurudi ndani kwa chuchu

Wekundu na kukakamaa kwa chuchu na ngozi ya titi

Kutokwa na majimaji

Matatizo mengine ya kiafya yanaweza kusababisha dalili hizi. Ni daktari pekee anayeweza kutofautisha kwa uhakika. Mtu yeyote mwenye dalili hizi anapaswa kumwona daktari ili tatizo lake ligunduliwe mapema iwezekanavyo.

WAKATI MUAFAKA WA KUMUONA DAKTARI.

  • Mwone mtoa huduma ya afya, kuhusu mabadiliko kwenye matiti kama:
  • Una uvimbe/donge ndani/karibu na titi au kwapa la mkono wako
  • Tishu ngumu ndani au karibu na titi au kwapa la mkono wako
  • Kuna majimaji yanatoka kwenye chuchu
  • Kuna maumivu kwenye chuchu
  • Chuchu imerudi ndani kwenye titi
  • Unawashwa ngozi, kuna mabadiliko kwenye ngozi kama vile wekundu, kukakamaa na kudumbukia kwa ngozi

Uchunguzi wa saratani ya matiti ni vyema wanawake kuanza uchunguzi wa matiti mapema kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea. Uchunguzi ufanyike mara moja kila mwezi, kati ya siku 3-5 baada ya kumaliza hedhi. Mwanamke aliyesitisha/ aliyekoma hedhi anaweza kujichunguza mwenyewe tarehe moja kila mwezi. Vipimo vya kitaalamu hushauriwa punde tu tatizo linapogunduliwa.

KUMBUKA:

-9 kati ya kila vivimbe 10 kwenye matiti ni magojwa yasiyo saratani

- Saratani ya matiti haiambukizi

- Asilimia moja ya wanaume hupata saratani ya matiti

- Mionzi hutumika kwenye tiba ya saratani ya matiti na sio chanzo cha saratani hiyo

- Kuondoa titi mapema ni tiba mojawapo ya saratani ya matiti na sio sababu ya kifo

MATIBABU YA KANSA YA MATITI.

Kuna aina tofauti tofauti za matibabu kwa wagonjwa wa saratani ya matiti. Lakini kuna aina kuu nne zinazotumiwa:

Upasuaji :Wagonjwa wengi wenye saratani ya matiti hufanyiwa upasuaji ili kuondoa kansa. Baadhi ya tezi za limfu (lymph nodes) kwenye kwapa huondolewa na kuchunguzwa kwa darubini pia,ili kuona kama zina seli za kansa.

Kama matiti ya mgonjwa yataondolewa ,daktari anaweza kuweka mpango wa kumtengenezea mgonjwa matiti mapya (reconstruction). Daktari anaweza kufanya hivyo kwa kutumia tishu za mgonjwa kutoka maeneo mengine au kwa kutumia silicone/saline implants.

 

Tiba ya mionzi: Tiba hii hutumia nguvu ya mionzi ya x-rays kuua seli za saratani au kuzuia zisiendelee kukua.

 

Tibakemikali: Ni aina ya matibabu ya kansa ambayo hutumia madawa ili kuzuia ukuaji wa seli za kansa au kuziua.

Unapokunywa au kuchomwa dawa kwenye mishipa, huingia kwenye mzunguko wako wa damu na kuzifikia seli zote za kansa kote mwilini (systemic chemotherapy).

Tiba ya homoni: Ni tiba ya kansa ambayo hupunguza homoni mwilini au kuzuia homoni zisifanye kazi ili kupunguza ukuaji wa seli za saratani. Baadhi ya homoni husababisha kansa fulani kukua kwa haraka zaidi. Homoni ya estrojeni inayotengenezwa na ovari husababisha kansa ya matiti kukua haraka zaidi. Tiba ya homoni hutolewa ili kupunguza uzalishwaji wa estrojeni.

NAMNA YA KUJILINDA.

  • Kuwa na uzoefu wa kujichunguza mwenyewe matiti yako mara kwa mara
  • Kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu angalau mara moja kwa mwaka Kufanyiwa uchunguzi wa matiii kwa njia ya mionzi angalau mara moja kwa mwaka kwa wenye umri zaidi ya miaka 40
  • Kupunguza/kuacha matumizi ya sigara na tumbaku
  • Kupunguza/kuacha matumizi ya mafuta kwa wingi kwenve chakula hasa yale yatokanayo na wanyama
  • Kula mbogamboga na matunda mara kwa mara Kuwa na uzito usiozidi
  • Kunyonyesha mtoto kwa muda mrefu iwezekanavyo

 

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post