DESIGNER MSOMALI atamba na kazi ya ubunifu

DESIGNER MSOMALI atamba na kazi ya ubunifu

UBUNIFU ni uwezo wa mtu kuanzisha au kuvumbua kitu chochote kipya chenye utofauti na ubora zaidi katika jamii.

Hata hivyo imeelezwa kuwa ubunifu ni kitu au vitu fulani halisi, vinavyojitokeza katika soko kwa hali ya upya na kuleta mchango wa wazi kwenye jamii kwa ujumla.

Ubunifu unaweza kuwa wa mapambo, mavazi, karatasi na kazi nyingine za mitindo ya sanaa ambazo watu hubuni na kuzitumia kupitia maarifa na uwezo wao.

Saidi Haji Othman almaarufu ‘designer msomali’ ni mbunifu chipukizi wa mavazi ya kiume anayevalisha zaidi wasanii mbalimbali hususani waimbaji wa muziki wa SINGELI.

Baadhi wa wasanii wa muziki huo ambao anawavalisha kwa sasa ni Balaa Mc, Dogo Elisha, Dulaa Kanda, Brown Kapaso, Kiluza Fanani, Msomali Vitamin na wengine wengi.

Mbali na kuwavalisha wasanii hao lakini pia chimbuko la ubunifu wake limetokana na kuanza kuvalisha watu wa kawaida ambao sio maarufu ndiyo watu wake wa kwanza kumfungulia kipaji chake hicho.

Mwananchi Scoop imefanya mahojiano maalumu na mbunifu huyo na kuzungumza naye masuala mbalimbali kuhusiana na kazi yake hiyo.

Othman ameeleza kuwa, ubunifu ndiyo sehemu ya maisha yake na ndiyo kazi yake ya kila siku inayompatia kipato.

“Nimeanza kazi ya ubunifu miaka minne iliyopita na nilianzia chini kabisa nilikuwa nikitandika kitambaa kibarazani  mbele ya duka la mama yangu nami nikawa nauza nguo zangu za mitumba mahali hapo,”anasema na kuongeza

“Kipindi hicho nilikuwa nimeanza na kuuza trucks peke yake nakumbuka watu ndipo walipoanza kunitambua kupitia nguo hizo na kuifahamu zaidi kazi yangu,” anasema.

Wakati anaanza kazi hiyo mazingira aliyokuwa anafanyia yalikuwa magumu sana lakini kutokana na uwezo wa kipaji chake alipambana na kuhakikisha anatimiza malengo yake.

“Nakumbuka mtu wa kwanza kabisa kumvalisha nguo ambayo niliibuni mwenyewe hakua msanii alikuwa mtu wa kawaida aliniona nikiwa nimeivaa ilikuwa yangu na akaipenda na nilimtengenezea kwa bei niliyoitaka mimi na akaichukua,” anasema.

Hata hivyo, hapo awali kabla hajawa mbunifu wa mavazi kijana huyo alikuwa dereva ambaye alisomea kazi hiyo katika Chuo cha Ufundi Veta kilichopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

 “Nilipomaliza elimu yangu ya kidato cha nne ndo nikaamua kwenda kusomea udereva mwaka mmoja nikiwa najishikiza tu katika kazi hiyo huku mwenyewe nikiwa na malengo katika kazi ya ubunifu,” anasema.

 Haji anaeleza kuwa malengo yake hakutaka kazi ya udereva ndipo baada ya mafunzo hayo, alifanya kazi hiyo kwa muda na kupata fedha zilizomsaidia kuendeleza kipaji chake cha ubunifu.

“Nilifanikiwa kupata fremu na kuanza kufanya kazi yangu kwa utulivu ambapo nikawa nachukua nguo za mitumba nazitengeneza ninavyojua na kuziuza dukani kwangu hiyo ilivutia zaidi wateja wangu,” anasema na kuongeza kuwa

“Kwa sasa nauza hadi nguo za dukani kutokana na uhitaji wa wateja kwani wapo ambao wanapenda nguo za dukani pia hivyo nikaamua kujiongeza kwenye hilo.”

Vilevile Haji anaeleza kuwa mara nyingi akiwa kazini shughuli ambazo anazifanya akiwa hapo ni kuongeza zaidi ubunifu wake kwenye kazi zake.

“Kuna vitu mwenyewe najiongeza kama kutengeneza nguo ambazo mtu akiziona tu zinamvutia wakati mwengine naingia mtandaoni naangalia nguo mbalimbali kisha natengeneza hata kama nitaikosea lakini nahakikisha itamvutia mtu na akainunua,” anasema.

Aidha Haji ameweka wazi kuwa ana uwezo wa kuwavalisha na wasanii wengine ambao wako kwenye tasnia nyingine kama vile bongo fleva.

 Changamoto

Changamoto kubwa ambayo anaipitia mbunifu huyo chipukizi, anasema kuwa suala la kukubalika nyumbani ndiyo tatizo kubwa ambalo anapitia kwa sasa.

 “Kwanza kukubalika nyumbani ni changamoto ukiangalia watu wa nyumbani kukukubali ni kazi sana mtu kukubali chako ni ngumu sana watu watakudharau ila tunaenda nao hivyohivyo lakini kukubalika ni ngumu.”

Kutokana na changamoto hivyo dizaina Msomali anaeleza namna anavyokabiliana na tatizo hilo ili kuhakikisha anazidi kuimarika kwenye kazi yake hiyo.

“Huwa nabadilisha mfumo, unaweza ukaona pengine watu hawapendi mitumba basi najitahidi naweka na nguo za dukani tunaangalia watapenda za duka au watabaki vilevile hivyo tunawabadilishia.”

Vilevile Msomali anasema kitu ambacho anakizingatia zaidi kwenye kazi yake ni kujiongeza yeye mwenyewe kwa kuhakikisha anatoa kitu chake binafsi.

“Ndiyo maana mimi sihangaiki na nguo za dukani napenda sana kuuza nguo za mitumba kwa sababu najua sio rahisi mtu kuupita tena hata akivaa mtu atakiangalia tu hatoweza kujua anakipata wapi na atakayevaa ndiyo atakaekuja kuuliza kinapatikana wapi.”

Kipindi kigumu alichopitia kwenye kazi

Wakati ameanza kuuza nguo za mitumba dizaina Msomali anasema kuwa  kwa eneo la  Mbagala yeye ndiyo aliyekuwa mtu wa kwanza kufanya kazi hiyo, ila mara baada ya watu kuiona fursa hiyo ndipo alipoanza kupitia magumu kwenye kazi yake hiyo.

“Unakuta mtu naye anafungua duka kisha anauza bei ya chini kabisa kuliko ile ambayo nauza mimi lakini niliweza kupambana na suala hilo kwa kuhakikisha natoa kitu changu mwenyewe ambacho mteja ataoana utofauti na cha mtu mwengine,” anasema. 

Mafanikio

Dizaina Msomali anasema kuwa kwa sasa amepiga hatua kwenye kazi yake ukilinganisha na awali alivyoanza kuifanya shughuli hiyo kwani tayari amefanikiwa kufungua duka lake linaloendesha maisha yake.

“Sasa namshukuru Mungu nina sehemu yangu tofauti na mwanzo hata mteja akifika dukani kwangu anajidai amefika mahala sahihi,”anasema na kuongeza kuwa

“Pia najivunia sasa hivi kwani kupitia mtandao wangu wa kijamii wa Instagram tayari nimeongeza wafuasi tofauti na hapo awali hivyo sikosi wateja watatu kwa siku ambao wanapiga simu kutoka mtandaoni ni jambo la kujivunia kwani wapo wenzangu ambao hawapati nafsi hiyo.”

Malengo yake

Anasema malengo ya kuhakikisha anapanua wigo wa kazi yake ya ubunifu kwa kuweza kutoka nje ya Tanzania na kufuata bidhaa katika nchi nyingine.

“Ndoto yangu nikanyage China watu wanakwenda kufuata bidhaa mbalimbali na mimi niwe na uwezo huo niende kwa gharama zangu na kuhangaika kwangu,” anasema.

Mfahamu kwa ufupi

Saidi Haji Othman ni kijana wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 20 ambaye alifanikiwa kupata elimu yake ya msingi katika shule ya Ruvuma iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam na kujiunga Sekondari katika shule ya Chamazi Islamic na kidato cha nne akamalizia katika shule ya Chimbande.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post