Miaka ya hivi karibuni imetufundisha mengi kuwa siku hizi unasaidiwa sana na rafiki kuliko ndugu uliyezaliwa naye, hii ni kutokana na kutiliana vinyongo na kutopenda mafanikio ya mtu.
Katika kazi leo nimekushushia mada ambayo itakufanya uchague kusuka ama kunyoa kutokana na marafiki ulionao either katika eneo la kazi au nyumbani kwa sababu kuna marafiki wapo kwa ajili ya kutaka ufanikiwe na wengine ambao hawataki kabisa ufanikiwe.
Na kama tunavyojua siku hizi kupata rafiki ni kawaida sana kutokana na kurahisishiwa na mitandao lakini tunarudi pale pale unaweza ukawa na namba za marafiki zaidi ya 100 lakini hakuna atakaye kusaidia kufikia malengo yako.
Mwananchi Scoop tukakutana na Shufaa Nassor Mwanzilishi wa Enliven Reusable pads anajulikana kama Madam Hedhi Salama alifunguka mawili matatu kuhusiana na marafiki ambao wamemfanya yeye kufikia malengo yake.
“Kwanza kabisa ninao marafiki ambao wapo tu siyo msaada sana kwa kunisaidia kutimiza ndoto ila ninao marafiki wachache ambao ni marafiki wa faida”
Aliendelea kwa kueleza kuwa marafiki ambao wanamsaada kwake ni wapambanaji na wenye exposure kwa jamii na malengo yao ni kila mmoja kumuona mwezie anafika pale anapotamani kufika huku nyenzo yao kubwa ya kumfanya mpaka abaki na watu hao ni kudai kuwa wanashikana mikono ili waweze kufanikiwa pamoja na kupunguza wivu baina yao.
Na mimi leo sitoishia hapo nataka kukupa siri ya urafiki na malengo, marafiki ambao watakufanya uweze kufikia malengo yako ya kufanya katika kazi zako na majukumu yako wengine ni wale ambao watakutia moyo katika kila jambo na hasa pale unapokuwa unataka kukata tamaa.
Watakao kushauri mambo mazuri siyo wale wa twende kidimbwi tuka-enjoy, watakao kuonesha fursa za mafanikio zilipo na wale tu ambao hawana kinyongo wala chuki za mafanikio yako, maana rafiki ndiyo nyoka mkubwa pindi ukimpita kimafanikio.
Ni vizuri kuwa makini sana wakati unapochagua marafiki wa kuwa nao karibu na kubadilishana mawazo kila mara, kwani ukipata rafiki mlevi kupindukia, mmbea, mtembezi, mvivu basi jua na wewe unaweza kuangukia katika vishawishi vyake. Kuna wakati utatakiwa kufanya maamuzi magumu ili kuhakikisha unafikia ndoto zako.
Hivyo basi ukiwa kazini angalia marafiki ambao wataendana na wewe katika utendaji kazi na wenye ndoto sawa za kufikia malengo, kazini siyo sehemu ya kufuata mkumbo fata kilicho kupeleka ukiona huna rafiki wa kuendana naye basi wabaki hao wa salamu basi inatosha.
Leave a Reply