Kama unadhani ni mate ya nyoka, unajidanganya

Kama unadhani ni mate ya nyoka, unajidanganya

Ni kawaida kuona povu linalofanana na mate kwenye mimea hasa asubuhi au kipindi cha masika.
Povu hilo wengi huamini ni mate ya nyoka na kusababisha kuogopa kuyashika.

Licha ya imani hizo, inaelezwa kuwa, povu hilo siyo mate ya nyoka bali ni majimaji yanayotolewa na wadudu waitwao 'Spittlebugs au Froghopper' wakiwa wadogo.

Kwa kawaida wadudu hao huyatoa kwa njia ya mfumo wa haja kubwa wakati wanakula kwenye shina la miti au majani.
Kwa mujibu wa tovuti za 'Wisconsin Horticulture', Nature History Museum na Missouri Department of Conservation, kadri wadudu hao wanavyokula ndivyo hutoa majimaji hayo ambayo huchanganyika na hewa; kupitia miguu yao huyakoroga majimaji hayo hadi kuwa katika mfumo wa povu.

Inaelezwa kuwa, povu hilo huwalinda wadudu hao ambao bado hawajakomaa dhidi ya wanyama waharibifu na kuwapa ulinzi wa mabadiliko ya joto na mazingira yenye unyevu mdogo ili waweze kukua vizuri.

Hata hivyo, baada ya muda mdudu huyo anavyoendelea kukua ndivyo povu hupungua kisha huisha na mdudu hutoka kwa kuruka akiwa kakamilika na kuanza maisha mapya.

Akizungumza na Mwananchi, Dennis Ikanda ambaye ni Mwanabiolojia wa Uhifadhi na Mtaalamu Wanyamapori kutoka Shirika la Wanyama Duniani (WWF), amesema ni kweli nyoka ana mate lakini hayawezi kutoka kwa wingi kama watu wanavyodhani. Mbali na hilo amesema mate hayo hayana sumu.

"Nyoka hatemi mate badala yake anarusha sumu, lakini kwa kuwa tumekariri mdomo una mate basi watu wanasema anatema mate, kwanza ni wachache wenye uwezo wa kurusha sumu, kawaida wao wana tundu chini ya ulimi linalotoka kwenye kimfuko ambacho ndicho kimehifadhi sumu, kwa hiyo hata nyoka ‘akikubusu’ huwezi ukafa.

"Kuna namna anavyofanya ili kurusha sumu, ananyanyua ulimi juu anajiminya shingoni ndiyo inaruka, kwa wale wanaouma matundu ya sumu yapo kwenye meno makubwa mawili yanakuwa kama sindano tunazochomwa, yanatundu dogo," amesema.
Ikanda amesema chini ya asilimia 20 ya nyoka ndiyo wenye sumu, na katika hao, wenye sumu inayoweza kumuua binadamu ni chini ya asilimia 5.

Amesema siyo kila nyoka anatakiwa kuuliwa wengine hawana muda na binadamu.
"Nyoka ana sumu siyo kwaajili ya kumuua binadamu, inamuwezesha kuua wanyama kama panya, ili apate chakula hawa wengine wakubwa kama Black Mamba, Cobra, Vifutu ambao wanamadhara kwa binadamu, wanakula wanyama wakubwa na ndiyo manaa ata sumu yao ni kali," amesema Ikanda.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post