Mshambuliaji John Bocco anatarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa na JKT Tanzania na tayari amepiga picha za utambulisho na kaingiziwa pesa zake za usajili.
Mwanaspoti imepata taarifa za ndani kutoka kwa uongozi wa timu hiyo zikieleza kwamba Bocco ndiye atakayekuwa nahodha mpya wa kikosi hicho.
Bocco amesajiliwa na JKT Tanzania kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya Simba kumpa mkono wa kwaheri, licha ya kwamba alipewa majukumu mengine ya kukinoa kikosi cha vijana wenye umri chini ya miaka 17.
Nyota huyo ameachana na Simba na kukubaliana na dili la kurudi kucheza uwanjani.
“Bocco tutampa heshima ya kuwa nahodha. Ndio maana tumemsajili kama kocha mchezaji tunaamini bado ana uwezo uwanjani. Pia ana vitu vya ziada atakavyowasaidia wenzake kuwaongoza,” amesema mmoja wa viongozi wa JKT Tanzania.
Nje na Bocco, Mwanaspoti inafahamu kwamba Said Ndemla na David Bryson baada ya kumaliza mikataba ya mkopo wamepewa mikataba mipya, hivyo wataendelea kuwa sehemu ya kikosi hicho msimu ujao.
“Ndemla na Bryson walikuwa wanacheza kwa mkopo kutoka Singida Fountain Gate kwa sasa tumewasainisha mikataba mipya kama wachezaji huru” amesema.
Leave a Reply