Wapenzi wa filamu leo ni siku yenu, kwenye magazine hii tumewaletea mkali wa kuvaa uhusika kwenye upande wa filamu, Daud Michael maarufu kama Duma Actor, wengi wamekuwa wakimtazama kwenye filamu mbalimbali anazocheza lakini kupitia Magazine hii ameweza kufunguka mengi yanayomuhusu.
Kwanza mkali huyu alianza harakati za kujitafuta mwaka 2007 akiwa kwenye kundi la Bahari Artist Group, huku njia za mafanikio aliyopata tangu akiwa anafundishwa sanaa hadi kutimiza ndoto zake zikiwa ni juhudi, nidhamu na kupigania ndoto zake.
Ile kasumba ya baadhi ya watu kuingia kwenye sanaa kwa lengo la kutaka umaarufu au kubebwa na ma-director kutokana na mionekano yao bila ya kuwa na vipaji, muigizaji huyu amesema kuwa ni kati ya sababu kubwa inayopelekea baadhi ya wasanii wapya kwenye soko la sanaa ya maigizo kutambulika kwa muda mchache na kisha majina yao kusahaulika kwa haraka na kupotea kabisa kwenye ramani.
"Wasanii wengi wanakuja kwenye sanaa bila ya mission na vision, hawajui jinsi gani ya kufanya majina yao yaendelee kuwepo, hawako tajari ku-sacrifice maisha yao kwa ajili ya sanaa, hakuna kazi ngumu kama kulifanya jina liendelee kutajwa, wengi hawajajitoa kwa ajili ya sanaa wao wanataka sanaa ijitoe kwa ajili yao, ndiyo maana wanapote". Anasema Duma
Wazee wa kutafuta sababu na kupindisha maneno msanii huyu anasema kuwa kati ya kitu ambacho ni sumu kwenye maisha yake na huwa hakiamini katika mafanikio ni uongo, yaani hapendi mtu muongo anaenda mbali zaidi kuwa endapo mtu akimdanganya na akajua basi safari ya ushikaji itakuwa imefika mwisho, kutokana na hilo mkali huyu anasema mafanikio yanayotafutwa kwa njia za uongo huwa hayadumu bali mafanikio ya mtu mkweli ndiyo hudumu.
Licha ya mkali huyu kufanya vizuri kwenye upande wa filamu pia ni kati ya vijana wanaofanya wenye miradi yao mbalimbali ya kuwaingizia kipato, kwa upande mwingine tunaweza sema anajua haswa kutafuta maokoto, kutokana na hilo anatueleza siri ya mafanikio yake, anasema ni ngumu kumkuta na wazee wa kula bata la kupitiza kwani wengi hujikuta wakiwaza sana starehe tofauti na kujitafutia mafanikio yao binafsi hivyo basi muigizaji huyu watu wa namna hiyo hataki hata kuwasikia.
Waswahili husema ukimuona nyani mzee basi ujue amekwepa mishale mingi, ndivyo ilivyo pia kwa Muigizaji huyu ambaye amekomaa haswa kwenye upande wa filamu, yeye pia amewahi kukutana na changamito mbalimbali huku akiwa anakosea kwenye baadhi ya mambo, anasema amewahi kukosea vitu vingi hivyo mara nyingi huwa anarudi kwa Mungu kisha anajua njia gani alikosea na kuitatua.
"Mwaka 2020 nilipata matatizo makubwa ikafika hatua nikasema hichi nini? nikataka kuacha sanaa kwa sababu yenyewe ndiyo ilifanya nipate matatizo, nilifunguliwa kesi na TCRA laini yangu ikapigwa faini milioni 7, lakini kwa kuwa naamini Mungu anaendelea kunilinda kila siku, ndiyo maana nipo hapa". Anasema Duma
Na katika kuhakikisha hilo kuwa bado ni mkali kwenye filamu, licha ya kupitia misukosuko hiyo mwaka 2020 bado Duma ni kati ya watu waliojiongeza kwenda sambamba na ulimwengu wa dijitali kwani ni miongoni mwa wamiliki wa channel za YouTube ambayo imekuwa ikiwapatia mashabiki wake kazi zake mbalimbali ambazo anaziachia.
Leave a Reply