Njia za kujiandaa na maisha ya kitaa toka ukiwa chuo

Njia za kujiandaa na maisha ya kitaa toka ukiwa chuo

Niaje wanangu wa vyuo mbalimbali, hii ni yenu sasa. Kama kawaida yetu katika segment ya UniCorner tumekusogezea mada ambayo kama kweli wewe una akili basi utaelewa lakini ukifuata mikumbo ya watu, basi hii mada utaiona kama ni ujinga tu na hapa wala simaanishi kuwa huna akili laaahashaa! Ila kama unahitaji kufanikiwa inabidi uanze na kujielewa kwanza.

Kama uko chuo, najua mpaka sasa ushajua au ushaona mitandaoni watu wakiongelea swala la ukosefu wa ajira, swali ni wewe unajionaje kuhusu maisha baada ya masomo? Au unasubiria na wewe kuongezeka kwenye maongezi yanayoendelea?

Kama uko chuo, najua wanafunzi wengi wanakaribia kurudi chuoni, hapa naongea na wewe unayekwenda kumaliza mwaka wako wa mwisho na wewe unaekwenda kuanza chuo yaani first year, una fursa nyingi sana za kujiandaa na kufikiria kuhusu maisha ya kitaa kabla hayajakufika kama wengine.

Njia za kuandaa mapema maisha yako kabla hujamaliza chuo

Wewe kama ni mwanafunzi wa chuo ni muhimu kujipanga na kujiandaa na maisha ya mtaani wakati ukiwa chuoni. Inabidi ukae na kufikiria kuwa ipo siku utamaliza chuo na familia yako itakuwa inakuangalia kwa ajili ya kuwasaidia maana wewe ndo utakuwa tegemeo lao.

Ukosefu wa ajira ni tatizo lililopo duniani kote na sio kwa nchi moja tu, wengi wanalalamikia ukosefu wa ajira, mwisho wa siku ni wewe ndio ujitengenezee mazingira na kujua kuwa ukihitimu maisha yatakuwaje, hapa nimekumbuka kamsemo kamoja hapa wanapenda kutumia waswahili wenzangu kuwa kuna maisha baada ya chuo hahha!

  • Kujifunza ujuzi mwingine ili ukija mtaani una cheti na ujuzi

Kila mtu anajua ujuzi ni kitu gani, sawa wewe umepata A zote katika masomo yako lakini inabidi ujifunze ujuzi wowote ambao utakuja kukuingizia pesa pale ukiwa huna kazi, mfano kwa wadada unaweza kujifunza kusuka, kupaka make-up nk na kwako wewe kaka unaweza kujifunza kupiga picha ndo ujuzi ambao vijana wengi wanatumia kupata kipato.

Haujakatazwa kusoma kitu unachopenda ila inabidi ujifunze ujuzi wowote ambao utaweza kuja kukusaidia hapo baadae, usifate mikumbo ya marafiki kwa kuogopa au kuona aibu kufanya jambo fulani kwasababu ya kuchekwa, kama hujui haya ni maisha yako, ukiyaharibu basi umeharibu mlolongo mzima wa maisha yako na familia yako.

  • Kutafuta connection na internships ukiwa chuoni

Najua lazima mkiwa chuo mtaenda kufanya field, basi pale utakapo fanyia field inabidi ujitume haswa na hata kama ukimaliza kufanya mafunzo yako basi usiache kuendelea kufanya kazi, ikiwezekana nenda kaombe kabisa, naamini hakuna ofisi ambayo itakukatalia kufanya internship. Hii itakupa urahisi ukimaliza chuo na kuja kuomba kazi na kampuni kukupatia kwa kujua mchango wako.

  • Kuanzisha biashara

Sasa hapa katika kuanzisha biashara kutakufanya uanze kusave pesa ulizonazo, kwa wale wanaopokea boom unaweza kuanzisha biashara yako ya mtaji mdogo tu kwa kuanza kuwauzia wanafunzi wenzio, pia ili kupata wateja zaidi inabidi kutumia mitandao yako ya kijamii kwa ajili ya kutangaza biashara yako kwa ajili ya kupata wateja wa ndani na nje ya chuo. Kwa mwanamke unaweza kuuza vitu vya kike mfano pochi, nguo nk na kwa mwanaume unaweza kuuza nguo za kiume kwa ajili ya kupata pesa.

Kwa hayo machache najua utakuwa umejifunza mengi wewe mwanachuo unayetarajia kuanza chuo na wewe unayekwenda kumaliza muhula wako wa masomo, anza sasa hujachelewa, soma kwa bidii na fanya mambo yako kwa matumaini na kwaajili ya familia yako. Kumbuka ipo siku utakuja kuwa baba au mama ambaye utategemewa na familia, amka sasa.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags